Baba yako wa Mbinguni Anataka Kuzungumza Nawe
Uwe na imani kwamba Baba yako wa Mbinguni anazungumza nawe. Yupo pale na anakupenda zaidi ya maneno yanavyoweza kusema.
Sisi ni wana na mabinti wa Mungu, tukiwa hapa duniani pamoja na tukiwa mbali kutoka nyumbani kwetu mbinguni. Haya ni maisha ya duniani, wakati wa kupokea mwili wetu, kuchagua mema dhidi ya uovu, kukuza imani yetu katika Mwokozi wetu Yesu Kristo na Upatanisho Wake mtakatifu, na kukumbatia mpango wa furaha wa Baba yetu.
Bila kumbukumbu ya maisha yetu kabla ya kuja duniani, sisi, wakati mwingine, tunahisi upweke kwa ajili ya ulimwengu tuliouacha nyuma. Baba yetu ametupatia zawadi ya kiroho ya kubaki tumeunganishwa Kwake na kupokea mwongozo, maelekezo, na faraja kutoka Kwake. Tunaijua zawadi hii vizuri sana; inaitwa sala.
Kwa Wale Watakaoniamini Mimi, na Dan Wilson,
Sali kwa Baba yako wa Mbinguni.
Malaika aliwaamuru Adamu na Hawa na wote ambao wangewafuatia “kutubu na kumwita Mungu katika jina la Mwana milele yote” (Musa 5:8).
Yesu alifundisha:
-
“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa” (Mathayo 7:7).
-
“Unaposali, … sali kwa Baba yako … kwa siri” (Mathayo 6:6).
-
“Basi ninyi salini hivi: Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe” (Mathayo 6:9).
Yesu alisali daima kwa Baba Yake (ona Luka 6:12; Marko 6:46). Gethsemane, Aliwaambia wanafunzi Wake, “Ketini hapa, muda niombapo” (Marko 14:32). Akiwa msalabani, Yesu aliwaombea askari waliomsulubisha: “Baba, uwasamehe; kwa kuwa hawajui watendalo” (Luka 23:34).
Tunashauriwa “kusali daima.” Wakati “tunaposhauriana na Bwana katika matendo [yetu] yote, … yeye [atatuongoza] kwa yale mema” (Alma 37:37). Kwa nyongeza, “tunatoa shukrani zote na sifa ambazo nafsi [zetu] zina uwezo wa kuwa nazo” (Mosia 2:20).
Lakini lililo tukufu zaidi, Baba yetu wa Mbinguni hujibu sala zetu! Swali la kutafakari kwetu ni jinsi gani tunapokea vyema na kuelewa majibu, maelekezo, na faraja inayotoka kwa Baba yetu?
Kupokea majibu ya sala zetu huanza na imani katika Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo. Tunamwamini Baba yetu, tunafanya kwa uwezo wetu wote kushika amri, na kutafuta mkono Wake katika mambo yote (ona Mafundisho na Maagano 59:21).
Baba yako wa Mbinguni atasimama karibu nawe, ataimarisha uwezo wako, kukufariji, na “kuweka wakfu masumbuko yako kwa faida yako” (2 Nefi 2:2) unapomlingana Yeye.
Sikiliza Sauti Yake
Tunapoonesha imani katika Mungu na kutii amri Zake, kiuhalisia tunajifunza kuisikia sauti Yake vizuri zaidi.
Mnamo 1993, Rais James E. Faust (1920–2007), wakati huo akiwa mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alitualika mimi na mke wangu, Kathy, kuhudhuria ibada katika Chuo Kikuu cha Brigham Young pamoja naye. Ibada hii ilitokea mapema kabla ya kuenea kwa upatikanaji wa simu janja, mitandao ya kijamii, na intaneti.
Katika hotuba yake, Rais Faust alionya: “Katika kizazi chenu mtazuiliwa na mfululizo wa sauti nyingi zikikuambieni jinsi ya kuishi, jinsi ya kuridhisha tamaa zenu, jinsi ya kupata yote.” Lakini “sauti ambayo lazima mjifunze kuitii ni sauti ya Roho.” Ili kufanya hivyo, “sisi … lazima tufungue masikio yetu, tugeuze jicho la imani kuelekea chanzo cha hiyo sauti, na tutazame kwa uimara kuelekea mbinguni.”
Miaka kadhaa baadaye, Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Ikiwa unazingatia zaidi malisho kutoka kwenye mitandao ya kijamii kuliko ilivyo kwa minong’ono ya Roho, basi unajiweka katika hatari ya kiroho.”
Sauti ya Roho inakuja katika akili zetu na hisia zetu. “Nitakujulisha wewe akilini mwako na katika moyo wako, kwa njia ya Roho Mtakatifu, ambaye atakujia na ambaye atakaa moyoni mwako” (Mafundisho na Maagano 8:2) Sikiliza dhamiri yako—ufunuo mara nyingi huanzia huko.
Sali kwa Moyo wa Kuamini
Majibu na misukumo kutoka kwa Mungu haiwezi kulazimishwa. Tunasali na kungoja kwa moyo wa kuamini. Baadhi ya majibu hayatakuja katika maisha haya, lakini kwa wenye haki, Bwana daima atatuma amani Yake (ona Yohana 14:27). Wakati mwingine, majibu huja “mstari juu ya mstari, kanuni juu ya kanuni” (Mafundisho na Maagano 98:12).
Sauti ya mbinguni inaweza kuja bila kutarajia mara nyingi katika nafasi tulivu na mahali patakatifu. Katika utulivu wa sala zangu za mapema asubuhi na kutafakari, ninapata baraka zisizo za kawaida. Usomaji binafsi, wa maandiko kila siku, usiokatizwa, wakati mwingine, unaweza kuleta sauti ya Roho ndani ya mioyo yetu kama moto wakati mwingine.
Wakati kelele na vivuruga mawazo vya dunia vikituzunguka, Bwana amemwelekeza nabii Wake kujenga mahekalu zaidi na zaidi. Katika nyumba hizi takatifu za Bwana, tunapoacha changamoto zetu nje na kuingia kwa sala na maswali yetu, tunafundishwa kweli za milele. Mwaka mmoja uliopita, Rais Nelson aliahidi kwamba tunapoabudu hekaluni, “Hakuna kitakachofungua mbingu zaidi. Hakuna!”
Kila mkutano mkuu pia huleta baraka tele za ziada. Katika mwezi ujao wa Aprili, tutakutana tena katika mkutano mkuu ili kusikia sauti ya Bwana. Ninaahidi kwamba unapojiandaa na kuja kwa sala kwenye mkutano mkuu, utapata majibu ya maswali yako na kujua kwamba “mkono wa mbinguni” u juu yako.
Kuwa na imani kwamba Baba yako wa Mbinguni anazungumza nawe. Yeye yupo! Ruhusu imani yako Kwake na kwa Mwanawe Mpendwa ikusaidie kulifunua pazia na kupokea sauti ya Baba yako. Ninashuhudia Yeye yupo na anawapenda zaidi ya maneno yanavyoweza kusema.