Liahona
Kubariki Familia Zote za Duniani
Machi 2026 Liahona


“Kubariki Familia Zote za Duniani,” Liahona, Machi 2026.

Kubariki Familia Zote za Duniani

Kama tutafuata na kushiriki mpango wa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya familia, Yeye atakuwa pamoja nasi, atatusaidia, na kujiunga nasi katika safari yetu ya kurudi Kwake.

Kielelezo cha Yakobo akipata ono

Ndoto ya Yakobo akiwa Betheli, na J. Ken Spencer

Hivi karibuni, Mimi na Dada Uchtdorf tulihudhuria ubatizo wa mmoja wa wajukuu wetu. Tulipokuwa tukitazama vizazi vingi kwa shangwe wakisherehekea tukio hili, tulihisi shukrani kubwa kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya mpango Wake wa wokovu kwa ajili ya watoto Wake. Tulihisi jinsi familia na maagano matakatifu yalivyokuwa muhimu Kwake tangu mwanzoni kabisa.

Umuhimu huo unaweza kuonekana katika hadithi ya Agano la Kale ya Yakobo mwaminifu, ambaye alisafiri safari ndefu na ya kuchosha ili kupata mke, kuoa katika agano, na kuanzisha familia. Jioni moja, Yakobo alisimamisha safari yake ili kupumzika kwa usiku huo lakini akapata mawe tu kwa ajili ya mto wake. Lazima alikuwa amechoka sana kwa sababu bado aliweza kulala—na kuwa na ndoto.

Akiwa na malengo yake ya kustahili ya ndoa ya agano na familia dhahiri akilini mwake, Yakobo aliona “ngazi iliyowekwa juu ya dunia, na kilele chake kikafika mbinguni: na tazama malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu yake.

“Na, tazama, Bwana alisimama juu yake, na kusema, Mimi ndimi Bwana Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka” (Mwanzo 28:12–13).

Bwana kisha alifanya baadhi ya ahadi muhimu za agano kwa Yakobo—ahadi ambazo yeye pia alikuwa amefanya na baba yake Yakobo, Isaka, na babu yake, Ibrahimu, ikijumuisha:

  • Ahadi kwamba Yakobo atakuwa baba wa “umati wa watu” (Mwanzo 28:3; ona pia mstari wa 14).

  • Ahadi za nchi kwa ajili ya vizazi vya Yakobo (ona Mwanzo 28:4, 13).

  • Ahadi kwamba kupitia Yakobo na “uzao wake familia zote za duniani zitabarikiwa” (Mwanzo 28:14; msisitizo umeongezwa).

Tukio hili la Yakobo lilikuwa takatifu sana kiasi kwamba yeye alitamka: “Hakika Bwana yuko mahali hapa. … Hapa sio pengine ila ni nyumba ya Mungu, na hili ni lango la mbinguni” (Mwanzo 28:16–17). Na hivyo, Yakobo akapaita mahali pale Beth-el, ambapo ina maana ya “nyumba ya Mungu” (Mwanzo 28:19, tanbihi a).

Baraka zilizoahidiwa zilizotolewa katika ndoto ya Yakobo zilihitaji kwamba Yakobo afanye kupanda ngazi kitamathali katika maisha halisi. Kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, si vigumu kuona muunganiko miongoni mwa ndoto ya Yakobo, maagano ya Bwana, na nyumba ya Bwana. Mahekalu kwa sehemu kubwa ni kama ile ngazi Yakobo aliyoiona. Mafundisho, ibada, na maagano ya nyumba ya Bwana huunganisha mbingu na dunia. Maagano yangeweza kulinganishwa na vipandio kwenye ngazi ambavyo hutusogeza karibu na Bwana. Na, kupitia huduma takatifu tunazotoa katika mahekalu matakatifu, tunabariki “familia zote za duniani”—zilizopita, zilizopo, na zijazo.

Ni Ugunduzi uliyoje!”

Mzee Bruce C. Hafen, mshiriki mstaafu aliyebaki na heshima wa Sabini, wakati mmoja alipokea simu kutoka kwa mhariri wa gazeti la kitaifa. Mhariri alitaka kuzungumza kuhusu kitabu cha hivi karibuni ambacho kilitafiti historia ya imani kuhusu mbinguni katika dini mbalimbali.

“Waandishi hao waligundua kwamba umma wanahisi njaa iliyosambaa duniani kote kwa ajili ya mbinguni—na familia zilizoko mbinguni,” Mzee Hafen aliandika. Lakini japo watu wengi zaidi bado waliamini katika maisha baada ya kifo, upendo wa milele, na miunganiko ya familia mbinguni, “makanisa mengi ya Kikristo yanatoa jibu dogo kwa njaa hii ya ndani zaidi”—isipokuwa moja: Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Katika Kanisa la urejesho la Mwokozi, tunayo mahekalu matakatifu. Tuna ndoa ya milele, na mamlaka ya kuunganisha ambayo hubariki zaidi ya kifo cha kimwili. Tuna ahadi ya siku za usoni ya milele na wapendwa wetu katika uwepo wa Baba na Mwana. Kutokana na haya yote, waandishi walihitimisha kwamba dhana ya Mbinguni ya Watakatifu wa Siku za Mwisho ni kamili zaidi—na, nitaongeza, yenye furaha zaidi.

“Ni ugunduzi ulioje!” Mzee Hafen alisema. “Watu zaidi leo wanatamani familia za milele, na hii [injili ya urejesho ya Yesu Kristo inatimiza hamu hiyo vyema zaidi kuliko wazo lolote linalojulikana [au imani ya kidini]. Ningetamani ulimwengu mzima ungesikia watoto [wetu] wakiimba habari hizi njema: ‘Familia zinaweza kuwa pamoja milele.’”

Familia sio tu mpangilio rahisi wa kijamii. Wao ni mpangilio wa milele wa mbinguni. Familia ni “kitovu cha mpango wa Muumba kwa kudra ya milele ya watoto wake.” Kama Rais Russell M. Nelson alivyotufundisha: “[Bwana] aliumba dunia [ili] kwamba tuweze kupata miili ya nyama na mifupa na kuunda familia. Alianzisha Kanisa Lake ili kuziinua familia. Yeye anatoa mahekalu ili kwamba familia ziweze kuwa pamoja milele.”

Lakini maslahi yetu katika familia imara sio tu kuhusu hatima ya milele. Familia ina jukumu muhimu katika furaha yetu duniani pia. Baba yetu wa Mbinguni, ambaye anajua kikamilifu kile kinacholeta furaha sasa na milele, anawatuma watoto Wake kwa familia—wasio wakamilifu kwa kiasi wanavyoweza kuwa—na anatualika kujenga na kulea familia imara. Bila shaka “Ulemavu, kifo, au hali zingine zinaweza kulazimu mabadiliko ya mtu binafsi.” Lakini hakuna kinachoweza kuchukua nafasi ya majukumu muhimu, yaliyoteuliwa ya mume na mke, baba na mama.

Utafiti juu ya “familia za kibaiolojia za wazazi wawili” unaendelea kuonyesha kwamba familia ni muhimu katika kuhifadhi “miunganiko ya kina ya upendo na huba.” Ni ”kiatamizi cha msingi kwa ajili ya watu imara, waliorekebishwa vizuri, na wenye ufahamu wa kijamii.”

Watetezi Wenye Bidii wa Familia

Bila shaka, haipaswi kutushangaza kwamba kitu muhimu sana kwa mpango wa Mungu kingekabiliwa na upinzani. Shetani hajawahi kuwa rafiki wa familia, na juhudi zake zinakuwa za dharura zaidi “kwa sababu anajua kwamba ana muda mfupi tu” (Ufunuo 12:12). Kama Rais M. Russell Ballard (1928–2023), Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alisema, “Shetani anajua kwamba njia ya uhakika na yenye ufanisi zaidi ya kuvuruga kazi ya Bwana ni kupunguza ufanisi wa familia na utakatifu wa nyumba.”

Kujua kile tunachojua kuhusu familia ya milele ya Mungu, mpango Wake kwa ajili ya watoto Wake, na umuhimu wa milele wa uhusiano wa kifamilia, tunapaswa kuwa miongoni mwa watetezi wenye bidii zaidi duniani wa familia.

Je, ni kwa jinsi gani tutafanya hili?

Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alitoa ushauri huu: “Tangazo kwa familia … ni msisitizo wa Bwana wa kweli za injili tunazohitaji ili kutuhimili kupitia changamoto za sasa kwa familia.”

Katika maisha yetu binafsi, tunaweza kufanya “vitu vidogo na rahisi” (Alma 37:6) ambavyo vinaimarisha uhusiano wa kifamilia. Hii inajumuisha kufuata kanuni za familia na ndoa zenye mafanikio zilizoainishwa katika tangazo la familia: “imani, sala, toba, msamaha, heshima, upendo, huruma, kazi, na shughuli za burudani zenye kuleta siha.” Bila kujali hali ya sasa ya familia yetu, tunaweza kuonyesha kwa matendo yetu kwamba mahusiano ya kifamilia ni muhimu milele kwetu.

Kama “wananchi wenye kuwajibika” katika jamii zetu, tunaweza “kukuza hatua hizo zilizokusudiwa kudumisha na kuimarisha familia.”

Sisi ni watu wa Bwana wa agano wa siku za mwisho. Sisi ni warithi wa ahadi zilizofanywa kwa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo—ahadi ambazo zina kila kitu kinachohusiana na familia. Ahadi zile huja na wito mtakatifu wa kubariki “familia zote za duniani.” Na njia moja muhimu tunayofanya ni kwa kuishi, kulinda, na kushiriki ukweli wa milele kwamba “familia imeamriwa na Mungu” na kwamba “ibada na maagano yaliyomo katika mahekalu matakatifu yanafanya iwezekane kwa wanadamu kurudi kwenye uwepo wa Mungu na kwa aji li ya familia kuunganishwa milele.”

“Mimi Niko Pamoja Nawe”

Wakati Mimi na Dada Uchtdorf tunapowaangalia wanafamilia wetu wakifanya maagano matakatifu na Baba yetu wa milele wa Mbinguni mwenye upendo, mioyo yetu inajawa na furaha na shukrani. Hatufurahii tu watoto wetu na watoto wao bali pia katika wazazi wetu na wazazi wao. Tunatafakari kwa upendo mkubwa jinsi maagano ya injili yanavyotuunganisha kupitia vizazi vyote. Ni tukio lisilo na mfano kuona “ngazi iliyowekwa juu ya dunia, … kilele chake [kikifika] mbinguni: na tazama malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu yake” (Mwanzo 28:12).

Baraka ambazo Bwana alimuahidi Yakobo katika ndoto yake zinaenea kwa watoto Wake wote wa agano—ikijumuisha wewe na mimi. Kama Bwana alivyofanya kwa Yakobo, atatujibu sisi “katika ile siku ya dhiki [yetu]” (Mwanzo 35:3) kama tutamchagua Yeye.

“Tazama,” Bwana alisema, “Mimi nipo pamoja nawe, na nitakuweka mahali popote uendapo, … kwa maana sitakuacha” (Mwanzo 28:15).

Kama Yakobo, sote tuna nyika ya kuvuka. Wakati mwingine baraka zilizoahidiwa huonekana kuwa mbali sana. Wakati matatizo makubwa au changamoto zinapokuja, tunaweza kutilia shaka upendo wa Bwana. Tunaweza hata kuhisi kwamba Mungu ametuacha. Licha ya juhudi zetu bora katika ufuasi, tunaweza kuhisi hatupokei baraka tulizokuwa tunazitumainia.

Akina kaka na akina dada, marafiki wapendwa, njia ya agano ni njia ya furaha, ingawa wakati mwingine inaweza kuchafuliwa na machozi. Ikiwa unahisi kwamba sehemu za mpango wa furaha hazijatimizwa katika maisha yako sasa, tafadhali amini kwamba Bwana anakujali na atakubariki katika wakati Wake, kulingana na hekima Yake.

Imani katika Yesu Kristo na ahadi Zake inatutia msukumo kutazama mbele, siyo nyuma. Kwa sababu Yake, siku zetu za baadaye hazihitaji kuwekwa mateka na kitu chochote ambacho kimetokea zamani au kinazuia mtazamo wetu sasa hivi. Ndiyo, sisi sote tuko, au tutakuwa, tumejeruhiwa kwa njia moja au nyingine. Lakini tunaamini katika Mponyaji Mkuu. Tunamwamini Yeye—sana, kwa kweli, kwamba tunakumbatia ahadi Zake, kikamilifu “tunashawishika nazo,” hata wakati bado “ziko mbali” (Waebrania 11:13).

“Sote tukumbushwe kwamba, katika njia na wakati wa Bwana mwenyewe, hakuna baraka zitakazozuiliwa kutoka kwa Watakatifu Wake waaminifu,” alisema Rais Nelson. “Bwana atahukumu na kumzawadia kila mtu kulingana na hamu ya moyoni pamoja na matendo yake.”

Ninaahidi kwamba tunapofuata na kushiriki mpango wa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya familia, Yeye atakuwa pamoja nasi, kutusaidia, na kujiunga nasi katika safari yetu. Kamwe hatatuacha peke yetu, hasa wakati majaribu yanapokuja kwetu au kwa wapendwa wetu. Atatubeba, atatuinua, na kutuleta kwenye nchi ya ahadi ya utimilifu wa shangwe pamoja Naye, pamoja na Mwanawe, Yesu Kristo, na familia zetu—milele.