“Katika Jukumu Lake,” Liahona, Machi 2026.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Katika Jukumu Lake
Sikujua jinsi ya kuiambia familia kwamba binti yao amefariki mpaka Roho Mtakatifu aliponisaidia.
Kielelezo na Briana Kranz
Ikiwa uzoefu wa binadamu wa kusikitisha zaidi ni kuvumilia janga, upotevu usiotarajiwa wa mpendwa, nadhani uzoefu wa pili mgumu zaidi unaweza kutokea ni wakati mtoa taarifa anapotazama machoni mwa mama na baba na kuwaambia mtoto wao amefariki.
Asubuhi moja nilipelekwa kuijulisha familia kwamba binti yao mdogo alikuwa amefariki wakati akiendesha gari kurudi nyumbani kutoka chuo. Alipitiwa na usingizi akiwa kwenye usukani na kufa papo hapo wakati gari lake lilipotoka barabarani na kuanguka vibaya sana. Ilikuwa asubuhi ya Pasaka.
Niliogopa sana kwa uchungu niliokuwa karibu kuusababisha kwa familia hii. Kwa njia isiyo ya kawaida, nilihisi kwamba kwa kuitaarifu familia hii, kwa namna fulani mimi nilijihisi kuwawajibika.
Nilipiga kengele ya mlangoni, na mtu alikuja. Macho yetu yalikutana kupitia dirisha la mlangoni. Aliganda, mkazo ukioneshwa usoni mwake. Alijua kwamba uwepo wangu ulielezea kutokuwepo kwa binti yake. Ghafla, nilipokea msukumo wa kiroho:
“Jason, jisahau mwenyewe. Uko katika jukumu langu na unayo haki ya nguvu zangu. Itumie. Iamini. Roho Mtakatifu atakuongoza kuleta uelewa na hali ya ushupavu kwa wale ambao hawakubaliani na hili au wamechanganyikiwa.”
Mtu huyo alifungua mlango kwa mshiko wa kutetemeka. Kujiamini kiroho kulibadilisha kusita kwangu nilipojitambulisha na kuomba kuingia ndani. Ingawa niliimarishwa na Roho, moyo wangu uliumia kwa kina kwa ajili yake. Nilitaka kushiriki katika huzuni yake, kuomboleza pamoja naye, na kulia pamoja naye (ona Mosia 18:8–9), nikihisi kwamba kufanya hivyo kungepunguza mateso yake.
Tulitembea kwenye ukumbi mfupi hadi kwenye chumba ambapo mkewe na watoto walikuwa wamekusanyika. Nikiwa na utegemezi wa Roho Mtakatifu, nilihisi kujiamini na uwazi wa akili. Nilijibu maswali yao na kisha nikatoa ushuhuda wangu kwamba kwa sababu ya Yesu Kristo, dhabihu Yake na Ufufuko, wangemwona tena binti yao.
Kupitia uzoefu huu, imani yangu katika Bwana ilibadilika kuwa tumaini. Nilitumaini kwamba imani yao pia ilibadilika.
Mzee Paul B. Pieper wa Sabini alifundisha, “Nyakati zingine njia iliyo bora ili kujifunza kumjua Mungu ni kumwamini tu Yeye.”
Kumwamini Bwana kumenisaidia kuwa na nguvu za kuwasaidia wengine. Pia kumeimarisha ushuhuda wangu na kuweka njia ya fursa zisizo hesabika za kuwahudumia wengine kwa niaba Yake.