Liahona
Huduma kama ya Kristo Imelainisha Mioyo, Imefungua Milango huko Corsica
Januari 2026 Liahona


“Huduma kama ya Kristo Imelainisha Mioyo, Imefungua Milango huko Corsica,” Liahona, Jan. 2026.

Huduma kama ya Kristo Imelainisha Mioyo, Imefungua Milango huko Corsica

Wakijitolea kuwasaidia wakazi kwa njia yo yote ambayo wangeweza, wamisionari kwa kisiwa hiki cha Mediterania walikuwa wamedhamiria kuwaalika watu kuja kwa Kristo.

picha ya Bastia katika kisiwa cha Corsica

Meya wa Bastia alijua vyema sana kwamba wamisionari waliosimama mbele yake walikuwa wageni kutoka nje ya nchi. Kwa nini, alijiuliza, wavulana wangetoka nchi zingine na kujitolea kuwasaidia watu wake katika kisiwa cha Corsica?

Baada ya kutafakari, alikubali ofa yao na kuwapa changamoto ya kujitokeza mapema asubuhi iliyofuata ili kupaka rangi hoteli yake ndogo.

Wakiwa wa kweli katika ahadi yao, wavulana hao walifika saa 1:00 asubuhi, wakiwa na shauku na tayari kusafisha hoteli ya meya kwenye kisiwa hiki chenye mandhari nzuri kwenye pwani ya Ufaransa katika Bahari hii ya Mediterania.

Wakati meya alipofika hotelini baadaye siku hiyo aliwakuta wamisionari wakiwa bado wanafanya kazi katika jua la pwani, “alistaajabu kutuona pale,” alisema Jake Lowry, mmoja wa wamisionari walio hudumu wakati huo.

Akiwa ameshangazwa na utayari wao wa kupinda migongo yao ili kuwasaidia watu ambao hawakuwajua, meya alilainisha upinzani wake na “alituomba tukae chini na tumwambie kile tulichohitaji,” Kaka Lowry alisema.

Wamisionari walishiriki injili na kueleza jinsi kusudi lao lilikuwa kuwabariki watu katika kisiwa cha Corsica. Walisimulia matatizo yao katika kutafuta nyumba ya kupanga kwa sababu ya wakazi ambao walikuwa na wasi wasi juu ya watu kutoka nje ya nchi. Miezi michache kabla, wamisionari wote walikuwa wameondolewa kutoka kisiwa hicho kwa sababu za kiusalama. Lakini wazee hawa sasa walikuwa wameifungua tena nchi hiyo kwa ajili ya kazi ya umisionari.

Meya aliwasikiliza wazee hawa. “Asubuhi iliyofuata,” Kaka Lowry alisema, “alikuwa amepata nyumba nzuri kwa ajili yetu na kuandika barua ya ukarimu.”

Jioni hiyo, baada ya kukaa katika malazi yao mapya, “wawakilishi wawili walio valia vizuri kutoka ofisi ya meya walisimama kwa kutusalimia na kutuhakikishia kwamba tulikuwa tunakaribishwa na salama jijini,” Kaka Lowry alisema.

Kwa kifupi, meya na mke wake walianza kuhudhuria mikutano ya Jumapili pamoja na tawi, ambapo walipenda kuimba nyimbo za dini. Punde mke wa meya alibatizwa.

Ardhi Yenye Rutuba

Kutoka miaanzo hii rahisi mwanzoni mwa miaka ya 1990, Kanisa liliota mizizi katika kisiwa hiki mashuhuri kama mahali pa kuzaliwa kwa Napoleon Bonaparte. Punde kazi ya umisionari ikastawi. Baada ya miezi mitatu, zaidi ya watu 40 walikuwa wakihudhuria ibada za Jumapili katika sehemu ya kupendeza ya mkutano iliyopangwa na meya.

“Tukiangalia nyuma, tunaweza kuona kwamba mkono wa Bwana ulikuwa dhahiri katika muda na njia ya kuanzisha Kanisa katika kisiwa cha Corsica,” alisema Richard W. Thatcher, rais wa misheni ya Ufaransa Marseille wakati ule, sasa ni Misheni ya Ufaransa Lyon.

Lakini kupata kukua katika kisiwa hicho haikuwa rahisi. Juhudi za mwanzo za kuweka wamisionari zilikutana na upinzani na vitisho vya hatari. “Kuchemka kwa hisia za kutopenda Ufaransa kwa wenyeji Wakorsika kulikuwa kunaongezeka mwanzoni mwa miaka ya 1990,” kaka Thatcher alisema.

Wakorsika wenyeji walionyesha kutofurahishwa kwao na wageni na walitengeneza mabomu ya nyumbani kuharibu biashara za kigeni na mali. “Ilikuwa kawaida,” alisema Mzee Darin Dewsnup wa wakati huo, “kusikia milipuko mingi kila siku katika jiji. Hatukuwa Wafaransa, lakini hatukuwa Wakorsika pia.”

Wamisionari hao walionywa kuhusu hatari hizo, na wakati bomu lilipolipuka katika kitongoji chao, wamisionari wale wanne katika kisiwa hicho waliondolewa na kwenda sehemu nyingine ya misheni huko Ufaransa bara.

“Wamisionari wetu hawakuwa tena kisiwani humo,” Kaka Thatcher alisema, akisema kipingamizi hiki kilikuwa ni fursa ya kujifunza na kukua.

Huduma kama ya Kristo Ilikuwa ndilo Jibu

Ili kuelewa vyema madhumuni ya mbingu, wamisionari walijitolea kujifunza maisha na huduma ya Mwokozi ili kujifunza vyema njia Zake. Walijifunza matendo Yake ya huduma na huruma, ambayo ilijumuisha kulisha na kuponya na kupenda. Walihitimisha kwamba huduma ilikuwa muhimu katika kupata kuaminika na watu na kuhudumu katika njia ya Bwana.

Kwa fokasi iliyofanywa upya ili kuhudumu, wamisionari watatu walitumwa kufungua tena kazi huko Corsica mnamo Machi 1992. Wakati huu, walipelekwa katika jiji la pili kwa ukubwa katika kisiwa hicho, Bastia. Huko waliamua kukutana na watu kwa njia ya asili badala ya kubisha milango, ambayo wakati mwingine ilisababisha hofu miongoni mwa wakazi.

“Sala zetu zilijibiwa. Tulitambua huduma inaweza kuonyesha uaminifu wetu kwa jamii na kulainisha mioyo ya watu waliopinga watu wa nje,” Kaka Thatcher alisema.

Wamisionari wapya walijitambulisha kwa wakazi kwa kutoa msaada kwa njia yo yote ambayo wangeweza. Waling’oa magugu ya bustani za familia, kutengeneza magari, na katika jambo la meya, walipaka rangi hoteli yake iliyokuwa imepauka. Mara nyingi walipata marafiki, na juhudi zao zilithaminiwa. Karibia kila siku walikuwa wakiombwa kukaa chini na kupewa glasi ya “limonata” (juisi ya limau) na “tuambie kuhusu kanisa lenu,” Kaka Thatcher alisema. Punde, “mafanikio yetu yalibadilika sana.”

Walioelekezwa kwetu mapema walisababisha ubatizo wa familia ya Lota, ambayo kisha ilisababisha kuletwa kwa familia nyingine. Wamisionari walipoingia katika nyumba ya familia iliyoelekezwa, mama wa familia, ambaye alikuwa akiomba ili kujua ukweli, “alipiga magoti na kulia kwa shukrani kwa Bwana kwa kujibu maombi yake.”

Kuziba Mgawanyiko

Mapema katika huduma yao huko Bastia, wamisionari walikuwa wamejitolea katika hospitali kuu ya Kikatoliki, lakini monsinyori kiongozi wa hospitali alikataa huduma yao alipojua dini yao. Alisita kuwa na imani tofauti za Kikristo kuhusika hospitalini.

Miezi michache baadaye, mwezi Mei 1992, sehemu kubwa ya uwanja wa soka iliporomoka wakati wa mechi ya ubingwa, na kuua 19 na kutuma maelfu ya watazamaji waliojeruhiwa vibaya hospitalini.

uwanja wa soka ulioporomoka

Wakati uwanja wa soka ulipoporomoka huko Corsica, na kuua watu 19 na kujeruhi maelfu, wamisionari walitumia muda mrefu kusaidia huduma za dharura zilizosimamiwa katika hospitali ya eneo hilo.

Picha na Craig Peterson

Majeruhi waliizidia hospitali. Mashabiki wa soka walio jeruhiwa walijaza vyumba na kusimama kwenye shoroba. Baadhi walisafirishwa kwa ndege hadi barani Ufaransa kwa ajili ya matibabu. Monsinyori, aliyekosa watu wa kujitolea wenye uwezo, alikumbuka kadi ambayo wamisionari waliiacha na kuwaita kwa ajili ya msaada.

Kwa saa 36, wamisionari walikimbia kutoka kazi moja hadi kazi nyingine, wakisaidia aina mbalimbali za huduma za dharura zilizo simamiwa, kama vile kuning’iniza mpira ya IV, kufunga mishipi, kusafisha vyumba, na kuwasogeza majeruhi. Walitoa baraka za ukuhani kwa waumini wa tawi walio jeruhiwa katika maporomoko haya ya kuta za uwanja wa mpira.

Wakati monsinyori alipoona juhudi zisizo na kuchoka za wamisionari, aliwaita pamoja na kuwaongoza kote hospitalini, akiwaambia wagonjwa kwamba wamisionari walikuwa watu wa Mungu na kuwaruhusu kutoa baraka kwa walio jeruhiwa.

Kaka Thatcher anakumbuka: “Tulipata heshima na kusifiwa na afisa wa mji mwenye cheo cha juu na mamlaka muhimu ya kidini kwa huduma yetu.” Ililainisha mioyo na kusaidia kuondoa upinzani katika jamii, alisema. “Hii ilikuwa muhimu sana kwa mafanikio ya juhudi zetu za kuhubiri.”

Jason Soulier, rais wa Misheni ya Ufaransa Lyon mwaka 2024, alisema: “Leo, miujiza ya ukuaji inaendelea huko Corsica, licha ya sumbufu mbalimbali. Katika mwaka 2024, waumini 14 wa Tawi la Bastia walisafiri kwenda Hekalu la Paris Ufaransa kufanya kazi nyingi za hekalu kwa siku kadhaa, kundi kubwa zaidi kuwahi kusafiri kutoka kisiwa hiki cha mbali cha Mediterania kwenda hekaluni. Kwa msaada wa wamisionari waandamizi wanandoa na wazee na akina dada watano wenye nguvu, Bwana anaendelea kubariki kisiwa hiki cha paradiso na waongofu wapya.

Muhtasari

  1. Ona Théophile Larcher, “30 Years On: Remembering France’s Furiani Football Disaster,” The Connexion, Mei 5, 2022, connexionfrance.com.