2025
Familia: Tangazo kwa Ulimwengu
Septemba 2025


“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Liahona, Sept. 2025.

Maadhimisho ya Miaka30

Familia

Tangazo kwa Ulimwengu

familia ikitumia muda pamoja

Sisi, Urais wa Kwanza na Baraza la Mitume Kumi na Wawili wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, kwa dhati tunatangaza kwamba ndoa kati ya mwanaume na mwanamke imeamriwa na Mungu, na kwamba familia ni kiini cha mpango wa Muumba kwa ajili ya hatima ya milele ya watoto Wake.

Wanadamu wote—mwanaume na mwanawake—wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Kila mmoja ni mwana au binti mpendwa wa kiroho wa wazazi wa mbinguni, na, kama hivyo, kila mmoja ana asili na takdiri takatifu Jinsia ni sifa muhimu ya mtu kabla ya kuja duniani, katika maisha ya duniani, na utambulisho wa milele na kusudi.

Katika maisha kabla ya haya ya duniani, wana na mabinti wa kiroho walimjua na kumwabudu Mungu kama Baba yao wa Milele na kuukubali mpango Wake ambapo ungewezesha watoto Wake kupokea mwili na kupata uzoefu wa duniani ili wasonge kuelekea ukamilifu na hatimaye watambue hatima yao takatifu kama warithi wa uzima wa milele. Mpango mtakatifu wa furaha unawezesha uhusiano wa familia kuendelezwa zaidi ya kaburi. Ibada takatifu na maagano yanayopatikana katika mahekalu matakatifu yanawezesha watu binafsi kurudi katika uwepo wa Mungu na kwa familia kuunganishwa milele.

Amri ya kwanza ambayo Mungu aliwapa Adamu na Hawa ilihusu uwezekano wao wa kuwa wazazi kama mume na mke. Tunatangaza kwamba amri ya Mungu kwa watoto Wake ya kuongezeka na kuijaza dunia bado ina nguvu leo. Tunatangaza zaidi kwamba Mungu ameamuru kwamba nguvu takatifu za uzazi zitumike tu, kati ya mwanamume na mwanamke, waliooana kisheria kama mume na mke.

Tunatangaza kwamba namna ambavyo maisha ya duniani huanzishwa imeteuliwa kiungu. Tunathibitisha utakatifu wa uhai na umuhimu wake katika mpango wa milele wa Mungu.

Mume na mke wanalo jukumu muhimu la kupendana na kutunzana wao kwa wao na kuwatunza watoto wao. “Watoto ni urithi wa Bwana” (Zaburi 127:3). Wazazi wana jukumu takatifu la kulea watoto wao katika upendo na utakatifu, kukimu mahitaji yao ya kimwili na kiroho, na kuwafundisha kupenda na kutumikiana mmoja na mwingine, kutii amri za Mungu, na kuwa wananchi wenye kutii sheria popote wanapoishi. Waume na wake—akina mama na kina baba—watapasishwa mbele ya Mungu kwa utimizaji wa majukumu haya.

Familia imeamriwa na Mungu. Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke ni muhimu kwa mpango Wake wa milele. Watoto wana haki ya kuzaliwa ndani ya mikataba ya ndoa, na kulewa na baba na mama wanaoheshimu viapo vya ndoa kwa uaminifu kamili. Furaha katika maisha ya familia itapatikana kwa urahisi ikiwa imejengwa katika mafundisho ya Bwana Yesu Kristo. Ndoa na familia zenye ufanisi zimejengwa na kukuzwa katika misingi ya imani, maombi, toba, msamaha, heshima, upendo, huruma, kazi, na matendo mazuri ya maburudisho. Kwa mpango wa kiungu, akina baba wanapaswa kusimamia familia zao katika upendo na haki na wanawajibika kukimu mahitaji ya maisha na ulinzi kwa familia zao. Akina mama wana jukumu la kimsingi kwa utunzaji wa watoto wao. Katika majukumu haya matakatifu, akina baba na akina mama wana wajibu wa kusaidiana kama washiriki walio sawa. Ulemavu, kifo, au hali zingine zinaweza kulazimisha utohozi wa kibinafsi. Ukoo unapaswa kutoa usaidizi unapohitajika.

Tunaonya kwamba watu binafsi wanaokiuka maagano ya usafi wa maadili, wanaowanyanyasa wenzi wao wa ndoa au watoto wao, au wanaoshindwa kutimiza majukumu ya kifamilia siku moja watawajibika mbele za Mungu. Zaidi, tunaonya kwamba kusambaratika kwa familia kutaletea watu binafsi, jamii na mataifa majanga yaliyotabiriwa na manabii wa zamani na wa kisasa.

Tunawasihi raia wanaowajibika na mafisa wa serikali kila mahali kuhimiza hatua hizo zilizosanifiwa kudumisha na kuimarisha familia kama kitengo muhimu cha jamii.