Liahona
Nyumba ya Bwana: Mahala Petu pa Sala. Kuabudu na Ufunuo
Machi 2026 Liahona


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Nyumba ya Bwana: Mahala Petu pa Sala. Kuabudu na Ufunuo

Baba Yeu wa Mbinguni anatupenda na kutujali sote. Anataka kila mmoja wetu arejee salama Kwake, awe na aina ya maisha aliyonayo Yeye, yanayojulikana kama uzima wa milele, kipawa ambacho ni kikuu katika vipawa anavyoweza kuvitoa (ona Mafundisho na Maagano 14:7). Alifunua mapenzi Yake kwetu kama vile alivyomfunza Musa “Tazama, hii ni kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu’’ (Musa 1:39), na Yeye ametayarisha njia kwa ajili yetu tupokee baraka hizi katika masha yetu.

Njia yetu ya kurejea Kwake salama na kwa mafanikio ni kuwa watiifu kwa sheria na ibada za injili ya Yesu Kristo. Wale wanaoishi kanuni hizi huwa wana na mabinti wa Mungu na wanafunzi wa Yesu Kristo (ona 3 Nefi 9:17).

Wakati mtu anapochagua kubatizwa na kuingia kwenye njia ya agano, anaunganishwa na Mungu katika uhusiano maalum, akiwa na ufikiaji kwenye upendo Wake wa agano.

Nyumba ya Bwana

Kamwe sitasahau uzoefu wangu binafsi nikiwa mtoto, jinsi daima nilivyokuwa na furaha na shauku wakati ambapo viongozi wangu na walimu wa Darasa la Watoto walipotufunza juu ya hekalu kupitia muziki (ona Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 95,), walitusimulia hadithi na kutuonesha picha za nyumba ya Bwana. Walitualika tuifanye nyumba ya Bwana iwe nyumba yetu, mahala petu pa kuabudu na kipaumbele chetu. Nilijifunza pia masomo haya nyumbani kwetu wakati wa kipindi cha kujifunza maandiko kama familia na jioni ya familia nyumbani.

Kama mtoto, nilielewa nyumba ya Bwana ilimaanisha nini lakini sikuelewa kikamilifu sababu ya nyumba ya Bwana katika maisha yangu. Sasa ninaelewa sababu na kwa nini lazima niabudu mara kwa mara ndani ya hekalu kadiri ninavyoifanya nyumba ya Bwana mahala pangu pa sala, kuabudu na ufunuo.

Kupitia ibada na maagano yanayofanywa katika jina la Yesu Kristo ndani ya nyumba Yake, Baba yetu wa Mbinguni hutoa ufikiaji mkubwa kwenye nguvu Yake pale tunapofanya na kushika maagano yetu na Yeye.

Sote tunahitaji zawadi hii ya nguvu Yake katika maisha yetu kama wanafunzi wa Yesu Kristo. Nguvu hii huleta ulinzi, uponyaji, faraja, hakikisho, mwongozo wakati tunapopaswa kufanya maamuzi muhimu, uponyaji na uwezo pale tunapokabiliana na changamoto za maisha haya ya duniani na mtazamo wa milele wa utambulisho wetu wa kweli na uwezekano wa kurudi na kuishi tena na Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye, Yesu Kristo.

Tunajifunza katika maandiko kwamba katika siku za mwisho, “vitu vyote vitakuwa katika vurugu” na “hofu itakuja juu ya watu wote” (Mafundisho na Maagano 88:91). Mkanganyiko utatawala. Ulimwengu hakika upo kwenye taharuki, na kuna hofu na vivuruga mawazo kote kutuzunguka.

Watu wa Agano

Licha ya kile kinachotukia ulimwenguni, Bwana aliahidi kwamba kutakuwepo watu wa agano, watu wanaosubiri kwa ari kurudi Kwake, watu wanaosimama mahali patakatifu na hawaondoshwi (ona Mafundisho na Maagano 87:8). Watu wake wenye haki hukataa uongo wote wa adui na kusonga mbele wakiwa imara katika Kristo, “wakiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini kwa Mungu na wanadamu wote” (2 Nefi 31:20). Watu wake wa agano hufikiria selestia, hushiriki katika kazi ya wokovu na kuinuliwa na hujitayarisha kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Mwokozi Yesu Kristo.

Kama wanafunzi wa Yesu Kristo, hatupaswi kuogopa na kuvurugwa umakini. Azimio letu la kushika maagano yetu halipaswi kutegemea vitu fulani au kubadilika kulingana na hali za maisha yetu.

Je, tunapaswa kufanya nini ili kustahili na kupokea zawadi hii ya nguvu ya Mungu na Mwanaye, Yesu Kristo, katika maisha yetu?

Tunajifunza katika makala ya nne ya imani kwamba “kanuni na ibada za kwanza za Injili ni: kwanza, Imani katika Bwana Yesu Kristo; pili, Toba; tatu, Ubatizo kwa kuzamishwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi; nne, Kuwekewa mikono kwa ajili ya kipawa cha Roho Mtakatifu.”

Kufuatia azimio letu la kujitahidi kuishi kulingana na kanuni na kupokea ibada hizi za injili ya Yesu Kristo, tunapaswa kuvumilia hadi mwisho, tukiendelea kuilisha imani yetu katika Yesu Kristo pale tunaposali na kujifunza maandiko kila siku, kutubu kila siku, kupokea sakramenti kila wiki, kubeba jukumu la ushuhuda wetu wenyewe, kulipa zaka zetu, kutii neno la hekima, kutii sheria ya usafi wa kimwili, kuwahudumia wengine, kutumikia Kanisani na kustahili kwa ajili ya kibali cha hekaluni ili kufanya maagano ya ziada ndani ya nyumba ya Mungu. Maagano haya ya ziada hufanywa pale tunapopokea endaumenti yetu na kuunganishwa kama mume na mke na kama familia ya milele.

Endaumenti ya Hekaluni

“Ibada ya endaumenti hujumuisha majukumu kadhaa upande wa mtu binafsi, kama vile agano na ahadi ya kutii sheria ya wema na usafi wa kimwili kikamilifu, kuwa mwenye hisani, mkarimu, mvumilivu na safi; kujitolea vyote, talanta na mali kwenye kueneza ukweli na kuinua mbari; kuendeleza kujitolea kwenye kusudi la ukweli na kutafuta katika kila njia kuchangia kwenye matayarisho makuu, kwamba dunia iweze kutayarishwa kumpokea Mfalme wake—Bwana Yesu Kristo. Kwa ufanyaji wa kila agano na ubebaji wa kila jukumu, baraka zilizoahidiwa hutamkwa, kutegemeana na kutii masharti kwa uaminifu.”

Uamuzi wa kupokea endaumenti ni binafsi na unapaswa kufanywa kwa sala. Endaumenti ni baraka ya nguvu na ufunuo kwa wote wanaojitayarisha kuipokea. Ili kupokea endaumenti yetu wenyewe, tunapaswa kukidhi vigezo vyote vifuatavyo:

  1. Kuwa na kibali hai cha hekaluni.

  2. Kuwa na angalau miaka 18.

  3. Umemaliza au hauhudhurii tena shule ya upili, shule ya sekondari, au elimu sawa na hiyo.

  4. Mwaka mmoja umepita tangu ubatizo na uthibitisho.

  5. Una tamanio la kupokea na kuheshimu maagano matakatifu ya hekaluni kwa maisha yako yote.

Kuunganishwa kwa ajili ya Milele Yote

Baada ya kupokea endaumenti yako mwenyewe, unaweza kuungana na mwenza wako na kuunganishwa katika ndoa ya milele. Bwana ametamka, “Maagano yote, mikataba, mapatano, ahadi, viapo, nadhiri, utendaji, mahusiano, ushirika, au matarajio, ambayo hayakufanyika na kuingizwa ndani na kufungwa na yule Roho Mtakatifu wa ahadi, na yule aliyepakwa mafuta, kwa muda na vile vile kwa milele yote, . . . hayataleta matokeo yanayofaa, uwezo, au nguvu katika ufufuko na baada ya ufufuko kutoka kwa wafu; kwani mikataba yote ile isiyofanywa kwa madhumuni haya inakoma watu wanapokufa” (Mafundisho na Maagano 132:7).

Sasa, kuhusu uhusiano wetu wa milele katika ndoa ya hekaluni, Rais Ezra Taft Benson (1899–1994) ametufunza: “Familia [ni] kitengo muhimu sana katika maisha haya na milele yote; . . . utunzaji wa maisha ya familia sasa na milele huchukua kipaumbele juu ya mapendeleo mengine yote. . . . Kwa sababu ya ujasiri huu katika mwendelezo wa nyumba na familia kwenye umilele, tunajenga majengo yetu makini na yenye gharama kubwa—mahekalu ya Mungu … ili kwamba mwanamume, mwanamke na watoto wao waweze kuunganishwa pamoja kwa agano katika muunganiko wa milele ambao utaenda zaidi ya vikwazo vyote vya maisha haya ya duniani.”

Katika mkutano mkuu wa Oktoba 20921 Rais Russell M. Nelson (1924–2025) alifundisha:

“Kama ingewezekana mimi kuzungumza na kila kijana mkubwa mmoja mmoja, ningewasihi mtafute mwenza ambaye mnaweza kuunganishwa naye hekaluni. Mnaweza kujiuliza hii italeta tofauti ipi katika maisha yenu. Ninawaahidi italeta tofauti yote! Mnapofunga ndoa hekaluni na kurudi mara kwa mara, mtaimarishwa na kuongozwa katika maamuzi yenu.

“Kama ningeweza kuzungumza na kila mume na mke ambao bado hawajaunganishwa hekaluni, ningewasihi mchukue hatua muhimu ili kupokea ibada hiyo ya juu, ya kubadili maisha. Je, italeta tofauti? Ikiwa tu mnataka kupiga hatua milele na kuwa pamoja milele. Kutamani kuwa pamoja milele hakutafanikisha hilo. Hakuna sherehe au mkataba mwingine wowote unaoweza kufanikisha hilo.

“Kama ningeweza kuzungumza na kila mwanamume au mwanamke anayetamani ndoa lakini hajampata mwenza wake wa milele, ningekuhimiza usisubiri hadi ndoa ili upokee endaumenti ndani ya nyumba ya Bwana. Anza sasa kujifunza na kupata uzoefu wa kile inachomaanisha kukingwa na nguvu za ukuhani.

“Na kwa kila mmoja wenu ambaye amefanya maagano hekaluni, ninakusihi utafute—kwa sala na bila kukoma—kuelewa maagano na ibada za hekaluni. Milango ya kiroho itafunguka. Utajifunza jinsi ya kutenganisha pazia kati ya mbingu na nchi, jinsi ya kuwaomba malaika wa Mungu wakuhudumie na jinsi bora ya kupokea mwongozo kutoka mbinguni. Juhudi zako za dhati za kufanya hivyo zitachochea na kuimarisha msingi wako wa kiroho.”

Na tujitayarishe wenyewe kwa ajili ya baraka za nyumba ya Bwana. Kupokea baraka hizi si kisanduku cha kuweka vema au jambo la mara moja.

Rais Nelson pia alifunza: “Ikiwa bado hupendi kuhudhuria hekaluni, nenda mara nyingi—si mara chache. Mruhusu Bwana, kupitia Roho Wake, akufunze na kukupa uvuvio huko. Ninakuahidi kwamba baada ya muda, hekalu litakuwa mahala pa usalama, faraja na ufunuo.”

Kama vile Isaya alivyofunza, mimi pia ninawaalika nikisema: Njoni twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo (ona Isaya 2:2–3) na tuifanye nyumba ya Bwana iwe nyumba yetu, mahala petu pa sala na kuabudu.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, ninawasihi, ikiwa unaweza na bado hujaongeza uhudhuriaji wako hekaluni, tafadhali tafuta muda zaidi wa kuabudu mara kwa mara ndani ya nyumba ya Bwana. “Mara kwa mara” humaanisha mara nyingi kadiri muda wako unavyoruhusu. Fanya hilo liwe kipaumbele.

Ninakuahidi unapokuja kwa kustahili kwenye nyumba Yake takatifu, utakingwa kwa nguvu Zake, jina Lake litakuwa juu yako, malaika Wake watakuhudumia na utakua katika baraka ya Roho Mtakatifu (ona Mafundisho na Maagano 109:15).

Tanbihi

  1. Ona Russell M. Nelson, “Agano la Milele,” Liahona, Okt. 2022.

  2. James E. Talmage, The House of the Lord (1976), 84.

  3. “America’s Strength—The Family,” maandishi ambayo hayajachapishwa ya hotuba iliyotolewa kama sehenu ya Programu ya National Family Night Seatle World’s Fair Coliseum, 23 Nov. 1976, uk. 5.

  4. Russell M. Nelson, “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” Liahona, Nov. 2021.

  5. Russell M. Nelson, “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” Liahona, Nov. 2021.