Liahona
Niliogopa kuzungumza na Askofu Wangu—Je, Angenichukulia Vipi?
Januari 2026 Liahona


“Niliogopa kuzungumza na Askofu Wangu—Je, Angenichukulia Vipi?” Liahona, 2026.

Kutoka kwa VW Kila Wiki

Niliogopa kuzungumza na Askofu Wangu—Je, Angenichukulia Vipi?

Nilikuwa nafanya chaguzi mbaya. Lakini nilipozungumza na askofu wangu, yote niliyojisikia yalikuwa ni faraja.

mtu akishikana mikono na askofu wake

Nilipokuwa nikiishi peke yangu kwa mara ya kwanza, nilijisikia hisia mpya ya uhuru.

Nilikuwa nimehamia Ufilipino kuanza shule, na kusafiri kwa ndege kwenda nyumbani ilikuwa ghali, kwa hivyo nilitembelea tu mara moja kwa mwaka ili kufanya upya visa yangu. Bila ushawishi aminifu wa familia yangu karibu, pole pole nilipotea kutoka kwenye injili.

Nilianza kuvuta sigara, kunywa, na kufanya mambo mengine ambayo nilifundishwa yalikuwa kinyume na amri za Mungu.

Kukumbuka Mimi ni Nani.

Mwanzoni, sikujali. Niliona sheria za Kanisa kama kizuizi. Bado nilienda kanisani, lakini kwa kina nilihisi kutostahili na nikaacha kupokea sakramenti kwa miezi kadhaa.

Kisha COVID-19 ikaja, na kusitisha shughuli zangu zote. Wakati huo huo, nilijifunza kitu cha kushtua: Mimi ni mtoto wa kupangwa. Wazazi wangu hawakuwahi kuniambia, na nilipitia hali ya wasiwasi mkubwa kiasi wa utambulisho.

Nilihisi kuwa mbali na kila kitu nilichoamini. Nilijua nilihitaji kuamua mimi nilikuwa nani kwa kweli tena. Mwishowe wakati nilipoenda nyumbani, nilifunguka kwa wazazi wangu kuhusu kila kitu—ikijumuisha chaguzi nilizokuwa nikifanya. Badala ya kunikaripia, wao walijibu kwa upendo. Walinikumbusha mimi ni nani hasa: mwana wao na mwana mpendwa wa Mungu.

Msaada katika Kubadilika

Nilitaka kubadilika. Wazazi wangu walinitia moyo kuzungumza na askofu wangu, kuanza mchakato wa toba, na kutegemea nguvu ya ukombozi ya Mwokozi.

Lakini nilikuwa ninaogopa!. Nilikuwa na wasiwasi kuhusu kuadhibiwa au kuhukumiwa kwa chaguzi zangu. Kwa kawaida sijali watu wanafikiria nini juu yangu, lakini askofu wangu alikuwa mtu wa kupendeza sana, na sikutaka kumkatisha tamaa kwa kumwambia kile nilichokifanya.

Lakini kama Mzee Scott D. Whiting wa Wale Sabini alivyofundisha: “Usijifiche kutoka kwa wale ambao watakupenda na kukuunga mkono; badala yake, wakimbilie. Maaskofu, maraisi wa matawi, na viongozi wengine wazuri wanaweza kukusaidia kuifikia nguvu ya uponyaji ya Upatanisho wa Yesu Kristo.”

Maaskofu “wanashikilia funguo za ukuhani ili kumwakilisha Bwana katika kuwasaidia waumini wa Kanisa kutubu.” Badala ya kukabiliana na hukumu kali nilipozungumza naye, yote niliyojisikia katika ofisi ya askofu wangu yalikuwa ni faraja. Nilitambua kwamba Bwana alimwamini yeye kunisaidia, na nilijisikia ningeweza kumwamini yeye pia.

Askofu wangu alinitia moyo kujifunza kuhusu Mwokozi na Upatanisho Wake kwa kujenga tabia za kiroho. Nilikutana na askofu wangu mara kwa mara, na aliniita kila wiki kunijulia hali. Nilihisi kupendwa sana kila mara nilipoongea naye.

Zawadi ya Toba

Hatimaye, kwa msaada wa askofu wangu, niliondoka mbali na uovu katika maisha yangu. Bado, nilikuwa na wasiwasi kuhusu kupokea sakramenti tena. Je, kweli nilikuwa mstahiki—hata baada ya matendo yote niliyofanya?

Lakini askofu wangu alinihakikishia. Alinikumbusha kwamba sikuhitaji kuwa mkamilifu—niwe mtu aliye tayari tu. Nilikuwa nikifanya kadiri niwezavyo, na Mwokozi alijua hivyo na angeendelea kunisamehe nilipotegemea zawadi Yake ya toba.

Dada Tamara W. Runia, Mshauri wa Kwanza katika Urais Mkuu wa Wasichana, hivi karibuni alifundisha, “Kuja kwa Kristo ni kusema, ‘Je, utanisaidia?’ kwa tumaini, hakikisho lililofunuliwa kwamba mikono Yake amekunyoshea wewe daima.”

Baada ya uzoefu huu, nilianza kufanya upya maagano yangu kupitia sakramenti kwa kujiamini. Nilihisi kama mtu mpya, nikiwa na hisia mpya ya mimi ni nani hasa na kile ninachoweza kufanya kwa msaada wa Bwana. Hata nilitumikia misheni kwa sababu baada ya kushuhudia ni kiasi gani zawadi ya Mwokozi ya ukombozi imebadilisha maisha yangu, nilitaka kuwasaidia wengine kupata tumaini Yeye analonipa mimi kila siku.

Amri hazizuii—zipo kwa sababu Mungu anataka tufanikiwe, tukue, na kuepuka mtego wa dhambi. Kitovu cha injili ya Yesu Kristo ni upendo ambao Yeye na Baba wa Mbinguni wanao kwa ajili yetu. Kwa sababu ninapata uzoefu wa upendo huo mkamilifu, ninajitahidi kuwa zaidi kama Wao.

Zawadi yao ya toba hujaza maisha yangu kwa shangwe.