“Ibada za Hekaluni Zinaleta Umoja, Kuunganika, na Kuunganisha,” Liahona, Sept. 2025.
Mitazamo ya Kihistoria juu ya Nyumba ya Bwana
Ibada za Hekaluni Zinaleta Umoja, Kuunganika na Kuunganisha
Historia ya kazi ya hekalu katika siku za mwisho inaonyesha shauku na ufunuo wa mstari juu ya mstari kwa ajili ya ubatizo kwa niaba ya wafu.
Kielelezo na Dan Burr
Betsy King Duzette aliingia katika maji yaliyoganda ya Mto Mississippi. Mjane huyo mwenye umri wa miaka 58 na mwongofu kutoka Connecticut kisha alibatizwa kwa niaba ya wajomba zake, mama mkwe, na baba wa kambo wa mumewe.
Nabii Joseph Smith karibuni alikuwa amewafundisha Watakatifu, mnamo Agosti 1840, kuhusu mafundisho ya ubatizo kwa ajili ya wafu. Katika msisimko wao, walifanya ubatizo ndani ya mto, kwa vile Hekalu la Nauvoo halikuwa limekamilika. Wanawake walibatizwa kwa niaba ya wanaume na wanaume kwa niaba ya wanawake. Punde, hata hivyo, Bwana alifunua kwa Joseph Smith kwamba ubatizo kwa niaba ya mababu waliofariki lazima ufanyike katika mahekalu yaliyowekwa wakfu (ona Mafundisho na Maagano 124:28–35). Na mwaka 1845, Brigham Young alitangaza kwamba wanawake wanapaswa kubatizwa kwa niaba ya wanawake na wanaume kwa niaba ya wanaume.
Mume wa Betsy, Philemon Duzette, alikuwa amefariki miaka sita mapema. Aliyakabili kwa ujasiri maji ya baridi ili abatizwe kwa ajili ya jamaa zake waliofariki. Hiyo ilijumuisha ubatizo kwa ajili ya baba wa kambo wa Philemon, Jesse Peas, ambaye alifariki miaka 50 mapema wakati Betsy alipokuwa msichana mdogo. Huenda hakuwahi kukutana naye lakini kuna uwezekano alijua kumhusu yeye na alijua jina lake na uhusiano wake na Philemon na mama yake, Martha Wing. Betsy alikuwa amemjua Martha alipokuwa hai.
Betsy alibatizwa kama mwakilishi wa Jesse mara moja kufuatia ufunuo juu ya ubatizo kwa niaba ya wafu. Na yeye na mumewe walimwita mmoja wa watoto wao kwa jina la Jesse. Baba wa kibaolojia wa Philemon, pia aitwaye Philemon, alikufa alipokuwa mtoto mchanga, na Jesse Peas akawa baba yake wa kambo wakati Philemon alipokuwa na umri wa miaka mitatu na kumsaidia Martha kumlea.
Ulezi wa kambo ulikuwa kawaida katika Amerika ya karne ya kumi na nane na kumi na tisa. Viwango vya juu vya vifo na viwango vya juu vya kuoa tena vilimaanisha watu wengi waliishi katika familia za kambo au familia zenye mchanganyiko. Hivyo, uhusiano wa familia ya Duzette-Peas ulijengwa upya mara mbili: mara moja wakati mama wa Philemon alipoolewa na Jesse Peas na mara ya pili kupitia ubatizo kwa ajili ya wafu.
Mchoro wa kisima cha ubatizo katika Hekalu la Nauvoo
Kuwakomboa Wapendwa
Ubatizo kwa niaba ulileta miunganiko hiyo ya duniani pamoja katika njia ambayo ingedumu milele. Kama Joseph Smith alivyoandika, ubatizo kwa niaba ya wafu ni “muunganiko” ambao unafunga walio hai na wafu, “kwani sisi pasipo wao hatuwezi kukamilika; wala wao pasipo sisi hawawezi kukamilika” (Mafundisho na Maagano 128:18).
Joseph Smith alifundisha kwamba bila kiungo hiki cha weko, dunia ingepigwa kwa laana, kitu ambacho kingeifanya dunia kuwa takataka, iliyoumbwa bila kusudi (ona Mafundisho na Maagano 128:17–18). Dhidi ya tangazo hili la wazi lilikuwa ufunuo mtukufu wa Joseph kuhusu nguvu ya kuwaunganisha watoto wote wa Mungu pamoja milele.
Kwa kuongezea kwenye umuhimu wa ibada kwa niaba ya wanafamilia waliofariki, Joseph alisisitiza kwamba walio hai pia wanafaidika: “Na sasa, ndugu na dada zangu wapendwa, acha niwahakikishieni kwamba hizi ni kanuni zinazohusiana na wafu na walio hai ambazo haziwezi kupitishwa kwa wepesi, kulingana na wokovu wetu” (Mafundisho na Maagano 128:15).
Kwa Joseph Smith, funuo hizi zilikuwa za kibinafsi sana. Kaka yake mkubwa, Alvin, alikuwa amefariki mwaka 1823, na Joseph alihisi kupoteza katika maisha yake. Katika ufunuo wa mwaka 1836, Joseph alipata ono la “ufalme wa selestia wa Mungu, na utukufu wake” na “uzuri usio na kifani wa lango” na “mitaa mizuri ya ufalme huo.” Katikati ya ono hili kuu kuhusu ufalme wa selestia, pia aliwaona wanafamilia binafsi aliowajua na kuwapenda, ikijumuisha kaka yake Alvin. “Alistaajabu” kwamba Alvin, ambaye kamwe hakuwa amebatizwa, alikuwa “mrithi wa ufalme wa selestia wa Mungu.” Ona Mafundisho na Maagano 137:1–6.
Kabla ya Msingi wa Ulimwengu
Uhusiano kati ya wapendwa walio hai na waliofariki unaonyesha kiwango kikubwa cha wokovu wa mwanadamu, kwa wale “wanaokufa bila ufahamu wa injili” (Mafundisho na Maagano 128:5) wanajulikana na njia ya ukombozi wao iliyotolewa kabla ya kuja duniani. Hakika, ubatizo kwa ajili ya wafu ulianzishwa kwa ajili ya “wokovu wetu kutoka kabla ya msingi wa ulimwengu” (Mafundisho na Maagano 128:8). Ufunuo kuhusu ubatizo kwa ajili ya wafu ulifuatiwa na ufunuo wa baadaye kuhusu ibada za kuunganisha. Kuunganishwa kwa watoto na wazazi ikawa ibada ya kilele ambayo ilitoa viungo kwa ajili ya kila mtu aliyewahi kuishi (ona Mafundisho na Maagano 138:47–48).
Katika hotuba nzuri ya mkutano mkuu kutoka Aprili 2018, Mzee Dale G. Renlund wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alielezea nguvu ya muunganiko huo wa kuunganisha:
“Mungu, katika uwezo wake usio na mwisho, huunganisha na kuponya watu na familia licha ya majanga, vifo na magumu.
“… Kupitia dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Yesu Kristo anatoa baraka hizi kwa wote, wafu na walio hai.”
Kama vile Besty King Duzette alivyoamini na kutumaini alipoingia katika Mto Mississippi kwa niaba ya baba mkwe wake wa kambo, sisi, sote, tunaweza kuunganika, kuunganishwa, kufungwa, na kuunganishwa pamoja milele.