Sauti za Wanachama
Kutoka kuwa Wakimbizi hadi Waanzilishi
Uanzishwaji wa Tawi la Kakuma kwenye Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma
Aprili 6 ni siku muhimu katika historia ya Kanisa. Katika siku hii mnamo mwaka 1830, Kanisa liliundwa huko mji wa Fayette, New York, likianza kwa waumini sita pekee. Mnamo Aprili 6, 2025, kundi lingine dogo lilikutana pamoja ili kuunda tawi la kwanza la kanisa kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kambi yenye takribani wakimbizi 300,000 kutoka nchi zaidi ya 20, iliyoko Kijiji cha Kalobeyei, Kenya.
Kama vile katika siku za mwanzo za kanisa, watafutaji wa ukweli wanasikia ujumbe wa urejesho wa injili na kwa shangwe wanajiunga na ufalme wa Mungu.
Kambi iko Kaskazini-magharibi mwa Kenya, (km 419 kutoka Kitale, ambapo tawi la karibu lililoundwa lilipatikana), na waumini wachache walioishi kambini walikuwa wamewasiliana mara nyingi na viongozi wa kanisa, zaidi ya kipindi cha takribani miaka 9, wakiomba tawi lianzishwe huko. Baada ya kupokea zana zilizotolewa kama msaada kutoka kwa wasamaria wema, kama vile Maak Impact (Shirika lisilo la Kiserikali), ambavyo vilitumika kutoa ufikiaji wa intaneti na kutengeneza kivuli ambapo waumini wangekutana, ndipo ilipokuwa rahisi kuwasiliana kwa urahisi na rais wa Misioni ya Nairobi West, David Sturt.
Kiongozi wa kundi, Elias Zablon, alisafiri hadi Kitale, ili kukutana na rais wa misioni, pamoja na rais wa wilaya, Anthony Matende, jambo ambalo lilisababisha Rais Matende kutembelea kambi ili kutathmini uhitaji. Ziara yake ilifuatiwa na ziara ya Rais Sturt na mshauri wake wa pili (wakati huo) Rais Munene (sasa ni Mzee Munene, sabini wa eneo).
Hatimaye, baada ya kupata idhini ya kuunda tawi, Rais Sturt na mshauri wake wa 2, Rais Meshack Odunga, walirejea kambini mnamo Aprili 6, 2025, ili kuunda Tawi jipya la Kakuma la Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, Imani Botrus akiitwa kama Rais mpya wa Tawi. Tawi hili jipya lililoundwa lilikuwa na watu watano pekee, sawa na mwanzo wa unyenyekevu wa kanisa katika mwaka 1830.
Akizungumza na watakatifu hawa Rais Odunga alisema, “Ni vizuri kujifunza kutoka kwenu na kuona jinsi mambo yanavyojifunua mstari juu ya mstari. Tuna shukrani kwa imani ya watakatifu hapa … tafadhali kumbukeni kwamba ninyi ni waanzilishi wa kweli wa mahali hapa … tafadhali kumbukeni safari iliyofanywa na waanzilishi wa mwanzo wa kanisa, kama isingekuwa dhabihu yao na ari yao, hatujui nini kingetokea. Nyakati zingine kuteseka kunatujenga, na tunaomba kwamba muwe na imani kubwa katika Bwana kama mwanzilishi na mtimizaji wa mambo yote, na mambo mazuri hakika yatakuja. Ninyi ni waanzilishi mahali hapa, na mnavyo vyote [ambavyo] vinahitajika ili kulikuza kanisa hapa”
Katika mazungumzo yake, Rais Sturt aliongeza, “Tunawashukuru wale wote waliofanya siku hii iwezekane, ikiwa ni pamoja na kaka zetu waliotoa intaneti na kivuli hiki, ambavyo vimefanya iwe rahisi sana tawi hili kuundwa. Leo ni siku kubwa kwetu sote na tawi la Kakuma sasa ni tawi rasmi la Kanisa.”
Kama vile waanzilishi wa mwanzo walivyolijenga kanisa, watakatifu wa Kakuma wanalikuza kwa haraka tawi lao dogo. Mnamo Mei 25, 2025, waumini ishirini na sita walibatizwa na kukaribishwa kwenye tawi la Kakuma, mwanzo wa kupendeza kwao, na ongezeko la kupendeza kwenye ufalme wa Bwana.