Liahona
Safari Yetu kuelekea Nyumba Nzuri ya Mungu, Hekalu
Januari 2026 Liahona


Sauti za Wanachama

Safari Yetu kuelekea Nyumba Nzuri ya Mungu, Hekalu

Peter Moses Gimeyi Ndigavania na Concy Mundrua Kadabara, kutoka Tawi la Wanyange huko Kigingi cha Jinja Uganda, ni wanandoa wa kwanza kuunganishwa kwenye Hekalu la Nairobi Kenya

Sote, [mimi na mume wangu], tangu tulipojuana, kupendana na kuelewana, tulitamani kutumia muda wa maisha yetu pamoja. Tukiwa na furaha kuwa sehemu ya injili ya urejesho, tulijua itakuwaje, na tulijitahidi kufikia lengo letu hilo.

[Safari yangu ya injili ilianza] mchana mmoja mtulivu nilipokuwa nikimsaidia binamu wangu mdogo, Tracy, kuoga, nilimtafuta mahali alipozoea kucheza lakini sikumpata. Nikiwa nimekanganyikiwa, nilimuuliza dada yangu mkubwa, Santa, na alinielekeza kwa jirani ambako nilimkuta akicheza na msichana mdogo, Promise na kaka yake, Byron, familia ya Bw. na Bi. Ondoga. Walikuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo ambao baadaye waliwaelekeza wamisionari kwenye nyumba yetu.

Mchana huo nilipojilaza kwenye kochi pasipo kazi yoyote, niliona kijitabu ambacho kina kichwa cha habari “Ono la kwanza la Joseph Smith”. Kilichochea hamu yangu hivyo nilikisoma, lakini baada ya kukimaliza, nilikuwa na kila aina ya mawazo yakizunguka katika kichwa changu ikijumuisha [swali], “Ni kwa jinsi gani mtu angeweza kuandika kitu cha kugusa kweli na kutengeneza picha nzuri ya kuwashawishi watu?” Hata hivyo, kulikuwa na wazo lililong’ang’ania lenye nguvu na liliendelea kujirudia, kwamba ilikuwa kweli, hasa mstari [katika Moroni 10:4-5] ambao ulisema

“Na mtakapopokea vitu hivi, ningewashauri kwamba mngemwuliza Mungu, Baba wa Milele, katika jina la Kristo, ikiwa vitu hivi si vya kweli; na ikiwa mtauliza na moyo wa kweli, na kusudi halisi, mkiwa na imani katika Kristo, atawaonyesha ukweli wake kwenu, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

“Na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu mtajua ukweli wa vitu vyote.”

Mstari huu ulinivutia sana kuliko mstari mwingine niliokutana nao. Nimekwepa masomo mengi ya wamisionari, lakini baada ya hili nilianza kuhudhuria masomo pamoja nao, na daima walisisitiza kwenye mstari huo. Hilo liliniingia kwa nguvu sana walipokuwa wakitusaidia kuelewa sauti mbalimbali katika vichwa vyetu, na sauti ya Roho Mtakatifu, na zawadi yake ya upendo, faraja na amani, miongoni mwa mengine.

Nilikuwa na hisia kubwa ya kutenda juu ya mstari huo, hivyo asubuhi moja, baada ya kazi za nyumbani, nilishawishiwa kuingia katika chumba nilichowahi kuishi pamoja na dada zangu na kuwa na muda wa peke yangu na kusali kwa dhati kwa Baba yangu wa Mbinguni ili kujua kama vitu nilivyofundishwa ni vya kweli. Nilipofanya hivyo, nilihisi utulivu, amani katika moyo wangu, na sauti zote zenye kelele nilizokuwa nazo awali zilitoweka kimya kimya na kupotea. Nilihisi hisia ya furaha pia. Badaaye, nilipokutana na wamisionari, walinisaidia kuelewa kwamba ilikuwa ni uthibitisho wa ukweli [wa injili] kutoka kwa baba yetu wa mbinguni.

Baada ya mwaka, mnamo Machi 13, 2011, mimi pamoja na dada yangu Agnes tulibatizwa kama waumini wa Kanisa na kaka yetu Emmanuel ambaye alibatizwa kitambo kuliko sisi tulipokuwa tukisubiri wazazi watoe kibali. Ilikuwa ni siku tuliyoitazamia sana kwa sababu ilionekana kutowezekana. Hii ilikuwa ni kwa sababu tumetokea kwenye familia ambayo wazazi wetu walitokana na uzazi wa Wakatoliki, na ilikuwa ni kama miiko kubadili kutoka kwenye dini ya wazazi wetu.

Hata hivyo, Bwana hufanya vitu katika njia za ajabu na baada ya [ubatizo wangu] … ndugu zangu wengine pia walikuwa waumini, na kaka … yangu Stephen, baadaye alitumikia misioni huko Harare, Zimbabwe. Baada ya kurejea kwake alikuwa ni uvuvio kwangu, baada ya kuona jinsi ambavyo injili imemfanya kuwa mtu mwema. Nilitamani sana kulipata hilo, … na kumtumikia baba yangu wa mbinguni, nikiangalia baraka zote nilizopokea.

Baada ya somo zuri la Rais wangu wa Wasichana, Dada Dianna, kuhusu baraka za kipatriaki, nilivutiwa kupata baraka zangu za kipatriaki ili kuongoza maisha yangu, hivyo niliongea na Askofu wangu, kisha badaye niliweka miadi na Patriaki wangu. Hatimaye nilipokea baraka yangu ya kipatriaki. Ilikuwa ni uzoefu mzuri nilipokuwa nikimsikiliza Patriaki Jiles akitamka baraka hizo juu ya kichwa changu.

Septemba 2019, vigingi vya Uganda vilipanga programu ya Kwa Ajili ya Vijana (KNV) ambako mimi pamoja na mume wangu Peter tulikutana. Baada ya kurejea kutoka kambi hiyo tulianza kufanya miadi na niligundua kwamba yeye alikuwa tu ndio amerejea nyumbani kutoka Misioni yake ya Kenya, Nairobi ambayo ilijumuisha sehemu ya Tanzania pia. Anatokea kwenye familia nzuri ya waumini ambapo mama yake, Jessca amemkuza kama mcha Mungu, mnyenyekevu, mwenye upendo, kijana mtiifu, pamoja na baba yake, Mbiro, ambaye alikuwa akihudumu kama Rais wa Kigingi wakati huo.Ni lipata fursa ya kukutana nao, walikuwa ni watu wenye upendo ikijumuisha ndugu zake pia, kwani yeye alikuwa mzaliwa wa kwanza. Hiyo ndio familia niliyoitaka, kuishimo na kujenga humo siku moja. [Familia] inayomtumikia Bwana, ikiwafundisha watoto wake kanuni za injili, wakijitahidi kuishi kanuni za injili, na kufanya maagano matakatifu hekaluni.

Peter alikuwa muujiza kwangu, na alikuwa ni sehemu ya fumbo inayokosekana kwangu. Mara moja tuliweka malengo na tulishiriki malengo yetu na matamanio. Hii ilijumuisha hamu yangu ya kutumikia misioni, ambayo nilimjulisha, na kwa dhati alinisaidia, na [nilihisi] ni fursa nzuri ya yeye kujiandaa, kwani ndio alikuwa amemaliza misioni yake. Pia tulipanga kuoana baada ya mimi kurejea kutoka misioni [yangu].

Mnamo 9 Desemba 2021, nilienda misioni, niliitwa kutumikia huko Ghana, Kumasi na nilirejea mnamo Mei 2023.

Baadaye tuliweka mipango ya ndoa yetu. Tuliposana mnamo 31 Septemba 2023, katika ndoa ya kimila, na baadaye ndoa ya kanisa mnamo 28 Novemba 2023. Ilikuwa vyema kuona mipango na ndoto zetu zikitimia, lakini bado tulihitajika kuunganisha ndoa yetu katika nyumba takatifu ya Bwana, hivyo tulianza kupanga na kufanyia kazi lengo letu, kwani ilikuwa ni ahadi mojawapo iliyowekwa kwenye baraka zetu za kipatriaki.

Maisha yalijaa kazi na vitu vingine na, kwa muda, tulighairi lengo letu la kuunganishwa, mpaka tukio la kusikitisha na la huzuni lilipotokea mnamo 8 Februari 2025, ambapo nilimpoteza mama yangu. Lilikuwa ni jambo la huzuni, familia zilihuzunika, hisia za upotevu zikipita hapa na pale. Baada ya msiba wa mama yangu, Rebecca, mambo yalikuwa magumu sana. Nilikuwa nikipata ndoto kuhusu yeye na mume wangu, na ningeamka, na kusali kwa ajili ya faraja na nafsi yake kupumzika kwa amani.

Bado nilipata ndoto hizo, mpaka nilipomuomba mume wangu kunipa baraka, ambayo kwa furaha aliitoa. Katika siku hiyo, nilihisi pia hisia ya nguvu ya kuwasilisha jina lake hekaluni kwa ajili ya ibada, kwani hakuwa muumini. Baada ya kufanya hili nilihisi kufarijiwa, na ndoto endelevu kuhusu yeye ambazo zilinifanya niwe mwenye huzuni na wasi wasi zilikoma. Nilihisi nilipata ndoto hizo kama ukumbusho kwangu wa kufanya sehemu yangu kwa kufanya ibada kwa ajili yake.

Jioni moja nzuri baada ya chakula cha usiku, Peter aliniambia kuhusu kurejea Kenya kwa rais wake wa misioni kutokea Afrika Kusini, na jinsi alivyokuwa akipanga muungano tena wa wamisionari waliotumikia katika misioni ya Kenya Nairobi katika kipindi chake. Hii ilikuwa kuelekea ufunguzi na uwekaji wakfu wa hekalu la Kenya Nairobi. Pia aliniambia jinsi ambavyo hili lingekuwa fursa kubwa ya kwenda na kuunganishwa, tukiwa tunaenda kwa ajili ya muunganiko huo. Niliridhia na sote tukaanza kujiandaa. Peter pia alimuomba rais wetu wa misioni kusimamia uunganishaji wa ndoa yetu, kwa furaha alikubali na akatuwekea miadi ya tarehe 20 Mei 2025 kama tarehe za kuunganishwa kwetu.

Kuelekea tarehe hizo tulipokea simu kwamba uwekaji wetu nafasi ya malazi ulikubalika; hata hivyo, usafiri haukuwezekana, ilibidi tufanye hilo sisi wenyewe, au uwekaji wetu nafasi usogezwe hadi Juni. Ilikuwa ni jioni yenye huzuni kwani ilikuwa tayari ni Ijumaa, na kabla ya Jumatatu tulitakiwa kuwa Kenya kwa ajili ya miadi yetu.

Tulikwama kwenye jinsi ya kujisafirisha wenyewe. Ilibidi tusubiri uthibitisho wa mwisho siku ya Jumamosi jioni, ambao ulidhihirisha kwamba haikuwezekana kwetu sisi kusafiri. Hatukuweza hata kwenda benki na kujaribu kupata pesa kwa ajili ya safari kwa sababu muda wa kazi unaisha Jumamosi mchana, na kuendelea Jumatatu, siku tuliyotakiwa kuwa Kenya.

Ilikuwa ngumu sana kwetu na kwa muda hatukujua nini cha kufanya. Tulipiga magoti baada ya chakula cha usiku na kuomba. Peter alitoa sala na alipokuwa akihitimisha alisema, “Baba wa mbinguni, tunaweka matakwa yetu katika mikono yako, hata ya kwenda hekaluni kuunganishwa katika nyumba yako takatifu, lakini sio mapenzi yetu bali yako yatendeke, Amina.” Dakika chache baada ya hili ndipo tulipoona mkono wa Bwana. Rafiki, aliyekuwa akijua tutasafiri, aliuliza kuhusu safari yetu kwa mume wangu, na mume wangu alishiriki changamoto tuliyonayo. Tulijua kidogo kuhusu mpango wa Bwana kwetu.

Bwana hutumia watoto wake kubariki maisha ya wengine. Tulipokea zawadi ya nauli yeta kupitia muamala wa simu, na nilianza kujiandaa usiku huo. Siku iliyofuata, baada ya kuhudhuria mkutano wa sakramenti, tulikata tiketi ya basi la jioni kuelekea Kenya ambalo liliondoka saa 11 jioni, na kufika Kenya Nairobi saa 10 alfajiri, kwenye muda muafaka wa kuhudhuria muunganiko wa wamisionari mchana huo pamoja na rais wa zamani wa misioni wa mume wangu, ambaye ni Mzee Ephraim Msane, Sabini wa Eneo.

Mnamo Mei 20, 2025, saa 3 asubuhi, mimi pamoja na mume wangu mpendwa, Peter tuliingia hekaluni. Ilikuwa ni siku tuliyoitazamia na amani na uzuri kote, tulipokuwa tukitembea kuelekea chumba cha kuunganishia, ulikuwa unapita maelezo yote ninayoweza kutoa. Nilipopiga magoti kwenye madhabahu, nikimuangalia mume wangu, na kusikiliza baraka zikitajwa na kuunganishwa kwa milele yote na Rais Sham Omondi, mbele ya marafiki zetu na rais wa zamani wa misioni, familia katika roho (kwani hawakuweza kusafiri pamoja nasi), na zaidi ya yote, mbele ya Baba wa Mbinguni, ilikuwa ni kila kitu kwetu.

Kuwa katika hali ya kuhisi hakikisho la Bwana katika chumba cha selestia na kujua kwamba niliweza kupata hakikisho la roho baada ya kufanya ibada kwa niaba ya wafu, ikijumuisha mama yangu, ilikuwa ni hisia nzuri.

Tulikuwa na hakikisho la mkono wa Bwana katika maisha yetu, na nguvu wezeshi ya Mwana, Yesu kristo, ya kushinda majaribu yamkini katika maisha yetu.