Tumaini Daima
Tunapofikiria kile ambacho Mwokozi ametufanyia, tunaweza kuendelea kwenda juu tukijua Yeye daima yuko pamoja nasi.
Kielelezo na Alberto Espi
Fikiria mikono yako imefungwa nyuma ya mgongo wako, miguu yako imefungwa pamoja, na kisha unatupwa kwenye bwawa lenye kina cha futi tisa! Ungefanya nini? Je, ungejitahidi kuelea na kujichosha mwenyewe, au ungebaki mtulivu na kupata njia kupitia hali hii ngumu?
Wale wanao jifunza kuwa Wanajeshi wa Majini wa Marekani wanakabiliwa na changamoto hii. Inaitwa “kuepuka kuzamishwa.” Lengo ni kuthibitisha uwezo wao wa kuendelea kuishi ndani ya maji katika hali mbalimbali. Mara wanapokuwa wamefungwa na kutumbukizwa ndani ya maji, sehemu ya majaribio inawahitaji kuzama chini ya bwawa bila kutaharuki, watumie miguu yao kujisukuma juu, kutoa uso juu ya maji, na kisha kwa haraka kuvuta pumzi kabla ya kuzama tena. Hii hurudiwa kwa muda fulani.
Wengi wetu hatutapitia mafunzo ya Uanamaji, lakini labda kuna baadhi ya mambo tunayoweza kujifunza kutoka na hilo—na labda hata kupata shukrani kubwa kwa Ajili ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake kadiri tunavyoendelea.
Mwokozi Wako Kupitia Mambo Yote
WANAMAJI hawa wanategemea mafunzo yao na hali ya kufanya hivyo kupitia majaribu haya makali—na lazima wayamalize yote peke yao. Sote tutapitia changamoto katika maisha, lakini tofauti na WANAMAJI katika mafunzo yao, sisi kamwe hatutakiwi kupitia changamoto zetu peke yetu.
Tunapofungwa na dhambi, wasiwasi, huzuni, au changamoto nyingine yoyote na kuhisi kama tunazama, tunaweza kumgeukia Yesu Kristo. Tunapohisi kama tuko chini na kamwe hatutarudi tena juu, tunaweza kukumbuka kwamba Mwokozi tayari ameshakuwepo pale, na Atatupa nguvu ya kujisukuma juu, kupumua tena, na kuendelea kusonga mbele. Pamoja Naye, daima kuna tumaini.
Yesu Kristo ni Mwokozi wako kukuokoa na dhambi na kifo. Yesu Kristo ni Mkombozi wako wakati unapokosea na unahitaji kufanywa mzima kiroho. Yesu Kristo ni Mponyaji wako kukuokoa na maumivu ya kihisia, kiroho, na wakati mwingine maumivu ya kimwili na maumivu ambayo Yeye pekee anaweza kuponya. Haya na majina mengine kwa ajili ya Yesu Kristo yanaonyesha ukweli kwamba Yeye ndiye wa kumgeukia, hususan wakati maisha yanapokuwa magumu.
Na Pasaka ikikaribia, tunasherehekea Ufufuko wa Yesu Kristo. Yu hai! Na kwa sababu Yeye yu hai, tutaishi tena na kuwa na ahadi ya uzima wa milele. Lakini kabla ya Ufufuko Wake, Mwokozi aliteseka huko Gethsemane na kufa msalabani kwa ajili yetu kwa sababu Yeye anatupenda. Yeye “alishuka chini ya vitu vyote”—akiteseka si tu kwa dhambi zetu, lakini pia akipitia kila aina ya maumivu, huzuni, mateso, na majaribu—ili aweze kujua jinsi ya kutusaidia (Mafundisho na Maagano 88:6; ona pia Alma 7:11).
Ona Tumaini Lako Kwake
Wakati Mwokozi aliposulubiwa, kila kitu kilionekana hakina tumaini. Wanafunzi wake walivunjika moyo. Walikuwa wamemfuata, walimwamini Yeye—na sasa Alikuwa ameondoka. Wakati Yesu alipolazwa kaburini, walikabiliana na huzuni na mashaka. Lakini siku tatu baadaye, siku ya Jumapili, kaburi lilikuwa tupu. Yesu Kristo alikuwa amefufuka! Kile ambacho wakati mmoja kilionekana kupotea sasa kiligeuka kuwa matumaini!
Kama vitu vinaonekana kuwa ni giza na kukatisha tamaa—kama vile umetupwa kwenye bwawa na mikono na miguu yako vikiwa vimefungwa—na hauoni njia ya kutokea, chukua muda kutafuta tumaini katika Yesu Kristo, na kumbuka bado hujafika mwisho.
Mwokozi hakufika Jumapili ile ya furaha ya Pasaka kabla ya kwanza kuvumilia maumivu ya Gethsemane na msalabani siku tatu kabla. Kwa hiyo, kama unapitia wakati mgumu, usikate tamaa! Kama Mzee Joseph B. Wirthlin (1917–2008) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alivyowahi kusema, “Katika giza la huzuni yetu, Jumapili itakuja. … Bila ya kujali huzuni yetu, Jumapili itafika.”
Kupitia dhabihu Yake ya kulipia dhambi na Ufufuko, Yesu Kristo daima yuko pale ili kukusaidia kupata amani na kusogea juu zaidi kuliko ambavyo ungeweza kutumainia.