Rafiki
Tayari Kutembea pamoja na Yesu
Januari 2026 Rafiki


“Tayari Kutembea pamoja na Yesu,” Rafiki, Januari 2026, 4–5.

Tayari Kutembea pamoja na Yesu

Wasichana mapacha wakiwa wameshikilia nakala ya toleo la Ubatizo na Uthibitisho la jarida la Rafiki

Habari!

Sisi ni Hailey na Violet, akina dada mapacha kutoka Arizona, Marekani. Tunataka kufuata mfano wa Mwokozi, kwa hiyo tunajiandaa kubatizwa!

Wasichana wamesimama ndani ya mto pamoja na mama na baba yao

Tunapenda kutembea kando ya mto karibu na nyumba yetu. Tunapobatizwa, tutaanza matembezi mapya ya kiroho pamoja na Yesu! Roho Mtakatifu atakuwa pamoja nasi tunapojaribu kumfuata Mwokozi kila siku.

Wasichana wakikusanya maganda kwenye ukingo wa mto

Wakati mwingine tunakusanya maganda madogo meupe kando ya mto. Yanatukumbusha juu ya kitu ambacho Mwokozi aliahidi: “Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji” (Isaya 1:18). Kwa sababu ya Yesu Kristo, tunaweza kutubu na kuwa wasafi tena baada ya kufanya uchaguzi mbaya. Tutavaa mavazi meupe siku yetu ya ubatizo ili kukumbuka hili pia.

Wasichana wakiruka mawe mtoni na baba yao

Baba yetu kwa kweli ni mzuri katika kuruka mawe mtoni! Anatufundisha jinsi ya kufanya hivyo, na tunakuwa bora kidogo kila wakati tunapojaribu. Hivi ni kama vile Yesu Kristo alivyo Mwalimu mkamilifu. Yeye anataka kutusaidia kujifunza na kukua.

Wasichana wakitembea mtoni wakiwa wameshikana mikono na mama yao

Mawe ndani ya mto yanateleza, na inasaidia kushikilia mkono wa mama yetu. Yesu daima yupo kwa ajili yetu wakati tunapohitaji msaada. Na tunapobatizwa, tutaahidi kuwasaidia wengine jinsi ambavyo Yeye angefanya!

Tunapenda kutembea kandokando ya mto pamoja na familia yetu. Tunapobatizwa, tutakuwa kwenye njia ya agano ambayo inaongoza kurudi nyumbani kwetu mbinguni. Tunaweza kuwa na familia yetu milele!

Ninasisimka kubatizwa kwa sababu ninataka kufuata mfano wa Yesu. Ninapata kumwonyesha Baba wa Mbinguni kwamba ninataka kutii amri.

Violet W., umri miaka 7, Arizona, Marekani

Ninataka kumfuata Yesu Kristo. Baada ya kubatizwa, ninaweza kumpata Roho Mtakatifu, na Roho Mtakatifu anaweza kunisaidia kuwa mkakamavu.

Hailey W., miaka 7, Arizona, Marekani