Rafiki
Mazungumzo na Emily kuhusu Ubatizo
Januari 2026 Rafiki


“Mazungumzo na Emily kuhusu Ubatizo,” Rafiki, Januari 2026, 34–35.

Mazungumzo na Emily kuhusu Ubatizo

Emily ni wa umri wa miaka 9 kutoka Sinaloa, Mexico. Tulimuuliza maswali kadhaa kuhusu ubatizo wake.

Tuambie kuhusu wewe mwenyewe.

Ninapenda kupaka rangi, kuchora, kuoka kitindamlo, kutengeneza sanaa za kiufundi, na kucheza dansi na kuimba pamoja na ndugu zangu. Pia ninapenda kwenda kwenye shamba la mifugo la babu yangu kupanda farasi.

Emily akiendesha farasi

Je, ulijiandaa kwa jinsi gani kwa ajili ya kubatizwa?

Wakati wa jioni ya nyumbani, wazazi wangu walinifundisha kuhusu imani, toba, ubatizo, na kipawa cha Roho Mtakatifu. Pia nilijiandaa kwa kusoma maandiko, kusali, na kuangalia video kuhusu Yesu Kristo. Ninapenda hasa video kuhusu ubatizo wa Mwokozi katika Mto Yordani. Ninapenda sehemu wakati njiwa mweupe anapotokea, ambayo inawakilisha Roho Mtakatifu.

Baba yangu pamoja nami pia tulifanyia mazoezi jinsi ambavyo tungesimama kwenye kisima. Niliogopa kwenda chini ya maji, lakini baba yangu alinifundisha jinsi ya kupinda magoti yangu, kufunika pua yangu, kufunga macho yangu, na taratibu kuanguka mikononi mwake. Tulifanya mazoezi haya mengi, na siku ya ubatizo wangu, niliweza kufanya hivyo kwa urahisi sana.

Ni nini kilikuwa maalumu kuhusu ubatizo wako?

Emily na baba yake katika kisima cha ubatizo

Ilikuwa siku isiyosahaulika kwangu. Baadhi ya wanafamilia yangu walitoa hotuba, wakasema sala, na kusimama kama mashahidi. Pia niliimba “Ninapobatizwa” kwa msaada wa mpiga kinanda wetu wa Msingi. Baada ya kubatizwa, nilihisi Baba yangu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, karibu sana nami. Nililia machozi ya furaha.

Ilikuwa pia maalumu kwa sababu nilikuwa na wazo la kuwaalika baadhi ya marafiki zangu na wanafamilia ambao si waumini wa Kanisa kuja kwenye ubatizo wangu, na walikubali kuja. Mmoja wa rafiki zangu aliyehudhuria bado anakuja kwenye shughuli za kanisa pamoja na wazazi wake.

Ni kwa jinsi gani unayakumbuka maagano yako ya ubatizo?

Ninajitahidi kukumbuka maagano yangu kwa kwenda kanisani, kupokea sakramenti, na kumkumbuka Mwokozi. Kujua kwamba Yeye alitoa uhai Wake kwa ajili yangu hunifanya nihisi shukrani. Pia ninasali kila siku, kusoma maandiko, kuwahudumia wengine, na kujitahidi kuwa mtu mwema.

Kwa marafiki zangu ambao wako karibu kubatizwa, natumaini mnaweza kuwa karibu na Baba wa Mbinguni na kuhisi upendo Wake mkamilifu!

Emily na mama yake wakikumbatiana