Kila Kitu Kinafanya Vizuri Zaidi Unapomtumainia Mungu
Unapomtumainia Baba wa Mbinguni, utaweza kukabiliana na cho chote unachopitia.
Picha na Giovana Flavia de Almeida Campos
Nimekuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho tangu nilipokuwa na umri wa miaka minane. Miezi michache baada ya ubatizo wangu, mimi na familia yangu tulitangatanga mbali na Kanisa.
Miaka kadhaa baadaye, tulipoamua kuanza kurudi, janga la ulimwengu la COVID-19 lilitokea, na mikutano ya kanisa ilianza kufanyika kwa mbali. Kwa mara nyingine tena, nilijikuta nikitangatanga, nikikabiliwa na changamoto nyingi njiani.
Magumu na Mashaka
Wakati huu, nilianza kuwa na shaka juu ya ukweli wa injili, ushuhuda wangu, na Yesu Kristo alikuwa nani. Wakati mmoja, hata nilihoji kuwepo Kwake na kuanza kufikiri nilikuwa mkanamungu. Moyo wangu ulikuwa mgumu na baridi kama jiwe la barafu.
Awamu hiyo ya maisha yangu ilikuwa ngumu sana na isiyoelezeka kwa urahisi. Nafikiri ni kwa sababu tunapoacha kuamini katika Yesu Kristo na nguvu Zake, maisha yetu yanapoteza maana na kuwa yenye huzuni.
Seminari Imenibadili
Hatimaye, baba yangu alinishawishi kuanza kuhudhuria kanisani tena. Nilifanya hivi ingawa bado nilikuwa nimechanganyikiwa na mwenye kuhangaika na maswali mengi.
Siku moja kanisani, niliona bango kuhusu seminari. Hii iliwasha hamu ndani yangu. Nilimwendea askofu wangu kumuuliza kuhusu hilo. Mara moja akaniongeza kwenye kikundi cha seminari cha mazungumzo na kuniambia darasa la seminari linaanza saa 11:30 asubuhi.
Kwa hiyo, nilianza kuhudhuria seminari. Hii ilinisaidia kupata marafiki wapya na hatimaye kupata ushuhuda juu ya hili Kanisa na maandiko. Nilikuwa na mwalimu ambaye kwa kweli alihimiza darasa langu na kuleta ubora ndani yetu. Niligundua kwamba kujifunza maandiko kwa kweli kunaturuhusu kumjua Mwokozi. Kuna tofauti kati ya kusikia ushuhuda wa mtu na kutafuta ushuhuda wa kwako mwenyewe kupitia kujifunza na imani.
Jasmine pamoja na marafiki zake Victória (kushoto) na Carol (kulia). Marafiki wa Jasmine wanamsaidia kuishi injili ya Yesu Kristo.
Vidokezo 10 vya Kuwa Mwanafunzi wa Kristo
Mwanzoni, nilijua kuhusu Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kupitia kile wengine walichoniambia. Lakini hatuwezi daima kutegemea tu shuhuda za wengine. Tunahitaji kutafuta kumjua Mwokozi sisi wenyewe.
Tunahitaji kutenga muda kwa ajili ya Mwokozi na kwa ajili ya mambo matakatifu ili tuweze kuwa mmoja wa wanafunzi Wake. Nimejifunza kwamba unakuja kumjua Yeye wakati wewe:
-
Kwa makusudi unapomtafuta Yeye.
-
Unaposoma maandiko.
-
Unapojitahidi kufanya vizuri zaidi kiroho.
-
Unaposali.
-
Unapohudhuria hekaluni.
-
Unapowahudumia wengine.
-
Unapofunga.
-
Unapofuata mfano Wake.
-
Unapokuwa na moyo safi
-
Kukataa kuzungumza mabaya au umbeya kuhusu wengine.
Mambo haya yalinisaidia kumjua Mwokozi—na kuwa mmoja wa wanafunzi Wake. Kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo ni muhimu sana kwa sababu tunaweza kutumia nuru Yake ili kuwasaidia wengine. Kupitia mifano yetu mizuri, wengine wanaweza kuona injili ni baraka kiasi gani.
Kwenda kanisani na kushiriki injili na familia yake kumebariki maisha ya Jasmine katika njia nyingi.
Mambo Yatakuwa Bora Zaidi.
Niliporudi kanisani, nilikuwa nimegonga mwamba—nikiwa nimejawa na mashaka, bila marafiki, bila matumaini, bila kujua mimi nilikuwa nani hasa au kusudi langu lilikuwa nini.
Sasa, injili ni “mwale” ambao umeangaza maisha yangu na unaonisaidia kufanya mambo sahihi na kuwa mtu bora zaidi. Bila injili, sijui ningekuwa wapi.
Kila kitu kinafanya vizuri zaidi katika maisha unapomtumainia Mungu. Kutoka wakati utakapomtafuta, utaanza kupanda kutoka kwenye shimo na vitu vitaanza kufanya vizuri zaidi. Bila shaka, dhiki bado itakuja, lakini uaminifu huu na hamu ya kuamini pole pole itakuinua. Inaweza kuchukua muda, lakini mambo yatakuwa mazuri!
Unapomtumainia Baba wa Mbinguni, utaweza kukabiliana na cho chote unachopitia—iwe ni changamoto, mashaka, matatizo ya kiafya, au upweke. Kwa mfano, unaweza kupata alama nzuri kwenye mtihani, kuboresha afya yako, au kupokea majibu—wakati mwingine majibu ambayo umekuwa ukitafuta tangu ulipokuwa na umri wa miaka 10, kama ilivyokuwa kwangu—kama unamtafuta Yeye na kumtumainia Yeye.
Nina uhakika wa mambo haya. Shukrani kwa injili, ninaweza kusema kwamba nimebadilika. Kwa kweli, kila kitu kimebadilika—moyo wangu, mawazo, tabia, na kanuni. Sasa ninajua ukweli, na hiyo inaleta tofauti yote. Kila kitu kinafanya vizuri zaidi kwa sababu ya injili ya Yesu Kristo.
Mwandishi anatoka São Paulo, Brazili.