“Maswali na Majibu kuhusu Afya ya Akili,” Liahona, Sept. 2025.
Kutoka VW Kila Wiki
Maswali na Majibu kuhusu Afya ya Akili
Yote yasiyo haki kuhusu maisha yatafanywa kuwa sahihi kwa sababu ya Yesu Kristo.
Kupata shangwe katika injili ya Yesu Kristo wakati ukisawazisha changamoto za afya ya akili wakati mwingine inaweza kuonekana kama haiwezekani. Nguvu ambazo ni ngumu kudhibiti zinaweza kutuzuia kuhisi ushawishi wa Roho Mtakatifu, pengine kutufanya tushuku kwa nini tunaendelea kujaribu.
Ingawa Bwana hajafunua majibu yote kwa sala zetu za dhati, Yeye ametoa mwongozo, ushauri, faraja na tumaini kupitia manabii Wake na mitume na viongozi wengine wa Kanisa.
Haya ni baadhi ya maneno yao yenye msukumo ambayo yanaweza kusaidia kujibu maswali ya kawaida yanayoulizwa na vijana wakubwa. Ikiwa baadhi ya maswali haya pia yana uzito akilini mwako, jua kwamba injili ya Yesu Kristo itakuletea amani na matumaini wakati hakuna kitu kingine kinachoweza.
Kumhisi Roho
S: Je, afya yangu ya akili ni changamoto zangu za dhambi?
J: “Ni muhimu kutambua kwamba [maradhi ya akili] si matokeo ya udhaifu, wala si daima matokeo ya dhambi. … Kwa pamoja, tunaweza kuvunja mawingu ya kutengwa na unyanyapaa ili mzigo wa aibu uinuliwe na miujiza ya uponyaji iweze kutokea.”
Dada Reyna I. Aburto, Mshauri wa Pili wa zamani katika Urais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi, “Katika Mawingu na Jua, Bwana, Kaa Nami!,” Liahona, Nov. 2019, 58.
S: Kwa nini sipati nafuu wakati ninafanya kile kilicho sahihi?
J. “Usidhani unaweza kutatua kila kitu. Tatua kile unachoweza. Kama huo ni ushindi mdogo tu, basi shukuru na kuwa mwenye subira. Mara kadhaa katika maandiko, Bwana anamwamuru mtu ‘kusimama kimya’ au ‘kutulia’—na kungoja. Kuvumilia baadhi ya vitu ni sehemu ya elimu yetu duniani.”
Rais Jeffrey R. Holland, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Kama Chombo Kilichovunjika,” Liahona, Nov. 2013, 41.
S: Ninawezaje kujua ninapata majibu ya sala wakati afya yangu ya akili inayafanya yawe magumu kutambua?
J: “Katika mengi ya mashaka na changamoto tunazokumbana nazo katika maisha yetu, Mungu anatutaka tufanye kwa uwezo wetu wote, kutenda na siyo kutendewa (ona 2 Nefi 2:26), na kumwamini Yeye. … Mara kwa mara tunaweza kusonga mbele tukitumaini na kusali—lakini bila hakikisho kamili—kwamba tunatenda kulingana na mapenzi ya Mungu. Lakini tunapoheshimu maagano yetu na kutii amri, tunapojitahidi zaidi kutenda mema na kuwa wazuri zaidi, tunaweza kutembea kwa ujasiri kwamba Mungu ataongoza hatua zetu.”
Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Roho ya Ufunuo,” Liahona, Mei 2011, 90.
S: Ninawezaje kuhisi shangwe katika injili wakati msongo wa mawazo unapoifanya kuwa vigumu sana kuhisi shangwe?
J. “Unapotafiti neno la Mungu kwa ajili ya uelewa wa kina wa mpango wa milele wa Mungu … na kujitahidi kutembea katika Njia Yake, utapokea “amani ya Mungu, ipitayo uelewa wote’ [Wafilipi 4: 7], hata katikati ya majonzi. Utahisi kipimo kikubwa cha upendo wa Mungu usioweza kupimika ukivimba ndani ya moyo wako. Mawio ya mwangaza wa selestia yatapenya vivuli vya majaribu yako, na utaanza kuonja utukufu usioelezeka na maajabu ya mbingu yasiyoonekana, makamilifu. Utahisi roho yako ikinyanyuka kutokana na mvuto wa ulimwengu huu.
Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Shangwe ya Juu Zaidi,” Liahona, Nov. 2024, 69).
Ufikiaji wa Nguvu za Yesu Kristo
S: Ninawezaje kujifunza kumwamini na kumtegemea Kristo ninapohisi kama siwezi kujiamini mwenyewe kwa sababu ya changamoto zangu za afya ya akili?
A: “Kadri unavyojifunza zaidi juu ya Mwokozi, ndivyo itakavyokuwa rahisi kutumaini katika rehema Yake, upendo Wake usio na kikomo, na nguvu Yake yenye kuimarisha, kuponya, na kukomboa.
“… Kama kila kitu na kila mtu mwingine ulimwenguni ambaye unamwamini atashindwa, Yesu Kristo na Kanisa Lake kamwe hawatashindwa.”
Ona Russell M. Nelson, “Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima,” Liahona, Mei 2021, 103104.
S: Je, Kristo kweli anajua jinsi ninavyohisi?
A: “Kunaweza kusiwepo mwanafamilia, rafiki, au kiongozi wa ukuhani—hata wawe wasikivu kiasi gani na nia nzuri yoyote ile—nani anajua hasa kile unachohisi au ana maneno halisi ya kukusaidia kupona. Lakini tambua hili: kuna Mmoja anayeelewa vyema kile unachopitia, ambaye ni “mkuu kupita ulimwengu wote,”1 Nefi 4:1, na ambaye “awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote [sisi] tuyaombayo au tuyawazayo’ [”Waefeso 3:20
Mzee Matthew S. Holland wa Sabini, “Zawadi Nzuri Sana ya Mwana,” Liahona, Nov. 2020, 46.
Kuhisi Upendo wa Mungu
S: Je, Mungu bado ananipenda ingawa nina changamoto za afya ya akili?
J. “Pengine kuna sauti za kiitikio za kukukatisha tamaa na kutia kiza ambazo zinajaza mawazo yako, jumbe zikikuambia kwamba umejeruhiwa sana na kukanganywa, mdhaifu sana na uliyesahaulika, wa tofauti sana au asiyejielewa ili kupata upendo wa kimbingu katika njia yoyote dhahiri. Ikiwa unasikia mawazo hayo, basi tafadhali sikia hili: sauti hizo ni za uongo. Tunaweza kwa ujasiri kupuuza uvunjikaji kwa njia yo yote yenye sifa kutokana na upendo wa mbinguni.
Mzee Karl D. Hirst wa Sabini, “Kipendwa cha Mungu,” Liahona, Nov. 2024, 11.
S: Kwa nini Mungu haondoi changamoto hii?
J: “Katika jitihada za kutafuta kiasi cha amani na ufahamu wa maswala haya magumu, ni muhimu kukumbuka kwamba tunaishi—na tulichagua kuishi—katika ulimwengu ulioanguka, ambapo kwa malengo ya kiungu utafutaji wetu wa uchamungu utatahiniwa na kujaribiwa tena na tena. Hakikisho kuu katika mpango kama huo ni kwamba Mwokozi aliahidiwa, Mkombozi ambaye kupitia kwa imani yetu Kwake angetuinua kwa ushindi juu ya majaribu na majaribio, hata ingawa gharama ya kufanya hivyo haingeeleweka kwa uzito wake kwake Baba ambaye alimtuma Yeye na Mwana ambaye alikuja. Ni kuthamini tu upendo huu wa kiungu ambao utafanya mateso yetu madogo kwanza kuwa yanaweza kuhimilika, kisha kueleweka, na hatimaye kukomboleka.
Rais Jeffrey R. Holland, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Kama Chombo Kilichovunjika,” Liahona, Nov. 2013, 40.
Kuchagua Kuishi
S: Kama najua maisha yajayo yatakuwa bora, kwa nini niendelee kuishi maisha haya?
J: “Bila kujali wasiwasi wako au magumu yako, kifo kwa kujiua sio jibu. Hakitapoza maumivu unayohisi au yale unayodhani umeyasabisha. Katika ulimwengu ambao unahitaji sana kila nuru unayoweza kupata, tafadhali acha kupunguza nuru ya milele ambayo Mungu ameiweka nafsini mwako kabla ya ulimwengu huu kuwepo. Zungumza na mtu. Omba msaada. Tafadhali acha kuangamiza uhai ambao ilimgharimu Kristo kuutoa uhai Wake ili kuulinda. Unaweza kukabiliana na changamoto za maisha haya kwa sababu sisi tutakusaidia ukabiliane nazo.”
Rais M. Russell Ballard, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Usiogope:Amini Tu!,” Liahona, Mei 2022, 36).
“Masumbuko yako yawayo yo yote, kaka zangu na dada zangu—kiakili au kihisia au kimwili, au vinginevyo—usipige kura dhidi ya uthamani wa maisha kwa kuyamaliza! Mtumainie Mungu. Shikilia upendo Wake. Jua kwamba siku moja jua litapambazuka kwa uangavu na vivuli vyote vya maisha ya duniani vitatoweka.
Rais Jeffrey R. Holland, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Kama Chombo Kilichovunjika,” Liahona, Nov. 2013, 42.
Kuwasaidia Wapendwa
S: Ninawezaje kumsaidia mpendwa wangu ambaye anakabiliwa na changamoto za afya ya akili?
J: “Kujielimisha wenyewe kuhusu maradhi ya akili kunatuandaa kujisaidia sisi na wengine ambao yawezekana kuwa wanateseka. Mijadala ya wazi na ya uaminifu kwa kila mmoja itasaidia mada hii muhimu kupata usikivu unaostahili kupata. Hata hivyo, taarifa hutangulia mwongozo wa kiungu na ufunuo. Changamoto hizi zisizoonekana mara nyingi zinaweza kumuathiri ye yote, na tunapokabiliana nazo, zinaonekana hazitatuliki.
“Moja ya vitu vya mwanzo tunavyohitaji kujifunza ni kwamba hakika hatuko pekee yetu. Ninawaalika mjifunze mada ya afya ya akili katika sehemu ya Msaada wa Maisha ya app ya Maktaba ya Injili. Kujifunza kutaongoza kwenye uelewa zaidi, kubalika zaidi, huruma zaidi, upendo zaidi. Unaweza kupunguza majanga, wakati kukitusaidia kukuza na kusimamia matarajio yenye afya na mahusiano yenye afya.
Mzee Erich W. Kopischke wa Sabini, “Kuzungumzia Afya ya Akili,” Liahona, Nov. 2021, 38.
S: Mmoja wa wapendwa wangu alikufa kwa kujiua kwa sababu ya changamoto za afya ya akili. Je, kitaitokea nini kwao?
J: “Kuna dhana ya zamani ya kidini ambayo kujiua ni dhambi na kwamba mtu ambaye [anakufa kwa] kujiua ametupwa jehanamu milele. Huo ni uongo kabisa. Ninaamini idadi kubwa ya kesi itagundua kwamba watu hawa wameishi maisha ya kishujaa na kwamba kujiua hakutakuwa tabia ya kufafanua ya umilele wao.”
Mzee Dale G. Renlund wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, “Kuelewa Kujiua” (video), Maktaba ya Injili.
Kusonga Mbele na Kutazama Juu
Baadhi ya majibu ambayo Mungu anatupa ni tofauti na yale tuliyotarajia, na baadhi ya majibu hayatakuja katika maisha haya. Wakati hatujui kila kitu sasa kuhusu kwa nini wengi wetu tunapambana na changamoto za afya ya akili, tunaweza kutumainii katika ahadi kwamba siku moja tutakuwa na uelewa kamili wa mambo yote. Juhudi zetu—bila kujali kutozaa matunda tunakojisikia wakati mwingine—zote zitastahili (ona Wagalatia 6:9; Mafundisho na Maagano 58:3).
Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha: “Imani ni nzuri kwa sababu inaendelea hata wakati baraka haziji kama ilivyotumainiwa. Hatuwezi kuona ya siku sijazo, hatujui majibu yote, lakini tunaweza kumwamini Yesu Kristo tunapoendelea kusonga mbele na juu kwa sababu Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu.”
Wakati wewe na wale unaowapenda mnapopitia ugumu wa afya ya akili, kumbuka kwamba hayo yote yasiyo haki kuhusu maisha yatafanywa yawe sawa kwa sababu ya Yesu Kristo. Endelea kusonga mbele na juu—pamoja Naye upande wako, unaweza daima kuvumilia kwa tumaini.