Liahona
Elder Rasband Arrives in Nairobi Bringing Aid for “Mully Children’s Family”
Machi 2026 Liahona


Kurasa za Karibu

Mzee Rasband Anawasili Nairobi Akileta Msaada kwa ajili ya “Familia ya Watoto wa Mully”

Mnamo Oktoba 23, 2025, Mzee Ronald A. Rasband, wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, pamoja na mke wake Melanie na mjukuu Hudson Werlich, walifika Nairobi Kenya, baada ya safari ndefu kutoka jiji la Salt Lake, Utah, Marekani. Siku iliyofuata, Mzee Rasband alipanga kutimiza ndoto aliyokuwa nayo tangu alipokutana na Dkt. Charles Mulli, mwanzilishi mwenza pamoja na mkewe Esther, wa Taasisi ya Familia ya Watoto ya Mully. Ndoto hii, alipokuwa anaelezea akimzungumzia Dkt. Mulli ni “kwamba kanisa letu na taasisi yako vitakuwa na mwendelezo wa kazi nzuri unayoifanya ili kubariki maisha ya watoto.”

Mzee Rasband kwanza alikutana na Dkt. Mulli huko Jijini Salt Lake ambako Dkt. Mulli alikuwa mgeni mwalikwa wa tamasha la mwaka la Krismasi la 2024 la Kwaya ya Tabernacle katika Temple Square. Kama sehemu ya programu ya Krismasi hadithi ya Dkt. Mulli ilisimuliwa, ikiongelea kutelekezwa kwake katika umri mdogo wa miaka sita, maisha yake kama mtoto asiye na makazi, uzoefu wake wa kupata ushuhuda wa Yesu Kristo, na kuinuka kwake taratibu kuwa mtendaji mkuu wa kimataifa wa biashara, kiongozi wa kijamii na waziri katika nchi yake.

Kufuatia mafanikio haya makubwa, hadithi yake kwa haraka ilibadilika tena alipofanya uamuzi wa kuuza biashara yake na kuyakita maisha yake katika kuokoa watoto waliokuwa wapweke na wanaoteseka, kama yeye alivyoteseka.

Licha ya kuwa na watoto nane wa kwao wenyewe, Dkt. na Esther Mulli, hawakufungua tu makazi yao, lakini walikwenda kwenye mitaa ya Nairobi na kupata watoto yatima na waliotelekezwa ambao waliwaleta kwenye makazi yao, kuwajali, kuwaelimisha na kuwafanya sehemu ya familia yao. Hivyo ikaanza Taasisi ya Familia ya Watoto wa Mully Mully Children’s Family—Saving Childrens Lives, ambayo kwa sasa imesaidia zaidi ya watoto 35,000 kote Kenya na Tanzania.

Kufuatia tamasha la Krismasi, Mzee Rasband alikuwa na fursa ya kuzungumza na Dkt. Mulli akimwambia kwamba atakuwa Kenya mwaka unaofuata akisema, “Nitakapokuja Kenya, nataka nikutane nawe, na nataka nikushukuru kwa mema yote unayoyafanya katika ulimwengu, na hasa Afrika.”

Tamanio hilo lilizaa matunda pale Dkt. Mulli, Esther na binti yao Grace, walipohudhuria tukio lililoandaliwa kwa heshima yao katika ofisi za eneo za Kanisa huko Nairobi, Kenya, wakija na kwaya iliyotengenezwa na kundi la watoto kutoka kwenye taasisi yao. Mzee Rasband alizungumza kwenye tukio hili akisema, “Ni ya kupendeza kwangu hivi leo kuwa hapa na kuona utimizwaji, Dkt. Mulli, wa matembezi yale mafupi tuliyokuwa nayo huko Jijini Salt Lake, ambapo nilikuahidi kwamba tungekutana tena Kenya.”

Dkt. Mulli pia alifurahishwa, alipokuwa akisema katika mazungumzo yake “Nina furaha sana, mwenye shangwe sana kuwa pamoja nawe… Nina furaha sana na kupendezwa, amani ya Mungu iwe miongoni mwenu, akina kaka na dada katika Kristo.” Pia alizungumza kuhusu muda wake huko Jijini Salt Lake akiufafanua kama “mbingu nyingine, shangwe, utukufu na nguvu ya watu hao na ni wakuu.”

Alitoa shukrani zake kwa Kristo kwa kumpa “Nguvu ya kusamehe” akisema “Nilipopata kujua nguvu hiyo ya kusamehe, kisha niliwaza, sasa ilikuwa muda wangu, kuwasamehe baba yangu na mama yangu. Na baadaye, tuliweza kukutana pamoja, badala ya kupigana, ilikuwa ni mpango mkubwa, kwamba ilikuwa ni shangwe kubwa, kushangilia kama familia.

Aliendelea akisema, “Na hapa nipo, nikiwa baba wa wasio na baba . . . na kweli najua sasa kwamba ni katika kuokoa maisha mengi ya vijana hao wadogo, walio na uraibu wa madawa ya kulevya yanayoleta kuiba, wezi, aina hiyo ya watu, . . . sasa ninapotazama nyuma, nasema haleluya, sifa ziwe kwa Bwana.”

Kufuatia mazungumzo yake, Dkt. Mulli alitambulisha kwaya ya watoto wake ambao waliimba na kucheza kwa umati, wakiwafurahisha wote waliohudhuria. Kuhusu kwaya yake Dkt. Mulli alisema, “Sifa ziwe kwa Bwana, Mungu wetu. Wale waliotengwa na kukataliwa na jamii, ndio watakaoimba sifa kwa Bwana. Wakati mwingine tunashangaa, tunapoona watoto wa mtaani huko Nairobi, au kwingineko, kwenye mabara mengine, tunashangaa, tutafanyaje? Ni mpango wa Mungu, mtoto mmoja kila wakati. Miaka yote hiyo, Mungu amefanya mambo makuu.”

Baada ya kwaya kuimba Mzee Rasband alisema, “Dkt. mulli, Bi. Mulli, Grace na watoto wazuri, kwaya, mnamcha Yesu Kristo kwa kuwa hapa leo na nahisi kwamba Yesu Kristo anatabasamu kwenu na kwa familia zenu hivi leo. Mnaleta utukufu kwa jina Lake. Na mnafanya yote kwa jina Lake. Ni mchango mkubwa ulioje kwako, Daktari.”

Aliendelea kwa kusema, “Kanisa letu hufundisha kuwapenda binadamu wenzetu, amri mbili kuu, ‘mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, uwezo, akili na nguvu’, amri kuu ya pili ni ‘mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe’. Taasisi unayoiwakilisha huonyesha upendo wako kwa Mungu kupitia upendo wako kwa wanadamu wenzako. Tunakusifu na tunamsifu Mungu kwamba amekufanya wewe kuwa chombo katika mikono Yake kuwaleta watoto hawa na [hivi karibuni] watoto wengine 9000 kutoka mitaani kokote unakowapata na kuwapa mahali wanakoweza kupaita nyumbani, na mama na baba wanaoweza kuwaheshimu.

Mzee Rasband kisha aliwakabidhi Dkt. Mulli na Bi. Mulli mchango wa taasisi yao na kusema, “inaweza kuonekana kama zawadi kutoka Kanisani, lakini ni kutoka kwa waumini wa Kanisa. Kile tunachokwenda kutoa kwako leo ni kutoka kwa waumini wa kanisa letu ambao wamejiunga pamoja kutoa mchango wa kipesa kwa ajili ya taasisi yako nzuri. Aliendelea kwa kuongeza, “Mungu akubariki wewe, mke wako, familia yako ya kibaiolojia, na familia yako kubwa ya kuasili, katika kazi yako ya Bwana, Yesu Kristo.”

Kwa kujibu wema huu Dkt. Mulli alisema, “Kwa kweli niseme nini kuhusu Kanisa la Yesu Kristo la Siku za Mwisho, linavyoonyesha upendo wa kweli wa Yesu Kristo? Alitupatia njia, alituonyesha njia, alisema ‘Waacheni watoto wadogo waje kwangu, kwani ufalme wa Mungu ni wao’. Kwa hivyo, katika siku zijazo watakuwa baba, watakuwa mama, watakuwa wamisionari, na watafundisha kwa ulimwengu mzima. Aliongeza, “Kutoka kwenye kanisa lenu, upendo ambao mmetuonyesha miaka michache iliyopita, . . . nimemuona Kristo ndani yenu. Shangwe ya Bwana ni nguvu yetu. Hii ni siku ambayo Bwana ameiandaa na ninahisi mwenye fursa kubwa ya kusema asante, asante, Bwana awabariki. Asanteni sana”.