Sauti za Waumini
Kujenga Kesho Angavu huko Mombasa
Waumini wa Kanisa huko Mombasa, Kenya wanajifunza na kustawi kupitia programu za kujitegemea.
“Wote Mombasa walimjua Dave kama ‘Mzee Nelson mjenzi’”, alisema Dada Nelson wakati yeye na mumewe walipofikia mwisho wa misioni yao ya miezi 18 huko Misioni ya Mashariki ya Kenya Nairobi, iliyoko Mombasa. Mzee na Dada Nelson walijenga zaidi ya majengo ya mbao. Walijenga ushuhuda, walijenga kujiamini, walijenga kujitegemea na usalama wa chakula, wakati walipojenga mabanda ya kufugia kuku, nyuki, madimbwi ya samaki, biashara za ushonaji na zaidi.
Walijenga kesho angavu kwa waumini wengi waliowatumikia kwa upendo. Lakini hawakufanya peke yao. Walijenga pamoja, bega kwa bega, pamoja na waumini waliojiunga na miradi yao, wakifundisha na kuwawezesha katika safari yao.
Dada Nelson, mwenye utaalamu wa uuguzi, alitumia ujuzi wake wa uuguzi katika wito wake kama muuguzi wa misioni, akiongezea pia kwenye utaalamu wake wa ushonaji kuanzisha programu ya ushonaji, kwa msaada wa Lucy, muumini wa Mombasa ambaye ana uzoefu kwenye ushonaji wa nguo za kike. Lucy aliwatumikia washiriki wenzake kama mkufunzi mkuu, akifundisha mbinu za kitaalamu za ushonaji. Programu hii haikutoa maelekezo pekee lakini, kupitia programu ya Kanisa ya msaada wa kibinadamu, pia ilitoa cherehani za kushonea ambazo washiriki walipewa ili kuanzisha biashara zao wenyewe za ushonaji.
Mshiriki mmoja wa programu alisema, “Jina langu ni Dada Susan kutoka tawi la Kenya Ukunda katika wilaya ya Mombasa. Programu ya ushonaji imekuwa baraka kubwa kwangu, kwa sababu sasa naweza kulipa zaka zangu, kulipa madeni yangu, sasa naweza kutafuta chakula, sasa naweza kushiriki ujuzi niliojifunza pamoja na kaka na dada zangu. Ninatazamia kutoshiriki ujuzi wangu pekee bali kupata ujuzi zaidi ili kwamba sote tuendelee kukua pamoja. Nina shukrani na furaha kushiriki ujuzi wangu na vyote nilivyojifunza kutoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.”
Lucy alitoa hisia sawa na hizo akisema “ninafurahi kwa fursa ya kuwa mshiriki wa mafunzo ya kujitegemea. Kwa kweli, maisha yangu yamebadilika kwa sababu natengeneza bidhaa za kuuza kwenye jamii nzima na ninaingiza kipato. Ninaweza kulipa gharama zangu na kulipa zaka. Ninaamini kwamba Baba wa Mbinguni atanibarikia zaidi katika siku zijazo na hata kuwa na biashara kubwa kwa sababu kuwa na mashine zangu mwenyewe kutaniletea fursa hizi. Nina matumaini ya kupata zaidi sasa kwa sababu nina njia ya kusonga mbele. Nitawahimiza wengine kuhudhuria madarasa ya kujitegemea ili na wao wajifunze jinsi ya kuanzisha biashara zao wenyewe. Inatupatia nguvu ya kuvuka matatizo tuliyoyapitia.”
Vivyo hivyo, mfuko wa Kanisa wa msaada wa kibinadamu hutoa njia kwa ajili ya kujitegemea kupitia miradi mingine ambayo waumini wanaweza kuchagua kuishiriki, kama wako radhi kutenga muda wao na jitihada ili kukamilisha programu hiyo.
Nelly Achieng alikuwa ni mmoja wa washiriki hawa ambaye alionyesha shukrani zake kwa msaada aliopokea akisema “nina shukrani sana kwa mradi wa kujitegemea. Ulianza kwa kuhudhuria madarasa ya kujitegemea, [kisha] kuhudhuria madarasa ya kiuongozi, . . . na baadaye [yalikuja] mafunzo ya ufugaji wa mifugo jamii ya kuku. Niliamua kushiriki ufugaji wa mifugo (kuku wa kisasa) kwa sababu niliwahi kufanya kazi kwenye duka la dawa za mifugo na hivyo nilikuwa na maarifa msingi kuhusu mifugo. Nilianza na kuku arobaini na kwa msaada wa mara kwa mara kutoka kwa Mzee na Dada Nelson, niliongeza kuku wangu hadi kufikia 350. Biashara yetu inakua vyema licha ya changamoto, lakini tunasonga. Ninajua kwamba mradi [huu] wa kujitegemea ni kitu kizuri kuwa ndani yake. Ninajua kwamba mradi huu wa kujitegemea utanisaidia vyema kukimu mahitaji yangu na yale ya familia yangu.”
Silvia Ochieng, mama wa Nelly, alishiriki uzoefu wake kwenye ufugaji wa mifugo jamii ya kuku kupitia mradi wa kujitegemea. Anasema: “Kabla ya mradi wa kujitegemea, nilikuwa na duka langu dogo la chakula..[Ilikuwa ni] changamoto, kipato ambacho ningeweza kukipata kilikuwa kidogo kuikimu familia yangu. Kitu pekee nilichojali ni kupata chakula cha siku. . . . Baada ya kuhudhuria madarasa ya kujitegemea niliandika pendekezo langu la biashara. Nilipata kuku 40 wa kwangu mwenyewe. Ee, ni baraka kiasi gani mradi huu umekuwa kwangu!
“Hapo kabla, nilihofia mara kwa mara jinsi ya kutatua mambo. Sasa, naona kuku wangu wakiwa na afya na wenye kuzaa kwa wingi, na moyo wangu umetosheka. Tumeunganisha na binti yangu na sasa tunakuza kuku 350. Tunashukuru kwa wamisionari wenza, Mzee na Dada Nelson, kwa msaada wao usio na kifani katika mradi wetu. Pia tuna shukrani kwa wataalamu wetu wa kujitegemea, Dada Georgina [Siele], ambaye ndiye aliyetupatia mafunzo. Pia tuna shukrani kwa msaada wa ziada tulioupata kutoka kwa mmoja wa rafiki zetu ambaye aliongezea mtaji kwenye akiba yetu kwa ajili ya uwekezaji wa pili wa kuku 150. Kama wanavyosema, tunahitaji kuwasaidia wengine katika kubeba mizigo yao na sasa nahisi ni mwepesi kwa sababu ya upendo usio na mwisho kutoka kwa rafiki zetu.
“Kitambo nilikuwa nikitumainia tu mazuri, lakini sasa, nahisi kama tunaiendesha kesho yetu. Biashara hii ya kuku imetupatia amani ya akili na hisia ya ufahari. Ni zaidi ya kuku; ni kesho ya familia yetu, kukua pamoja na kila kifaranga. Hatukuzi kuku tu; tunaijenga kesho yetu.
“Nimejifunza mengi, sio tu kuhusu kufuga kuku, lakini kuhusu kusimamia fedha, kuelewa mienendo ya masoko na hata kidogo kuhusu huduma kwa wateja. Mabadiliko hayakuwa bila changamoto—kulikuwa na magonjwa, panda shuka na masoko, kununua na kusomba maji zaidi kutoka kwa muuza maji, kwa kuwa hatukuwa nayo kwenye eneo letu, na kazi ngumu ya kusimamia kundi kubwa la mifugo. Lakini kila wakati tulipokumbana na kikwazo, tulikumbuka lengo na ono letu na daima kumtegemea Mwokozi.
“Mradi wa kujitegemea haukutupatia kuku tu; ulitupatia njia ya uhuru na hisia mpya ya tumaini. Ningemwalika kila mtu kushiriki katika madarasa ya kujitegemea ili waweze kupokea baraka hii ya kuongeza kipato chao na kuwa na cha kutosha kulipa zaka. Kujitegemea hakujanibariki mimi tu binafsi lakini kumewabariki pia wale wanaonizunguka.”
Pamoja na waumini huko Mombasa, akina Nelson pia wamehisi kubarikiwa na Bwana katika jitihada hizi na kutoa shukrani zao kwa uzoefu wao wote wa misioni. Dada Nelson anashiriki, “Tuna shukrani kwa fursa ya kuwafundisha, kuwaongoza na kuwahimiza wote kukuza biashara zao. Thawabu ya kweli ilikuwa ni kuona mafanikio yao, na wao hatimaye kuweza kukimu kwa ajili ya familia zao na kuwa wenye kujitegemea wakiwa na biashara inayokua, yenye mafanikio. Walijifunza kile kinachohitajika kuwa mwenye mafanikio katika jitihada zao. Wote walizungumzia umuhimu wa watoto na wajukuu wao kushuhudia mafanikio hayo kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo vitajifunza umuhimu wa kujitegema kiroho na kimwili.
“Tukiangalia nyuma katika misioni yetu, tulihisi ni faraja kuwatumikia watu wazuri wa Mombasa ambao walikuwa na imani hiyo na ustahimilivu dhidi ya vikwazo vingi—hasa kukosa kazi na [kutokuwa] na uwezo wa hata chakula juu ya meza kila siku. Tunajua kwamba Baba yetu wa Mbinguni alikuwa na mpango mkuu kwa wito wetu huko Kenya. Dave alipenda kweli mtazamo wa kujitegemea katika wito wake, na nilipenda wito wangu wa kitabibu pia. Tunawapenda Wakenya na tutawakumbuka sana tunapoondoka Afrika.”