Yesu Kristo Ni Mambo Mazuri Zaidi Yajayo
Shangwe ambayo Yesu Kristo huitoa daima inapatikana kwako.
Fikiria kuhusu wakati ulipodhani ulimwengu unaenda kwisha. Hapana, kweli kabisa! Je, umewahi kupitia kitu kigumu sana ambacho ulidhani hutaweza kukivuka?
Sawa, labda hukufikiria ulimwengu ulikuwa unaisha. Lakini ulijisikia kama ulimwengu wako ulikuwa unaisha? Hii inaweza kuwa kitu chochote kutokana na kushindwa mtihani muhimu, kwa rafiki yako bora kuhama, au mpendwa anayefariki bila kutarajia.
Bila kujali jinsi ulivyokabiliana na mapambano hayo ya zamani, jiangalie mwenyewe sasa: ulinusurika! Hata vizuri zaidi, manabii na mitume wanatukumbusha kwamba tunaweza kufanya zaidi ya kunusurika na mapambano ya sasa na ya baadaye. Tunaweza kupata shangwe katikati ya hayo.
“Mambo Mazuri Zaidi Bado Yako Mbeleni”
Mwokozi aliteseka zaidi ya tunavyoweza kufikiria katika Gethsemane na msalabani. Kubeba maumivu, magonjwa, na dhambi za ulimwengu mzima (ona Alma 7:11–13) ingekuwa vigumu, kusema kweli! Lakini yeye alishinda yote.
Mzee Patrick Kearon wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha, “Ndio, tunatafakari mateso na udhalimu ulioletwa juu ya Mkombozi wetu kwa ajili ya dhambi zetu, na hiyo husababisha tafakari ya huzuni. Lakini wakati mwingine tunakwama hapo—kwenye bustani, msalabani, ndani ya kaburi. Tunashindwa kusonga juu kwenye shangwe ya kaburi likipasuka wazi, kushindwa kwa kifo, na ushindi wa Kristo!”
Kwa sababu ya Yesu Kristo, hatupaswi kubaki tumekwama katika mateso yetu wenyewe. Tunaweza kusonga mbele na hata kutazamia siku zijazo kwa furaha na imani.
Kwa hiyo, wakati maisha yanaweza kuonekana kuwa magumu zaidi kuliko tunavyodhani tunaweza kuhimili, kumbuka kile Rais Russell M. Nelson alichokifundisha hivi karibuni: “Mambo mazuri zaidi bado yako mbeleni!” Ni ahadi tukufu jinsi gani! Rais Nelson anajua mengi kuhusu maumivu na machungu ya moyo ambayo ulimwengu huyaona kila siku. Lakini bado anaweza kusema kwamba “Mambo mazuri zaidi bado yako mbeleni!”
Je, mtazamo wako ungebadilikaje kama kweli ungejua mambo mazuri zaidi bado yako mbeleni? Je, ingebadilishaje jinsi unavyokabiliana na changamoto za maisha?
Kumweka Kristo katika Fokasi kwenye Kila Kipengele cha Maisha
Tukio moja la siku zijazo ambalo Rais Nelson ametualika kutazamia kwa shangwe ni Ujio wa Pili wa Yesu Kristo.
Kabla ya kusema kwamba “mioyo ya watu itazimia” (Luka 21:26) na uharibifu unaonyesha juu ya waovu hausikiki kama “mambo mazuri zaidi yajayo,” hebu tufafanue kitu: ni Ujio wa Pili wa Yesu Kristo. Tunakosa hoja kama tutamtoa nje ya fokasi ya kila kipengele cha maisha. Yeye ni “mambo mazuri zaidi ” ambayo bado yako mbeleni—Yeye ndiye sababu ya shangwe yetu! Kama Rais Nelson alivyosema, “Mambo mazuri zaidi bado yako mbeleni … kwa sababu Mwokozi anakuja tena!
Waangalie Wanefi, kwa mfano. Ingawa walikuwa katika bara tofauti kabisa, wakati Mwokozi alipokufa, walivumilia baadhi ya majanga ya aina ya Ujio wa Pili: kifo, uharibifu, majanga ya asili. Miji yote ilizama baharini (ona 3 Nefi 8).
Lakini baada ya vurumai hiyo yote, wale walioamini katika Mwokozi walijua kwamba majanga yalikuwa ishara ya kifo cha Mwokozi. Katika wakati ule ule walipokuwa wakizungumza kuhusu Yesu Kristo na ishara walizoziona, Mwokozi akawatokea (ona 3 Nefi 11:1–11).
Fikiria ni shangwe kiasi gani Wanefi walijisikia! Baada ya maangamizo hayo mabaya, Mwokozi aliwatumikia na kuwaponya. Baada ya hofu na kuingiwa na wasiwasi, Wanefi walishangilia na kumsifu Mungu kwamba waliweza kukutana na Mwokozi wao (ona 3 Nefi 11:14–17).
Mwokozi anaweza asikutembelee kimwili katika maisha haya kama alivyofanya kwa Wanefi. Lakini unaweza kuja kumjua Yeye kupitia kusoma maandiko, kupokea sakramenti, kushika maagano, na zaidi. Anaweza kukusaidia kujisikia mwenye shangwe sasa na baadaye, bila kujali hali zako.
Wakati Tukingojea …
Ujio wa Pili wa Mwokozi unaweza kutokea katika maisha yako, au huenda isiwe hivyo. Kwa njia yoyote ile, kuna shangwe katika Yesu Kristo sasa hivi.
Rais Nelson alifundisha ukweli ufuatao wa kutia msukumo ambao unasaidia wakati tunaposubiri kurudi kwa Mwokozi: “Wapendwa kaka zangu na dada zangu, mambo mengi ya kupendeza yapo mbeleni. Katika siku zijazo, tutaona madhihirisho makubwa zaidi ya nguvu za Mwokozi ambayo ulimwengu kamwe haujapata kuyaona. Kati ya sasa na wakati Yeye anaporudi ‘kwa uweza na utukufu mkuu,’ Atatoa fuesa zisizo na idadi, baraka, na miujiza juu ya walio waaminifu.”
Kwa maneno mengine, tunaweza kupata amani na furaha katika Kristo hivi sasa, hadi ujio Wake, na milele. Yesu Kristo ndiye nuru na uzima wa ulimwengu. Yeye ni shangwe katika magumu binafsi. Yeye ni faraja kutokana na hofu. Yeye ni Mwokozi wangu. Unapofokasi Kwake, amani na furaha vinapatikana kwako hapa, sasa, na daima.