“Usalama katika Injili ya Urejesho ya Yesu Kristo,” Liahona, Jan. 2026.
Wanawake wa Agano
Usalama katika Injili ya Urejesho ya Yesu Kristo
Njia ya kurudi kwa Mungu imewekwa alama zilizo wazi kama tunayo imani na tunamwamini Mwokozi wetu.
Kwa sababu ya asili zetu za anguko na hali za maisha ya duniani, sote tuko katika hatari ya kutangatanga mbali na Mungu tuliyemjua na kumpenda katika maisha kabla ya kuja duniani. Ni asili ya maisha ya duniani. Na hivyo, Yeye ametupatia njia za kutuweka salama Kwake, kuifunga mioyo yetu Kwake, na kutusaidia kutembea salama iwezekanavyo kupitia uwanda huu wa mabomu ya maisha ya duniani.
Wakati wa vita vikuu vya ulimwengu, vikosi vya majeshi vingeficha mabomu, au vilipuzi, chini ya ardhi. Kulikuwa na viwanja vikubwa vya mabomu yaliyofichwa, na jeshi pasipokujua wangeweza kwenye viwanja hivi vya mabomu na kulipuliwa.
Baada ya vita, maelfu ya mabomu ambayo hayajalipuka yalibakia, na watu wengi, ikiwa ni pamoja na watoto, walipoteza maisha au viungo vyao pale ambapo bila kujua waliingia kwenye viwanja hivyo vyenye mabomu. Mashirika yaliyojitolea kuyatafuta na kuwekea alama viwanja hivyo vyenye mabomu yameokoa maisha ya watu wengi.
Maisha ya duniani ni kama uwanja wenye mabomu. Adui ni mwerevu sana katika kuficha hatari ili zionekana kutoweza kudhuru na zenye kualika, kama uwanja mzuri. Amekuwa na maelfu ya miaka ya uzoefu wa kufanya hivi. Ni mtaalamu wa kufanya njia kuonekana zenye kualika ambazo huongoza kwenye matokeo hatari na maumivu ya moyo.
Ongozwa Salama Nyumbani
Baba yetu wa Mbinguni anajua jinsi ya kutuweka salama na ameweka alama kwenye njia ya kutuongoza nyumbani salama. Bila shaka, kuna hatari nyingi na magumu ambayo ni sehemu ya uzoefu wetu duniani. Lakini tunaweza kuepuka chaguzi ambazo zinaweza kuleta mizigo isiyohitajika na maumivu ya moyo.
Hiyo ndiyo sababu Baba yetu ametupatia amri, kipawa cha Roho Mtakatifu, manabii ili kutuongoza sisi, na miunganiko ya maagano yenye nguvu pamoja Naye na Mwokozi wetu kupitia ibada na maagano ya hekaluni. Ni hapa tu katika Kanisa la Yesu Kristo lililorejeshwa ndipo tunapopata alama hizo zote zenye nguvu na ulinzi ambazo zinaweza kutuongoza nyumbani kwa usalama.
Kuna baraka kuu katika kuwa na manabii wa siku za leo. Rais Hugh B. Brown (1883–1975), aliyekuwa mshauri katika Urais wa Kwanza, alielezea kuhusu majadiliano aliyokuwa nayo na mshiriki wa Bunge la Umma la Uingereza ambaye hapo awali alikuwa jaji. Mtu huyu alisema alidhani Mungu hakuwa amezungumza na watu duniani tangu karne ya kwanza, na Rais Brown alijibu kwa kumwelezea kuhusu Joseph Smith na Urejesho.
“Jaji aliketi na kusikiliza kwa makini,” Rais Brown anakumbuka. “Aliuliza baadhi ya maswali mahsusi sana na ya kuchunguza kwa undani, na mwishoni mwa mahojiano alisema, ‘Bwana. Brown, nashangaa kama watu wako wanathamini umuhimu wa ujumbe wako. Je, unajua? … Kama kile ulichoniambia ni kweli, ni ujumbe mkuu zaidi ambao umekuja duniani tangu malaika walipotangaza kuzaliwa kwa Kristo.’”
Mungu huwaita manabii kwa sababu Yeye anawapenda watoto Wake. Kupitia watumishi Wake, manabii, Yeye amefunua mpango Wake wa wokovu, mpango Wake wa furaha wa kuwaongoza watoto Wake. Bwana huwaonyesha manabii, waonaji, na wafunuzi vitu ambavyo wengine hawawezi kuviona. Wao ni walinzi juu ya mnara (ona Ezekieli 33:1–7) ambao wanaweza kuona mbali na kutoa onyo kwa wote watakaosikiliza, mara nyingi miaka mingi kabla. Wao wako mahali pafaapo ambapo sisi hatupo kwa sababu ya mawasiliano yao na Mungu kama watumishi Wake wenye mamlaka. Ni muhimu sana kwamba sote tupate shuhuda za kina, za kibinafsi juu ya manabii, waonaji, na wafunuzi wetu wa sasa.
Ukweli katika Yesu Kristo
Ni vigumu sana kutambua ukweli katika ulimwengu wetu leo. Kuna sauti nyingi zinazotoka pande nyingi sana—Instagram, TikTok, Facebook, X, podcasts, habari za televisheni, na kuendelea. Na sasa kwa akili unde, au AI, kwenye eneo, ni vigumu zaidi kutambua kile kilicho kweli na kisicho cha kweli—au hata kile kilicho halisi! Video bandia sana za udanganyifu zinaweza kuifanya ionekane kwamba mtu amesema au kufanya kitu ambacho hawajafanya. Itakuwa vigumu sana kutambua ukweli na uongo katika miaka ijayo.
Wakati wa mkutano wake wa kwanza kama Rais wa Kanisa mnamo Aprili 2018, Rais Russell M. Nelson alifundisha:
“Mimi ninayo matumaini makubwa kuhusu siku zijazo. … Lakini mimi pia sio mjinga kuhusu siku zilizo mbele yetu. Tunaishi katika ulimwengu ambao ni tata na unaoongezeka kuwa wa mabishano. Upatikanaji daima wa mitandao ya kijamii na mzunguko wa taarifa za habari saa 24 zinatushambulia kwa jumbe zisizokoma. Kama tunatakiwa kuwa na matumaini yoyote ya kuchuja sauti nyingi sana na falsafa za watu ambazo zinashambulia ukweli, lazima tujifunze kupokea ufunuo.
“Mwokozi na Mkombozi wetu, Yesu Kristo, atatenda baadhi ya kazi Zake kuu zaidi kati ya sasa na wakati atakapokuja tena. Tutaona dalili za ajabu kwamba Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, wanaongoza Kanisa hili katika ukuu wa enzi na utukufu. Lakini katika siku zinazokuja, haitawezekana kunusurika kiroho bila ushawishi endelevu wenye kuongoza, kuelekeza, na kufariji wa Roho Mtakatifu.
“… Ninawasihi muongeze uwezo wenu wa kiroho wa kupokea ufunuo. … Chagua kufanya kazi ya kiroho inayohitajika ili kufurahia karama za Roho Mtakatifu na kuisikia sauti ya Roho kila mara na kwa uwazi zaidi.”
Katika Agano la Kale kitabu cha Amosi 3:7 tunasoma, “Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lo lote, bila kuwafunua watumishi wake manabii siri yake.” Wakati sauti za ulimwengu zinapozidi kuwa kubwa na kusadikisha zaidi, kila mmoja wetu anahitaji kuweza kusikia sauti tulivu ya Roho kila mara na kwa uwazi zaidi ili kwamba tusikie na kufuata maelekezo ya Bwana kupitia manabii wanaoishi.
Mungu Anawapenda Watoto Wake Wote
Katika vyote viwili Agano Jipya na Kitabu cha Mormoni, tunasoma kwamba Mungu ni yeye yule jana, na leo, na hata milele (ona Waebrania 13:8; Mormoni 9:9). Mungu anawapenda watoto Wake katika siku yetu kama vile Yeye alivyowapenda watoto Wake katika nyakati za kale, na kwa sababu Yeye anawapenda watoto Wake, Yeye anafanya sasa kile alichofanya wakati ule. Yeye anaweka alama kwenye uwanja wa mabomu wa maisha ya duniani kwa amri ili kutuweka kwenye barabara salama; manabii wa kutoa sauti ya kuonya wanapoona hatari mbele; na maagano ya ukuhani ambayo hutuunganisha kwa uthabiti zaidi kwa Mungu.
Tunapoweka imani yetu katika Mwokozi na kumwamini, Yeye atatuongoza nyumbani kwa usalama kupitia minong’ono ya Roho Mtakatifu; kupitia maandiko ya kale na ya sasa; kupitia sauti za manabii, waonaji, na wafunuzi wa sasa; na kupitia muunganiko wa kina pamoja Naye na Baba yetu wa Mbinguni unaowezeshwa na ibada na maagano ya hekaluni.
Hakuna mahali pengine popote ambapo kuna wingi wa mwongozo na maelekezo, usalama na ulinzi, na faraja, kitulizo, na tumaini katika Kristo kuliko hapa katika injili ya urejesho ya Yesu Kristo na katika Kanisa Lake lililorejeshwa.