“Washiriki wa Asili ya Kiungu,” Liahona, Januari 2026.
Washiriki wa Asili ya Kiungu
(2 Petro 1:4)
Maarifa juu ya mpango wa wokovu yanatoa mtazamo wa thamani, unaorutubisha shangwe yetu, na kutuimarisha ili kushinda changamoto zetu na dhiki.
Kristo Akiwaita Wanafunzi Wawili,, na Gary E. Smith
Mtume Petro anatukumbusha kwamba kwa wanafunzi wa Yesu Kristo, “Uweza Wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua Yeye aliyetuita kwa utukufu Wake na wema Wake mwenyewe:
“Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani: ili kwamba kwa hizo tupate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, (2 Petro 1:3–4; mkazo umeongezwa).
Mpango wa Baba wa Mbinguni unaelezea kweli kuu na za thamani na ahadi ambazo zinaelezea utambulisho wetu wa milele na dhumuni letu.
Kama ilivyoelezewa katika “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”
“Wanadamu wote—wanaume na wanawake—wameumbwa katika mfano wa Mungu. Kila mmoja ni mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni, na, kama hivyo, kila mmoja anayo asili takatifu na takdiri. …
“Katika maisha ya kabla ya duniani, wana na mabinti wa kiroho walimjua na kumwabudu Mungu kama Baba yao wa Milele na kukubali mpango Wake ambao ungewezesha watoto Wake kupokea mwili na kupata uzoefu wa kidunia ili kukua kwa ukamilifu na hatimaye kutambua majaaliwa yao ya kiungu kama warithi wa uzima wa milele.”
Baba wa Mbinguni anawaahidi watoto Wake kwamba kama watafuata muongozo wa Mpango Wake na mfano wa Mwana Wake Mpendwa, kushika amri, na kuvumilia katika imani hadi mwisho, watapata uzima wa milele, zawadi iliyo kuu katika zawadi zote za Mungu” (Mafundisho na Maagano 14:7).
Kazi ya Mungu imefokasi juu ya maendeleo na kuinuliwa kwa watoto Wake. Kila sehemu ya mpango Wake imesanifiwa ili kuwabariki wana na mabinti Zake kwa sababu “thamani ya nafsi ni kubwa mbele [Zake]” (Mafundisho na Maagano 18:10).
Mpango wa Baba
Katika baraza la mbinguni kabla ya kuja duniani, Baba wa Mbinguni aliwasilisha kwa watoto Wake wa kiroho mpango Wake kwa ajili ya maendeleo yao ya milele na furaha.
“Tutaifanya dunia mahali ambapo hawa watapata kukaa;
“Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru;
“Na wao ambao watatunza hali yao ya kwanza wataongezewa; na wao ambao hawatatunza hali yao ya kwanza hawatapata utukufu katika ufalme ule ule pamoja na wale walioitunza hali yao ya kwanza; nao wale watakaoitunza hali yao ya pili watapata kuongezewa utukufu juu ya vichwa vyao kwa milele na milele.
“Na Bwana akasema: Nimtume nani? Na mmoja aliyekuwa mfano wa Mwana wa Mtu akajibu: Niko hapa, nitume mimi. Na mwingine akajibu na kusema: Niko hapa, nitume mimi. Na Bwana akasema: Nitamtuma wa kwanza.
“Na wa pili akakasirika, na hakuitunza hali yake ya kwanza; na, katika siku ile, wengi wakamfuata” (Ibrahimu 3:24–28).
Kumbuka kwamba mpango mmoja tu uliwasilishwa katika baraza kule mbinguni kabla ya kuja duniani—mpango wa Baba. Baba yetu wa Mbinguni hakuuliza swali, “Tutafanya nini?” Hakutafuta mchango, hakutaka mapendekezo, au kuomba ushauri. Badala yake, aliwasilisha vipengele vya msingi vya mpango Wake na kuuliza, “Nimtume nani?” Kiini cha swali Lake kililenga kwa nani anapaswa kutumwa kutekeleza vigezo na masharti ya mpango Wake.
Matokeo ya uasi wa adui pia yameelezewa katika maandiko.
“Kwa hiyo, kwa sababu yule Shetani aliasi dhidi yangu, na akatafuta kuangamiza haki ya mtu ya kujiamulia, ambayo Mimi … nimempa, na pia, kwamba alinitaka nimpe yeye uwezo wangu mwenyewe … , nikamfanya atupwe chini;
“Naye akawa Shetani, … ibilisi, baba wa uwongo wote, ili kudanganya na kuwapofusha watu, na kuwaongoza utumwani kadiri apendavyo, hata wengi kadiri wasivyosikia sauti yangu” (Musa 4:3–4).
Lusiferi hakuwasilisha mpango ambao ulipingwa kwa kura ya wengi wa washiriki katika baraza kabla ya kuja duniani. Yeye sio mtu mwenye huruma ambaye alipoteza uchaguzi. Yeye aliasi! Kiburi, majivuno, na ubinafsi vilichochea uasi wake dhidi ya mpango wa Baba.
Mpango wa Baba na Injili ya Mwokozi
Mpango unaelezea kazi za Baba na Mwana ambazo zinafanya baraka za uzima wa milele zipatikane kwa wanadamu wote.
Injili ya Yesu Kristo inajumuisha njia ambayo kwayo tunaweza kupokea baraka zilizoahidiwa katika mpango wa Mungu, hata mafundisho, kanuni, ibada, na maagano ambayo wanaume na wanawake lazima waamini na kufuata. “Hakuna jina lingine ambalo limetolewa chini ya mbingu ila tu awe huyu Yesu Kristo, … ambamo kwamba mwanadamu anaweza kuokolewa” (2 Nefi 25:20). Kweli, Bwana Yesu Kristo ndiye “njia, ukweli, na uzima: mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya [Yeye]” (Yohana 14:6; mkazo umeongezwa).
Rais Russell M. Nelson alielezea:
“Mpango ulihitaji Uumbaji, na hili nalo lilihitaji yote Anguko na Upatanisho. Hizo ndizo sehemu tatu za msingi za mpango huu. Uumbaji wa sayari ya kiparadiso ulitoka kwa Mungu. Maisha ya duniani na kifo vilikuja ulimwenguni kupitia Anguko la Adamu [ona 2 Nefi 2:25; Musa 6:48]. Kutokufa na uwezekano wa uzima wa milele vililetwa na Upatanisho wa Yesu Kristo [ona 2 Nefi 2:21–28]. …
“… Tunakuja duniani kwa muda mfupi, kuvumilia mitihani na majaribu yetu, na kujiandaa kusonga mbele na juu kwenye makaribisho matukufu ya kurudi nyumbani [ona Zaburi 116:15; Alma 42:8]. Mawazo na matendo yetu wakati [tukiwa duniani] hakika yatakuwa yenye kusudi zaidi kama tunaelewa mpango wa Mungu na kuwa wenye shukrani kwa ajili ya na watiifu wa amri Zake” [ona Mafundisho na Maagano 59:20–21].”
Majina ya Mpango huu katika Kitabu cha Mormoni
Tunajifunza kweli muhimu kwa kutambua na kujifunza majina mengi tofauti ya mpango wa Baba katika Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo. Kwa mfano, fikiria sampuli ifuatayo iliyochaguliwa ya vichwa:
“Mpango wa huruma wa Muumba mkuu” (2 Nefi 9:6).
“Mpango wa Mungu wetu” (2 Nefi 9:13).
“Mpango wa wokovu” (Yaromu 1:2; Alma 24:14).
“Mpango wa ukombozi” (Alma 12:25, 26, 30, 32, 33; 42:11, 13).
“Mpango wa urejesho” (Alma 41:2).
“Mpango wa furaha” (Alma 42:16).
“Mpango mkuu wa rehema” (Alma 42:31).
Kila moja ya vichwa hivi hutusaidia kuelewa kwa uwazi zaidi ahadi za thamani za mpango wa Baba na hurutubisha mtazamo wetu kuhusu malengo na maana ya maisha yetu duniani.
Cha muhimu zaidi, kichwa kinachotumika mara kwa mara kwa mpango wa Mungu katika Kitabu cha Mormoni hufokasi juu ya ukombozi uliowezeshwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.
Alma alisema, “Kama hakungekuwa na mpango wa ukombozi, ambao ulipangwa tangu msingi wa ulimwengu, hakungekuwa na ufufuo wa wafu; lakini kulikuwa na mpango wa ukombozi ambao ulipangwa, ambao utawezesha ufufuo wa wafu” (Alma 12:25).
Alionya pia, “Uanze kuamini katika Mwana wa Mungu, kwamba atakuja kukomboa watu wake, na kwamba atateseka na kufa ili alipie dhambi zao; na kwamba atafufuka tena kutoka kwa wafu, na kutimiza ufufuo, kwamba watu wote watasimama mbele yake, kuhukumiwa katika siku ya mwisho na ya hukumu, kulingana na matendo yao” (Alma 33:22).
Njia Imeandaliwa
Nafsi zetu zinapaswa kuvimba kwa shukrani tunapofikiria mpango mkuu wa wokovu, ukombozi, urejesho, rehema, na furaha. Maarifa ya mpango Wake hutoa mtazamo wa thamani, unarutubisha shangwe zetu, na kutuimarisha ili kushinda changamoto zetu na dhiki.
Baba wa Mbinguni anatamani turudi nyumbani Kwake. Yeye anaalika na kuahidi baraka, lakini Yeye kamwe hatalazimisha, kushurutisha, au kuzuia matumizi yetu ya maadili ya haki ya kujiamulia aliyotupatia. Lazima tutende na kuchagua kurudi Kwake kwa kufuata mfano wa Mwanawe Mpendwa.
Mkono Wake Umenyooshwa Bado, na Elizabeth Thayer
“Njia imetayarishwa, na ikiwa tutaangalia tutaishi milele” (Alma 37:46; mkazo umeongezwa).
Kwa shangwe ninashuhudia kwamba Baba wa Mbinguni ni mtunzi wa mpango mtakatifu kwa ajili ya watoto Wake. Yesu Kristo ni Mkombozi na Mwokozi wetu. Na kama mmoja wa Mitume wa Bwana wa siku za mwisho, ninashuhudia kwamba hakika Yeye ndiye “ njia, kweli, na uzima” (Yohana 14:6; mkazo umeongezwa).