Liahona
Tazama, Mimi Hapa
Machi 2026 Liahona


Njoo, Unifuate

Mwanzo 22:1-18

Tazama, Mimi Hapa

Na daima tumjibu Bwana kama Ibrahimu alivyofanya.

kielelezo cha Ibrahimu akimkumbatia Isaka

Kielelezo na Julia Yellow

Joseph Smith wakati mmoja alisema, “Bwana anapoamuru, tenda.” Onyesho hili la imani na matendo huleta uzoefu mwingine, sawa na huo kwenye akili yangu.

Kwa mfano, wakati Adamu alipoulizwa kwa nini alikuwa akitoa dhabihu, jibu lake lilikuwa kwamba hakujua lakini kwamba alijua ni nani aliyemwamuru (ona Musa 5:6). Pia ninakumbushwa utayari wa Lehi kuacha nyuma nyumba yake na mali yake kufuata maelekezo ya Bwana (ona 1 Nefi 2:2–4) au imani ya Nefi katika kukubali kurudi ili kupata mabamba (ona 1 Nefi 3–4).

Ningeweza kunukuu mifano mingi ya wazi katika maandiko ambayo inaakisi roho ya utiifu, lakini ningependa kufokasi kwenye uzoefu wa Ibrahimu.

Utii wa Ibrahimu

Bwana aliahidi uzao mkubwa kwa Ibrahimu na Sara. Baraka hiyo ilichukua muda mrefu kuwasili, au, badala yake, ilipokelewa katika wakati wa Bwana. Hata hivyo, Bwana aliweka imani ya Ibrahimu kwenye majaribu wakati alipomwomba kumtoa dhabihu mwanawe, Isaka, ambaye alikuwa baraka ambayo walikuwa wameiomba na walikuwa wamesubiri kwa muda mrefu. Yawezekana kuwa tumesoma maelezo haya ya maandiko mara nyingi, lakini ni mara ngapi tumejiweka wenyewe katika viatu vya Ibrahimu?

Ni vigumu hata kufikiria hisia njema za baba kabla ya jukumu kama hilo. Hata hivyo, azimio la Ibrahimu katika kuamua kutii kamwe halikomi kunishangaza alipokuwa akijiandaa kwenda mlimani huko Moria na kutoa dhabihu iliyoombwa. Katika onyesho la utayari na utiifu kwa mapenzi ya Baba wa Mbinguni, jibu lake daima lilibaki, “Tazama, nipo hapa.” (Ona Mwanzo 22:1–2.)

Kama malipo kwa ajili ya utii wake, alibarikiwa kwa kuhifadhiwa kwa maisha ya Isaka, pamoja na baraka kuu na zisizo na mwisho kwa ajili yake mwenyewe, kwa Sara, na kwa vizazi vyao (ona Mwanzo 22:15–18).

kielelezo cha kondoo mdogo

Kukubali kwa Mwokozi

Bila shaka, mfano mkuu wa utiifu na unyenyekevu kwa Baba wa Mbinguni kitovu chake ni Mwokozi, Yesu Kristo. Alionyesha utayari Wake wa kutii kwa kuja kwenye dunia hii; kwa kubatizwa, kuwa msafi na mkamilifu; na kwa kutoa uhai Wake kama matoleo na kujichukulia juu Yake maumivu, mateso, unyonge, dhambi na mauti ya watu Wake, ili ajue jinsi ya kutusaidia katika mwili (ona Alma 7:11–13).

Kwa hivyo uzoefu ulikuwa mchungu kwamba, kwa muda mfupi, ulimfanya Yeye kuuliza kama kulikuwa na njia yoyote ya kuruhusu kikombe hicho kichungu kimpite. Kisha mara moja akasema, “Hata hivyo, si mapenzi yangu, bali yako yatendeke” (Luka 22:42)—kwa maneno mengine, “Tazama, mimi hapa”—kwa hiyo kuonyesha utayari Wake wa kufanya mapenzi ya Baba.

Utiifu na Upendo

Ni kwa jinsi gani tunaweza kukuza utayari huo wa kutoa “Tazama, mimi hapa” katika kujibu kila ombi ambalo Baba wa Mbinguni hutufanya sisi kama waumini wa Kanisa, au wakati mwingine katika ngazi binafsi?

Paulo aliwafundisha Warumi, “Upendo ni kutimiza sheria” (Warumi 13:10). Kama ningetaka kupata neno lililo na maana sawa ambalo lingechukua nafasi ya kishazi “kutimiza sheria,” nafikiri neno utiifu kwa haraka lingekuja akilini. Hivyo, tunaweza kusema kwamba upendo ni utiifu. Na kwa hiyo kauli ya Mwokozi “Mkinipenda, mtazishika amri zangu” (Yohana 14:15) inaleta maana kubwa.

Tungeweza kujibu “Tazama, mimi hapa” au, katika maneno ya Nefi, “Nitakwenda na kutenda” (1 Nefi 3:7). Katika lahaja yetu ya kisasa, tungesema, “Bila shaka niko tayari kufanya kile Baba wa Mbinguni anachoamuru, bila kujali hali.”

Hata hivyo, kile ambacho ningependa kusisitiza, ni uhusiano wa utiifu wa upendo, ikimaanisha kwamba tunamtii Baba kwa sababu tunampenda Yeye. Ninaamini kwamba kuchagua kutii ni mojawapo ya njia bora za kutamka wazi upendo wetu Kwake. “Imani pasipo matendo imekufa” (Yakobo 2:26), na mimi binafsi sifikiri upendo kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo pasipo utiifu kuwa ni jambo hai.

Jinsi ya Kuongeza Upendo Wetu na Utiifu

Ni kwa jinsi gani tunaongeza upendo wetu Kwake na utiifu wetu Kwake? Mwokozi alisema, “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yohana 17:3). Kumjua Yesu Kristo—na, kupitia Kwake, Baba—hutuwezesha kujua upendo ambao Wanao kwa ajili yetu na mambo yasiyoelezeka ambayo wamefanya na bado watafanya kwa ajili yetu ikijumuisha wakati wa nyakati ngumu ambazo tunapitia katika maisha haya ya duniani. Kujua juu Yao kunabadilisha mioyo yetu, kutufanya kuwa na hamu ya kufuata mifano Yao katika matendo yetu na kuwa tayari kusema, kwa maneno na matendo, “Tazama, mimi hapa.” Utayari huu unaakisiwa katika hamu ya kusoma maandiko au katika kumtaja Baba wa Mbinguni katika sala.

“Tazama, mimi hapa” inaweza kuwa jibu kwa wito wa kuhudumu misheni au kuwekwa wakfu zaidi katika kutii amri kama vile kuishika kitakatifu siku ya Sabato, kuwaheshimu wazazi wetu, au kutafuta kuishi maisha safi ya kimaadili. “Tazama, mimi hapa” ni onyesho ambalo daima huambatana na wanafunzi wa Kristo, hata wakati dhabihu iliyoombwa inaathiri kile ambacho tunatamani zaidi au ambacho tumelipa gharama kubwa.

Utayari huu wa kutii ni wa thamani sana, hasa kuhusu maagano tuliyofanya wakati tulipobatizwa au kuingia hekaluni. Je, unaweza kufikiria maisha yetu yangekuwaje kama daima tungefikiria, “Tazama, mimi hapa” wakati tukijichukulia juu yetu jina la Kristo au ili kumkumbuka Yeye daima na kutii amri Zake? Kushiriki sakramenti kunatualika kufanya upya ahadi hiyo, ambayo inapaswa kuakisi katika matendo yetu katikati ya wiki. Vivyo hivyo hutumika tunapokwenda hekaluni tunapofanya au kukumbuka maagano tunayofanya huko.

Mfano wa Mke wa Kijana Mmoja

Ninakumbuka mazungumzo niliyokuwa nayo na wanandoa wapya miaka mingi iliyopita wakati nikihudumu kama askofu. Usiku mmoja, walikuwa na mjadala mrefu, wenye joto kuhusu malipo ya zaka. Mume kijana alikuwa amepitia wiki ngumu kazini na alitaka kuweka akiba fedha alizopata kwa ajili ya baadhi ya matumizi yao binafsi. Hata hivyo, nakumbuka maneno ya mke kijana wakati, mbele ya mumewe, alisema, “Askofu, niko tayari kutofanya matumizi hayo na hata kuacha kula, ikibidi, lakini ninataka kulipa zaka na kumtii Bwana.”

Jambo kuu ni kwamba “Tazama, mimi hapa,” ikielezwa kwa ushuhuda mkubwa kama huo na mke kijana, kiasi kwamba mume na mimi tulihisi roho yenye nguvu wakati wa mazungumzo. Mwishowe, sijui kama ilikuwa ni kwa hamu yake mwenyewe au kwa sababu alishawishiwa na mkewe, lakini mume aliishia kulipa zaka yake mwishoni mwa wiki ile.

Jumapili iliyofuata, kabla ya mikutano, mume kijana aliomba neno la haraka pamoja nami. Pamoja na uso ambao ulikuwa tofauti na wiki iliyopita, aliniambia, “Askofu, unajua kwamba wiki iliyopita mimi nililipa zaka yangu, na niliogopa kwamba nisingekuwa na pesa ya kutosha kwa ajili ya chakula, lakini nataka tu ujue kwamba wiki hii tulikuwa na mara mbili ya kiasi cha pesa kwa ajili ya chakula tunachokuwa nacho kwa kawaida. Askofu, ilikuwa muujiza, na ninataka daima kuona miujiza hiyo katika maisha yangu.” Kwangu mimi, ilikuwa kama yule kijana alikuwa akiniambia, “Askofu, niko tayari kujibu ‘Tazama, mimi hapa’ kwa chochote Mungu atakachotaka.”

Ahadi Yetu

Bwana amesema kwamba analazimika tunapofanya kile anachoomba ( ona Mafundisho na Maagano 82:10). Je, tunaamini kwa hakika katika ahadi hiyo?

Pengine baraka haziji katika wakati wetu au jinsi tunavyotaka, lakini ninashuhudia kwenu kwamba ahadi ni halisi na ya kweli. Inadai upendo Kwake, kutii, hamu ya kufanya mapenzi Yake, na kuishi kama wanafunzi wa Kristo. Yeye atatusaidia na kutubariki ili kuelewa na kushika maagano yetu. Kwa njia hiyo, anapotutaka kufanya mapenzi Yake, na tujibu kwa sauti yenye mwangwi “Tazama, mimi hapa, Bwana!”

Muhtasari

  1. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 160