“Pale Dhambi Inaposababisha Machafuko, Kristo Huleta Amani,” Liahona, Jan. 2026.
Kutoka VW Kila Wiki
Pale Dhambi Inaposababisha Machafuko, Kristo Huleta Amani
Hata katikati ya machafuko ya maisha, Kristo anaweza kuleta nuru, utaratibu, na amani katika nafsi yako.
Kielelezo na Kate Birch
Je, unahisi maisha kidogo yana … machafuko?
Kupata hisia ya machafuko ni kitu ambacho sote tunapitia wakati mwingine. Uchangamani wa ulimwengu hufanya iwe rahisi kusahau kwamba sisi ni viumbe wa kiroho tukiwa na uzoefu wa maisha ya duniani—kitu ambacho hatujawahi kufanya hapo awali.
Zawadi mbili za kimiujiza ambazo Mungu alitupatia ni miili na haki ya kujiamulia. Zawadi hizo zinaturuhusu kuhisi, kutamani, na kujitendea wenyewe. Kawaida sana, mambo yanaweza kuonekana kuchafuka au kutokuwa na uhakika kwa sababu ya chaguzi mwanamke wa asili au mwanaume wa asili anaelekea kufanya.
Sisi sote tunafanya makosa. Lakini tunapo pambana na dhambi au tabia ambazo hatuwezi kuonekana kuzishinda, bila kujali ni vigumu kiasi gani tunajaribu kubadilika, ni rahisi kuhisi hisia ya vurugu. Tukiwa na upande wetu wa kiroho ukituvuta kuelekea mbinguni na upande wa duniani ukituvuta kuelekea ulimwenguni, inaweza kuonekana kama mvutano wa ndani wa kila mara.
Iwe tunapambana na vitu kama umbeya, hasira, hukumu isiyo ya haki, kujihusisha na vyombo vingi vya habari, matumizi ya ponografia, au kitu kingine cho chote, adui ni mwepesi wa kupuliza miale ya aibu, kutokuwa na matumaini, na hatimaye, machafuko ya kiroho.
Kwa bahati nzuri kwetu sisi, Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanajua jinsi ya kushughulikia machafuko.
Kutafuta Nuru Yake Ni Hatua ya Kwanza
Wakati wa Uumbaji—mwanzo wa kila kitu tunachokijua—ulimwengu unaelezwa kuwa katika hali ya machafuko, isiyo na mpangilio: “Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi” (Mwanzo 1:2). Machafuko haya na giza lisilo na matumaini ni makumbusho ya jinsi adui anavyoweza kutufanya tujisikie wakati tunapotenda dhambi au kufanya chaguzi ambazo zinakwenda kinyume na maadili yetu. Anafurahia kutufanya tujisikie kunaswa na mara nyingi anatuhimiza tujifiche.
Lakini kama Dada Tamara W. Runia, Mshauri wa Kwanza katika Urais Mkuu wa Wasichana, alivyofundisha: “Yesu Kristo anatoa nuru kwa wale wanao kaa gizani. Hivyo, katika siku hizo unapohisi sauti ile ikikuambia ujifiche, kwamba unapaswa kujificha kwenye chumba chenye giza ukiwa pekee yako, ninakualika uwe jasiri na amini katika Kristo! Tembea na uwashe Nuru—Mng’aro wetu Mkamilifu wa Tumaini.”
Chini ya maelekezo ya Mungu, wakati wa Uumbaji kitu cha kwanza Yesu Kristo alichofanya ili kutawanya giza la machafuko ilikuwa ni kuleta nuru (ona Mwanzo 1:3; Musa 2:2–5). Kutoka hapo, Yeye aliendelea kupanga kila sehemu ya vurugu ya mambo, kutoka mbingu kubwa hadi kwenye mche mdogo sana.
Kama Yeye angeweza kuleta utaratibu ulimwenguni, fikiria kile kinachoweza kutokea wakati unapomgeukia Mwanawe kwa ajili ya uponyaji na nguvu za ukombozi kila siku. Unapohisi kama umelemewa na mapambano yako na giza la ulimwengu, kufikia nuru ya Kristo ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye amani na mpangilio wa kiungu.
Halafu, Kumbuka Wewe U Nani
Baada ya mbingu na dunia kupangwa na kurembeshwa, Baba wa Mbinguni aliandaa njia kwa ajili ya watoto Wake wa kiroho kuja duniani na kupokea miili. Lakini wakati wa muda wetu duniani, adui anafanya kazi kwa bidii ili kutufanya tusahau sisi ni kina nani.
Tunaweza kuona juhudi zake za kutuyumbisha kutoka kwenye utambulisho wetu wa kiungu katika wakati ambapo Mungu anazungumza na nabii Musa na kushiriki maarifa naye. Katika Musa 1, Mungu anaongea na Musa kwa kumwita jina na mara kwa mara anamwita Musa Mwanaye.
Lakini mara Mungu anapoondoka, Shetani anatokea na kumwita Musa “mwana wa mtu” (Musa 1:12), akimjaribu ili asahau kwamba yeye ni nani hasa.
Shetani anatutaka sisi tusahau kuwa hakika sisi ni kina nani. Anaingiza shaka katika uwezo wetu wa kubadilika. Anataka sisi tuamini sisi ni wanaume na wanawake, wasio badilika na daima tutakuwa hivyo.
Lakini Mzee Patrick Kearon wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili anatukumbusha: “Unaweza kuja kwa Kristo kwa kujiamini katika ukarimu Wake wa upendo na kupokea karama Zake zote za furaha, amani, tumaini, nuru, ukweli, ufunuo, maarifa, na hekima. … Wewe ni binti mpendwa wa Mungu, wewe ni mwana mpendwa wa Mungu, na Yeye amekuzawadia wewe Mwanawe Mkamilifu Mwanawe mtakatifu, ili kukukomboa, kukutetea, na kukutakasa.”
Ukombozi ni kitu ambacho Shetani kamwe hatakuwa nacho. Na tunapoegemea kwenye utambulisho wetu wa kiroho, tunaweza kusema, kama Musa alivyofanya:
“Wewe ni nani? Kwa maana tazama, mimi ni mwana [au binti] wa Mungu, katika mfano wa Mwanawe wa Pekee. …
“Nenda zako, Shetani; usinidanganye; kwa maana Mungu aliniambia: Wewe ni mfano wa Mwanangu wa Pekee”(Musa 1:13, 16).
Kama maisha yanaonekana kuwa vurugu, tulia. Kumbuka utambulisho wako wa kiungu. Acha ukweli huo, kwamba wewe ni mtoto mpendwa wa Mungu, ukuvute kuelekea mbinguni. Mgeukie Yesu Kristo ili aweze kukusaidia kurejesha utaratibu kwenye nafsi yako.
Hatimaye, Mruhusu Kristo Ageuze Machafuko kuwa Amani
Wakati Adamu na Hawa walipoondoka kwenye Bustani ya Edeni, urahisi walio ujua daima ulibadilishwa na ulimwengu wa upweke na wa kutisha. Lakini Baba wa Mbinguni aliahidi kwamba wangeweza kuwa na amani kwa sababu Yeye alimtayarisha Mwokozi ili kuwakomboa kutokana na dhambi zao na huzuni zao (ona Musa 5:7–10).
Wakati unapohisi kuzidiwa na maisha ya duniani, kumbuka ukweli huu: Baba wa Mbinguni alijua tulikuwa tunakwenda kukabiliana na majaribu, kufanya makosa, na kutenda dhambi kote katika safari hii ya kurudi nyumbani Kwake—hiyo yote ilikuwa sehemu ya mpango.
Kwa kupitia Yesu Kristo, Baba wa Mbinguni daima anaweza kutusaidia kufukuza nguvu za giza katika maisha na kutwaa nuru. Bila kujali ni mara ngapi tunakosea, kwa sababu ya Mwokozi wetu, tunaweza kubadilisha machafuko kuwa amani ndani ya nafsi zetu pale tunapotubu.
Rais Russell M. Nelson alishuhudia:
“[Yesu Kristo] atakuimarisha wewe. Yeye atakubariki na amani, hata katikati ya machafuko. …
“Yesu Kristo alijichukulia juu Yake mwenyewe dhambi zako, maumivu yako, kuvunjika moyo , na madhaifu yako. Huna haja ya kuyabeba pekee yako! Yeye atakusamehe unapotubu. Yeye atakubariki na kile unachohitaji. Yeye atatibu nafsi yako iliyo jeruhiwa.”
Cho chote unacho pambana nacho, unapomgeukia Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kwa ajili ya msaada, Wanaweza daima kurejesha kile kilicho katika machafuko, kukuweka huru kutokana na machafuko ya dhambi na majaribu, na kuyapendezesha maisha yako.
Wamefanya hivyo tena na tena.