2025
Kubarikiwa kwa Mamlaka na Nguvu za Ukuhani
Septemba 2025


“Kubarikiwa kwa Mamlaka na Nguvu za Ukuhani,” Liahona, Sept. 2025.

Kubarikiwa kwa Mamlaka na Nguvu za Ukuhani

Waumini wa Kanisa hutumia nguvu za Mungu katika kuwahudumia na kuwabariki wengine katika Kanisa, nyumbani na kote ulimwenguni.

Mzee D. Todd Christofferson

Ushuhuda wetu kwa ulimwengu ni kwamba ukuhani mtakatifu wa Mungu ni muhimu katika kukamilisha kazi Yake ya wokovu na kuinuliwa, kwamba amerejesha ukuhani duniani kwa kusudi hilo, na kwamba unasimamiwa na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Umuhimu wa Mamlaka ya Ukuhani na Nguvu

Yesu Kristo ndiye kichwa cha Kanisa. Kanisa ni chombo alichokiunda ili kukamilisha kazi muhimu ya kuwakomboa wanadamu katika kipindi hiki cha mwisho cha injili kama vile katika kipindi cha maongozi ya Mungu alipoishi duniani. Kupitia Kanisa:

  • Anaweza kutangaza injili Yake kote ulimwenguni.

  • Anaweza kutoa ubatizo na maagano mengine yote—hata njia ya agano kuelekea ufalme Wake wa selestia.

  • Anaweza kuunganisha familia milele.

  • Anaweza kutoa karama za wokovu, hata kwa wale walio kufa bila ibada hizo.

  • Anaweza kuhudumia mahitaji ya kimwili ya watoto wa Mungu kwa sasa.

Ili kutimiza malengo haya makuu, na kujiandaa kwa ajili ya kurudi kwa Mwokozi, Kanisa linahitaji mwongozo endelevu, mamlaka endelevu na nguvu endelevu za Mungu. Kanisa hili ni “kanisa la kweli na lililo hai” (Mafundisho na Maagano 1:30) kwa sababu Kristo amelipatia uongozi Wake na nguvu kupitia ukuhani Wake, “Ukuhani Mtakatifu, kwa mfano wa Mwana wa Mungu” (Mafundisho na Maagano 107:3).

Lakini bila ukuhani huu mtakatifu, Kanisa kimsingi lingekuwa shirika la kidunia, likifanya mema ulimwenguni lakini lisiwe na uwezo wa kufikia lengo kuu la kuwatayarisha wana na mabinti wa Mungu kwa furaha ya uzima wa milele katika uwepo Wake. Kwa ukuhani huu, na funguo za kuongoza kazi ya ukuhani huu, kuna vyote mamlaka na utaratibu katika Kanisa.

“Katika Kanisa, mamlaka yote ya ukuhani yanatumika chini ya maelekezo ya wale ambao wanashikilia funguo za ukuhani.

“Waumini wa Kanisa wanaume wanaostahili wanapokea mamlaka ya ukuhani kupitia utunukiwaji wa ukuhani na kutawazwa kwenye ofisi za ukuhani. “Waumini wote wa Kanisa wanaweza kutumia mamlaka yaliyonaibishwa ya ukuhani pale wanaposimikwa au kupangiwa kusaidia kutimiza kazi ya Mungu.”

Kupitia funguo za ukuhani, vipaumbele vya Bwana daima vitashinda. Hakuna anayeweza kuidhinisha ajenda binafsi ambayo haiendani na maelekezo Yake. Hakuna anayeweza kufanikiwa katika ukuhani wa uongo, akitafuta faida binafsi na ufuataji wa mambo binafsi.

Ukuhani pia una jukumu muhimu katika nyumba za waumini wa Kanisa. Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alifundisha, “Kanuni ya kwamba mamlaka ya ukuhani yanaweza tu kutumika chini ya maelekezo ya yule ambaye ana funguo kwa ajili ya kazi hiyo ni muhimu katika Kanisa, lakini hii haitumiki katika familia.” Akina baba husimamia na kutumia ukuhani katika familia zao—kushauri, kufanya mikutano ya familia, kutoa baraka za ukuhani au uponyaji kwa wanafamilia au wengine, na kadhalika—bila maelekezo au idhini ya mtu anayeshikilia funguo za ukuhani.

“Kanuni kama hiyo hutumika pale baba akiwa hayupo na mama ni kiongozi wa familia. Mama anasimamia katika nyumba yake na ni chombo katika kuleta nguvu na baraka za ukuhani ndani ya familia yake kupitia endaumenti na kuunganishwa kwake hekaluni.”

Urejesho wa Ukuhani katika Siku Zetu

Yohana Mbatizaji akirejesha Ukuhani wa Haruni kwa Joseph Smith Mdogo na Oliver Cowdery.

Mei 15, 1829

Urejesho wa mamlaka ya ukuhani katika kipindi hiki cha mwisho uliendelea katika maendeleo ya utaratibu, hatua kwa hatua. Kama maandiko ya msingi kwa ajili ya kipindi chetu cha maongozi ya Mungu, Kitabu cha Mormoni, kilikuwa kikitafsiriwa mnamo 1829, Bwana alianza kuweka muundo Wake wa ukuhani mahali pake. Katika kujibu uchunguzi wa sala ya Joseph Smith na Oliver Cowdery kuhusu ubatizo, Yohana Mbatizaji aliyefufuka alitokea na kutunuku juu yao Ukuhani wa Haruni, ukuhani ambao “unashikilia funguo za huduma za malaika, na za injili ya toba, na za ubatizo kwa kuzamishwa kwa ondoleo la dhambi” (Mafundisho na Maagano 13:1). Kwa mamlaka hayo, Joseph na Oliver walibatizana na baadaye kuwabatiza wengine kama Kanisa lilivyoanzishwa rasmi.

urejesho wa Ukuhani wa Melkizedeki

Punde baada ya Mei 15, 1829

Si muda mrefu baada ya kutokea kwa Yohana Mbatizaji, Mitume wa kale Petro, Yakobo, na Yohana walitokea na kutunuku ukuhani wa juu zaidi, au ukuhani wa Melkizedeki, ikijumuisha “funguo za ufalme wangu, na kipindi cha injili cha … utimilifu wa nyakati” (Mafundisho na Maagano 27:13; ona pia 128:20).

mimbari katika Hekalu la Kirtland

April 3, 1836

Mamlaka ya ziada ya ukuhani yalikuja baadaye wakati, katika Hekalu la Kirtland, manabii watatu wa kale, Musa, Elia na Eliya, walipomtokea Joseph na Oliver na kuwakabidhi funguo za kukusanyika kwa Israeli na za kazi zinazohusiana na mahekalu ya Bwana ( ona Mafundisho na Maagano 110:11–16).

Joseph Smith Mdogo anatoa wito kwa Watakatifu wa mwanzo kuwaidhinisha waumini katika miito mipya

Majira ya Kiangazi 1829–Aprili 1835

Mafunuo ambayo sasa yanatumika katika Mafundisho na Maagano yalimwelekeza Nabii Joseph Smith kuhusu kutawazwa kwa wanaume kwenye ofisi za ukuhani wa juu (Melkizedeki) na ukuhani wa matayarisho (Haruni); kuteuliwa kwa maofisa wa ukuhani, kama vile maaskofu; na kuundwa kwa akidi na mabaraza ya ukuhani.

waanzilishi wakivuka nyanda tambarare

1835–1973

Mwongozo wa kinabii unaendelea kuongoza mpangilio wa ukuhani na kufanya kazi katika Kanisa. Kwa mfano, akidi za Sabini zilipangwa katika zama za Kirtland kusaidia Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Baada ya msafara mkubwa kwenda Magharibi na kutawanyika kwa waumini wa Kanisa katika maeneo mapana ya kijiografia, akidi hizi zilipangiwa kufanya kazi katika vigingi vya Kanisa.

kwaya ikiimba kwenye mkutano mkuu

1973–Sasa

Chini ya usimamizi wa Marais Spencer W. Kimball (1895–1985), Ezra Taft Benson (1899–1994) na Gordon B. Hinckley (1910–2008), Sabini na akidi zao walianza kufanya kazi moja kwa moja chini ya Akidi ya Mitume Kumi na Wawili katika ngazi ya Kanisa na katika maeneo ya Kanisa. Akidi katika ngazi ya kigingi ziliondolewa. Leo, akidi kumi na mbili za Viongozi Wakuu wenye Mamlaka na Sabini wa Maeneo huwasaidia Mitume “katika kujenga kanisa na kurekebisha masuala yote yahusianayo na Kanisa katika mataifa yote” (Mafundisho na Maagano 107:34). Akidi za ziada za Sabini zinaweza kuundwa kadiri Kanisa linavyopanuka.

Mzee Christofferson akisalimiana na waumini wa Kanisa huko Gambia

Mzee Christofferson akisalimiana na kaka Sampson na Daniel Amako huko Gambia, Afrika Magharibi, mnamo Februari 2022.

Ukuhani: Nguvu ya Kubariki

Katika neno, lengo la mamlaka ya ukuhani na nguvu ambazo Yesu Kristo alirejesha ni kubariki. Inawawezesha waumini wa Kanisa kutumia nguvu za Mungu katika kuwahudumia na kuwabariki wengine Kanisani, nyumbani na kote ulimwenguni. Waumini wanaungana na Mwokozi katika kukamilisha kazi Yake ya wokovu na kuinuliwa, wakitumia karama takatifu na uwezo unaozidi sana uwezo wao wenyewe ili kusaidia ufalme wa Mungu kukua ili kuijaza dunia ( ona Mafundisho na Maagano 65:2, 5–6).

Bwana ameelezea kwamba “ukuhani huu mkuu wa [Melkizedeki] huihudumia injili na hushikilia ufunguo wa siri za ufalme, hata ufunguo wa kumjua Mungu.

“Kwa hiyo, katika ibada hizo, nguvu ya uchamungu hujidhihirisha.

“Na pasipo ibada hizo, na mamlaka ya ukuhani, nguvu za uchamungu haziwezi kujidhihirisha kwa mwanadamu katika mwili” (Mafundisho na Maagano 84:19–21).

Ibada, bila shaka, ni sherehe zinazotolewa na ukuhani au sakramenti ambazo kwazo tunafanya maagano na Mungu, tukianza na ubatizo na kuendelea kupitia maagano yaliyopokelewa katika nyumba ya Bwana. Ni katika kushika maagano haya kwamba tunabadilishwa kutoka kuwa wanaume na wanawake “wa kawaida” kuwa watakatifu (ona Mosia 3:19) kwa neema ya Kristo ya kulipia dhambi na kuwa wenye kuhesabiwa haki na kutakaswa—bila hatia na bila doa—mbele ya Mungu ( ona Mafundisho na Maagano 20:29–31; 3 Nefi 27:16–20).

Nukuu hii kutoka “Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo kwa Ulimwengu la Maadhimisho ya Miaka Mia Mbili,” lililotolewa na Urais wa Kwanza na Baraza la Mitume Kumi na Wawili, linaelezea muhtasari unaofaa:

“Tunatangaza kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lililoanzishwa mnamo Aprili 6, 1830, ni Kanisa la Kristo la Agano Jipya lililorejeshwa. Kanisa hili limeweka nanga katika maisha makamilifu ya jiwe lake kuu la pembeni, Yesu Kristo, na katika Upatanisho Wake usio na mwisho na Ufufuko wake halisi. Yesu Kristo kwa mara nyingine tena amewaita Mitume na amewapa mamlaka ya ukuhani. Yeye anatualika sote kuja Kwake na kwenye Kanisa Lake, ili kumpokea Roho Mtakatifu, ibada za wokovu na kupata shangwe ya kudumu.”