2025
UVIKO Karibu Iharibu Ndoto Yake kwenye Kwaya ya Tabernacle
Septemba 2025


“UVIKO Karibu Iharibu Ndoto Yake kwenye Kwaya ya Tabernacle,” Liahona, Sept. 2025.

UVIKO Karibu Iharibu Ndoto Yake kwenye Kwaya ya Tabernacle

Kutengwa kwa karantini kulifundisha somo kubwa: Upendo kama wa Kristo kwa upweke.

Laura Echarri Hermoso

Katika majira ya majani kupuputika ya 2024, si muda mrefu baada ya kuitwa kuwa mshauri wa shirika la eneo katika Eneo la Kati la Ulaya, Laura Echarri Hermoso alisafiri zaidi ya maili 5,000 (8,047 km) kutoka nyumbani kwake huko Pamplona, Hispania, kuimba kama mgeni wa Kwaya ya Tabernacle katika Temple Square.

Alikuwa katika Jiji la Salt Lake, Utah, Marekani, kwa siku tatu tu wakati alipopima na kukutwa na UVIKO-19 na kujitenga mwenyewe. Fursa yake ya kuimba katika kwaya kwa ajili ya mkutano mkuu ujao ilionekana kutofika.

Katika upweke na kutengwa katika chumba chake cha hoteli, alipiga magoti na kusali. Alitumainia uponyaji. Alitamani kuweza kuimba. Alitunza imani yake.

Mwaka Mmoja Kabla

Katika wakati mgumu wa upotevu wakati matibabu ya uzazi yalipothibitisha kutofanikiwa na mama yake alikuwa akiugua maradhi ya alzheimer, Dada Echarri hakuweza kupata sauti yake ya kuimba kama ilivyokuwa awali. Ilikuwa vigumu kwa sababu muziki daima ulikuwa sehemu muhimu ya maisha yake. “Ni haja ambayo daima nimekuwa nayo tangu nikiwa msichana,” alisema.

Dada Echarri pamoja na mama yake

Dada Echarri (kushoto) pamoja na mama yake, María.

Wakati akisali, wazo lilikuja kwamba alihitaji kuimba na watu wengi zaidi. Wiki moja baadaye, aliwasiliana na kiongozi mwenye mamlaka wa Kanisa ambaye alimhoji. “Alizungumza kuhusu mradi wa muziki ambao Kanisa lilikuwa linaanzisha na kwamba walikuwa wakitafuta waimbaji,” Dada Echarri alisema.

Hakusema lengo mahususi, lakini baada ya mahojiano ya pili, kiongozi mwenye mamlaka huyu alifunua kwamba Kanisa lilitaka waimbaji wageni wa Programu ya Kwaya ya Tabernacle ya Washiriki wa Ulimwenguni Kote kuimba katika mkutano mkuu.

“Na nilianza kulia kwa sababu sikujua nini kitatokea, lakini nilihisi Bwana alikuwa pale na kwamba Bwana alikuwa ananijua, na ilikuwa ni kitu ambacho sikuwahi kutarajia,” alisema.

Njia ya Kuelekea Kwenye Mkutano Mkuu

Mahojiano yalikuwa ya awali tu na yalifuatiwa na mahojiano ya pili na mengineyo. Dada Echarri pia alilazimika kujirekodi mwenyewe akiimba na kuwasilisha rekodi kadhaa. Kisha alikuwa na mahojiano ya mwisho, ya mtandaoni na mkurugenzi mshirika wa muziki wa Kwaya ya Tabernacle Ryan Murphy. “Nilikuwa na wasiwasi mwingi,” alisema.

Hatimaye, alichaguliwa na wengine 13 ulimwenguni kote kuimba katika mkutano mkuu, na mnamo Septemba 2024, alipanda ndege kwenda Marekani. Baada ya kuwasili, aligundulika kuwa na UVIKO-19 na hapo ndipo karantini yake ilipoanza.

Kutengwa katika upweke mbali na nyumbani kulifundisha somo kubwa: Mwokozi angetoa faraja katika nyakati zake za upweke (ona Yohana 14:26–27). “Nilidhani haitawezekana,” alisema. “Nilivunjika moyo sana, lakini nilikuwa na imani. Wakati huo huo, sikuwa najihisi vizuri. Sasa mojawapo ya malengo yangu makuu ni kuwatafuta wale wanaohisi kuwa wapweke na kujaribu kuwapa faraja.”

Baada ya siku nane za kutengwa, afya yake na sauti yake ilipona, na alifanya mazoezi na kwaya. Aliunganisha sauti yake na mamia kwenye jukwaa katika Kituo cha Mikutano na kuimba katika mkutano mkuu wa Oktoba 2024.

Picha ya kikundi cha Kwaya ya Tabernacle

“Mungu yu hai. Yeye anatufahamu, kila mmoja wetu,” alisema. “Muziki ni uponyaji, una nguvu ya uponyaji, na tunahitaji kujaza maisha yetu na muziki. Ni muhimu sana. Ninahisi kwamba hilo ni jambo ambalo Bwana anajaribu kuniambia: Jaza maisha yako kwa muziki.”