Liahona
Kufanya Maagano ya Bwana Yaandikwe katika Mioyo Yetu
Januari 2026 Liahona


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Kufanya Maagano ya Bwana Yaandikwe katika Mioyo Yetu

Miaka mia sita kabla ya Kristo, Nabii Yeremia alitabiri kwamba katika “siku zijazo”, Bwana “atafanya agano jipya na nyumba ya Israeli …[na] nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” (Yeremia 31:31-33; msisitizo umeongezwa).

Urejesho wa utimilifu wa injili kupitia Nabii Joseph Smith hujumuisha agano jipya na lisilo na mwisho lililoahidiwa na Yeremia (M&M 66:2). Agano ni jipya kwa sababu lilirejeshwa katika siku zetu na halina mwisho kwa sababu ni agano lile lile ambalo Mungu ametoa kwa watoto wake katika kila kipindi katika historia yote ya dunia (Ona, Mwongozo wa Maandiko, “Agano Jipya na Lisilo na Mwisho,” Maktaba ya Injili).

Mungu hutoa agano jipya na lisilo na mwisho na ahadi zake kwa watoto Wake wote. Hata hivyo, Yeye hatamshurutisha yeyote kufanya agano pamoja naye. Kila mmoja lazima achague kukubali agano na kudhihirisha kwa kushiriki katika ibada zilizotajwa na Bwana. Ibada hizi hujumuisha ubatizo, Kipawa cha Roho Mtakatifu, utawazo wa ukuhani kwa wanaume, endaumenti ya hekaluni na kuunganishwa. Tunachagua kuandika maagano na sheria za Mungu ndani ya mioyo yetu kwa hiyari kujiandaa na kwa kustahili kupokea kila ibada ya injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo.

Ubatizo na Njia ya Agano

Waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wameingia kwenye agano na Mungu kupitia ibada za ubatizo na uthibitisho. Kila mmoja ameingia njia ya agano na kuanza safari kurejea kwenye uwepo wa Bwana. Nguvu ya utakaso ya upatanisho wa Yesu Kristo na mwongozo wa Roho Mtakatifu huwapa waumini uwezo wa agano na nguvu ya kutunza amri za Mungu na kubakia kwenye njia inayoongoza kwenye maagano mengine ambayo ni sehemu ya agano jipya na lisilo na mwisho. Tunatunza maagano yetu yaliyoandikwa kwenye mioyo yetu kwa kushiriki sakramenti kila wiki.

Kufokasi kwenye Nyumba ya Bwana

Baada ya kubatizwa, tunaweka malengo yetu ya kukuza uanafunzi wetu kwa kupokea ibada za Nyumba ya Bwana. Mbele ya kila hekalu yameandikwa maneno “Utakatifu kwa Bwana, Nyumba ya Bwana.” Bwana humwalika kila muumini wa Kanisa kujiandaa na kwa kustahili kupokea baraka maalum zinazopatikana kupitia maagano yanayofanywa katika Nyumba Yake Takatifu pekee. Waumini wa Kanisa wenye miaka 18 na wamebatizwa kwa angalau mwaka mmoja wanafaa kupokea ibada zao za hekaluni. Wale wa miaka 11 na zaidi wanaweza kuingia hekaluni kufanya ibada kwa niaba ya mababu waliofariki.

Waumini wote wanaweza kufanya agano la Mungu kuandikwa katika moyo wao kwa:

  1. Kupokea na kuwa na kibali halali cha hekaluni katika maisha yao yote

Kila muumini wa miaka 11 na zaidi, ikijumuisha waliobatizwa karibuni, wanaweza kupokea kibali kwa kupanga mahojiano na askofu.Tunastahili kupokea kibali kama tunaishi sheria za Mungu ambazo tulijifunza na kuweka agano kuzitii wakati wa ubatizo wetu. Kuwa na kibali ni ukumbusho kwamba tumeahidi kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo na kuishi amri za Mungu. Kuwa na kibali halali cha hekaluni ni ukumbusho wa mara kwa mara wa maagano yetu na Mungu.

  1. Kujifunza kuhusu hekalu na ibada zake

Waumini wapya na wa zamani wanapaswa kujifunza kuhusu hekalu, ibada zake na maagano yanayohusiana na ibada hizo kuwa sehemu ya mafunzo yao ya injili hasa wanapojiandaa kufanya maagano yao wenyewe. Aplikesheni ya Gospel Library hujumuisha nyenzo nyingi saidizi kwenye kipengele cha “Hekalu na Historia ya Familia”. Nyenzo hizi hutusaidia kuelewa umuhimu na utakatifu wa mahekalu na vitu tunavyohitaji kubadilisha katika maisha yetu tunapojiandaa kutembelea Nyumba ya Bwana. Sehemu ya 27 katika Kitabu cha Maelezo ya Jumla, kwenye kipengele, Vitabu vya Maelekezo na Miito inaweza kutupatia uelewa wa kina wa ahadi na maagano tutakayofanya. Jitihada za dhati na za kweli za kujifunza kuhusu hekalu na ibada zake zitatusaidia kuelewa umuhimu wa hekalu na nguvu tunayoweza kupokea ya kustahimili magumu ya maisha na kurejea kwenye uwepo wa Mungu kwa kupitia ibada za hekaluni. Mafunzo ya hekalu na ibada zake vitasaidia kuandika maagano ya Mungu kwa kina katika mioyo yetu.

  1. Kutafuta majina ya mababu na kuwasaidia wao kupokea ibada za hekaluni

Moja ya kweli kuu zilizofunuliwa kama sehemu ya urejesho ni kwamba Mungu ameandaa njia kwa ajili yetu ya kuwabariki na kuwasaidia mababu zetu waliofariki kupokea baraka kamili za injili iliyorejeshwa kwa kufanya ibada muhimu kwa ajili yao katika Mahekalu Matakatifu. Tunapowabainisha mababu waliofariki na kupangilia taarifa kuhusu maisha yao (tarehe za kuzaliwa, ndoa, kifo, majina ya watoto, n.k) katika aplikesheni ya FamilySearch daima tutakumbushwa kuhusu maagano ya Mungu.Tunapohudhuria hekaluni kwa mara ya kwanza, tunaingia kwenye maagano na Mungu. Kisha, tunaweza kuwa kama wakala ili kuwasaidia mababu zetu kupokea ibada zao. Kuna wengi wanatusubiri sisi katika ulimwengu wa kiroho kufanya ibada kwa niaba yao. Nakuahidi kwamba utahisi shangwe yao unapofanya ibada kwa niaba yao katika Nyumba ya Bwana. Kuwahudumia wao kutafanya maagano ya Bwana kupandwa kwa kina katika mioyo yetu.

  1. Hudhuria hekalu mara nyingi kadiri hali inavyoruhusu

Kila muumini wa Kanisa anaweza kuhudhuria hekalu angalai mara moja ili kupokea ibada zao. Baada ya kutunza na kutoa dhabihu kile ambacho mtu anaweza, Kanisa linaweza kutoa msaada kupitia Mfuko wa Jumla wa Msaada wa Mhudhuriaji Hekaluni (GTPAF). Kadiri mtu alivyo tayari kutoa dhabihu kuhudhuria hekalu, ndivyo kwa kina atahisi nguvu ya maagano yaliyofanywa pamoja na Mungu. Kila mara mtu ahudhuriapo, maagano yataandikwa kwa kina zaidi na zaidi katika mioyo yao. Kila wakati mtu afanyapo ibada kwa niaba ya wengine, mtu huyo atakuwa karibu zaidi na Mungu na kuhisi kipimo kikubwa cha upendo Wake na nguvu.

Babu yangu mkuu, Heinrich Friedrich Christian Pieper, alibatizwa katika miaka yake ya 20 huko Ujerumani mnamo 1895. Kama muumini mpya, alijifunza kuhusu hekalu na alianza maandalizi ya kupokea ibada zake katika Nyumba ya Bwana. Kwa sababu hakukuwa na hekalu karibu yake, ilipita miaka saba kabla ya yeye kutimiza ndoto yake. Kwa kipindi hicho, alikuwa ameoa na aliweza kupokea endaumenti na kuunganishwa mnamo 1902. Sasa alikuwa anaishi umbali wa lisaa limoja hadi hekaluni na alifanya kazi kwa bidii kuandaa majina ya mababu. Yeye pamoja na mkewe walitembelea Nyumba ya Bwana mara nyingi ilivyowezekana ili kubanya ibada za uwakilishi kwa wale wawapendao. Mpaka 1952, yeye pamoja na mkewe walikuwa wamefanya zaidi ya ibada 20,000 kwa ajili ya wengine.

Kama Yeremia alivyotabiri, agano lililorejeshwa liliandikwa kwa kina kwenye mioyo ya babu yangu mkuu na bibi yangu mkuu na, kama matokeo, katika maisha yangu na vizazi vingine. Huduma zao za hekaluni ziliwapa nguvu za kuvumilia changamoto nyingi za maisha na kubakia waaminifu kwa Mungu wao.

Nabii wetu aliye hai ametufundishwa kwamba hekalu ni kitovu muhimu cha nguvu za kiroho tunazohitaji kukabiliana na majaribu na changamoto za ulimwengu unaotuzunguka. Ninashuhudia kwamba tunapofanya Nyumba ya Bwana na maagano ya hekaluni kuwa kipaumbele chetu cha muhimu zaidi kwa kuwa na kibali, kujifunza kuhusu hekalu na ibada zake na kuzipokea kwa ajili yetu wenyewe, kisha kuwasaidia mababu zetu kupokea ibada kupitia mahudhurio ya mara kwa mara, tutahisi upendo wa agano la Mungu kwa ajili yetu na kuwa na nguvu inayohitajika kukabiliana na changamoto katika maisha yetu.