Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana
Tembea pamoja Nami
Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana Januari 2026


Dhima ya Vijana kwa Mwaka 2026

Tembea pamoja Nami

Dhima ya Vijana kwa mwaka 2026 itasaidia wewe kukumbuka kwamba unapobaki karibu na Mungu, Yeye atatembea pamoja nawe—daima.

Urais Mkuu wa Wasichana

Kutoka kushoto hadi kulia: Tamara W. Runia, Mshauri wa Kwanza; Emily Belle Freeman, Rais; na Andrea Muñoz Spannaus, Mshauri wa Pili

Hauko Peke Yako.

Je, umewahi kuombwa kufanya kitu ambacho hukufikiria kuwa hungeweza kufanya? Pengine hukujisikia mwenye nguvu vya kutosha au mwerevu vya kutosha, au una wasiwasi kwamba wengine wangekucheka na kukukosoa. Kama umewahi kuhisi hivi, hauko peke yako.

Maelfu ya miaka iliyopita, kulikuwa na mtu aliyeitwa Henoko. Mungu alimwomba Henoko ahubiri toba kwa watu—baadhi ya watu waovu zaidi ambao dunia haijawahi kuwaona.

Henoko hakufikiri kama angeweza kufanya hivyo. Alimwambia Mungu kwamba yeye alikuwa yu mdogo sana, hakuwa na marafiki wa kutosha, na hakuwa mwerevu vya kutosha (ona Musa 6:31).

Lakini Mungu alimpa Henoko ahadi. Alimwambia mtu yule aliyejawa na hofu, “Nenda ukafanye kama nilivyokuamuru wewe” na “milima itakukimbia mbele yako, na mito itageuza njia yake; nawe utakaa ndani yangu, nami ndani yako; kwa hiyo tembea pamoja nami” (Musa 6:32, 34).

“Tembea pamoja nami.” Ni mwaliko rahisi, wa kupendeza ulioje.

Mungu alimwahidi Henoko kwamba kama angekuwa jasiri vya kutosha kuanza, basi Mungu angekuwa pamoja naye kila hatua ya njia hiyo. Mungu angemfanya Henoko kuwa mkuu na kumuimarisha ili afanye zaidi na kumsaidia kuwa zaidi kuliko ambavyo angeweza kufikiria.

Moja ya majina mengi ya Mwokozi ni Emanueli, au “Mungu pamoja nasi” (Mathayo 1:23). Iko katika jina la Bwana na asili ya kutembea pamoja nasi. Chaguo ni letu—je, sisi tutatembea pamoja Naye, pia?

Siku hizi, tunamtazama Henoko kama mtu wa imani na nabii mkuu na kiongozi. Lakini kabla ya Henoko nabii, kulikuwa na kijana Henoko ambaye alijitilia shaka yeye mwenyewe lakini bado alichagua kutembea na Mungu.

Maisha yanapokuwa magumu, unapokuwa hujisikii kama unatosha, kumbuka ahadi ya Bwana kwa Henoko, na kwako wewe. Yeye atatembea pamoja na wewe, Hatakuacha peke yako, hata kwa hatua moja.

Emanueli. Mungu pamoja nasi. Mungu pamoja na wewe!

Urais Mkuu wa Wasichana

Urais Mkuu wa Wavulana

Kutoka kushoto kwenda kulia: David J. Wunderli, Mshauri wa Kwanza; Timothy L. Farnes, Rais; na Sean R. Dixon, Mshauri wa Pili

Kwa Msaada Wake, Unaweza Kufanya Mambo Yote

Kama ninyi wavulana, Bwana alimuomba Henoko kutimiza majukumu muhimu ya ukuhani. Kazi yake ilikuwa ni kuhubiri toba kwa watu waovu. Henoko alielezea mashaka yake. “[Nami] ni kijana mdogo,” yeye alisema. “Watu wote wanichukia … Mimi si mwepesi wa kusema; kwani mimi ni mtumishi wako?” Musa 6:31.

Bwana alijibu kwa nguvu na hakikisho. “Nenda na ukafanye kama nilivyokuamuru. … Fumbua kinywa chako, nacho kitajazwa … . Roho yangu i juu yako … ; milima itakukimbia mbele zako … ; kwa hiyo tembea pamoja nami” (Musa 6:32, 34).

Henoko alijifunza kwamba wakati Bwana anapotupatia kazi, hatukabiliani nayo sisi pekee yetu. Tunapofanya na kushika maagano na Kristo, tunatembea pamoja Naye na kushiriki katika nguvu Zake—tunakuwa vyombo katika mikono Yake.

Kama Henoko, una jukumu muhimu: utumishi, kuhudumu hekaluni, kusimamia sakramenti, kujifunza maandiko, kuishi viwango vya injili, kutubu, kujiandaa kwa ajili ya misheni, na zaidi. Unaweza kuhisi kuzidiwa. Unaweza kuhisi hautoshi. Hiyo ni SAWA. Siyo tu kuhusu kufanya pekee yako. Ni kuhusu kuchagua leo—siku hii na kila siku—kutembea pamoja na Mungu.

Kwa msaada Wake, unaweza kufanya mambo yote. Yeye atakuimarisha, atakusamehe, na kukuwezesha kupita uwezo wako wa asili. Yeye anakupenda! Kama Urais Mkuu wa Wavulana, tunakupendeni na tunatazamia kuungana nanyi katika kupekua dhima ya kuvutia ya mwaka huu 2026: “Tembea Pamoja Nami.”

Urais Mkuu wa Wavulana