2025
Baraka za Mamlaka na Nguvu ya Ukuhani
Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Septemba 2025


Baraka za Mamlaka na Nguvu ya Ukuhani

Ukuhani wa Mungu umerejeshwa katika siku yetu ili kuwabariki watoto Wake wote.

urejesho wa Ukuhani wa Melkizedeki

Urejesho wa Ukuhani wa Melkizedeki, na Walter Rane

Vijana mara nyingi huuliza maswali kuhusu ukuhani. Kuhusu ukuhani, ushahidi wetu kwa ulimwengu ni:

  1. Ukuhani mtakatifu wa Mungu ni muhimu katika kukamilisha kazi Yake ya wokovu na kuinuliwa.

  2. Mungu amerejesha ukuhani duniani.

  3. Ukuhani unasimamiwa na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Kwa Nini Tunahitaji Mamlaka na Nguvu ya Ukuhani

Yesu Kristo ndiye kichwa cha Kanisa hili. Kanisa ni chombo alichokiumba ili kukamilisha kazi muhimu ya kuwakomboa wanadamu. Kupitia Kanisa, Anaweza:

  • Kutangaza injili Yake kote ulimwenguni.

  • Kutoa ubatizo na maagano mengine yote—hata njia ya agano kwenye ufalme Wake wa selestia.

  • Kuziunganisha familia milele.

  • Kutoa zawadi za wokovu, hata kwa wale waliokufa bila kuwa nazo.

  • Kuhudumia mahitaji ya kimwili ya watoto wa Mungu kwa sasa.

Yesu Kristo akifundisha

Yesu Akimfundisha Mariamu, na Dan Burr

Ili kutimiza madhumuni haya makuu, na kujiandaa kwa ajili ya kurudi kwa Mwokozi, Kanisa linahitaji mwongozo, mamlaka, na nguvu endelevu za Mungu. Kanisa hili ni “kanisa la kweli na lililo hai” (Mafundisho na Maagano 1:30) kwa sababu Kristo anawekeza kwa uongozi Wake na nguvu kupitia ukuhani Wake.

Bila ukuhani huu mtakatifu, Kanisa kimsingi lingekuwa shirika la kidunia kama wengine wengi, likifanya mema ulimwenguni lakini bila nguvu ya kufikia lengo la kuwatayarisha watoto wa Mungu kwa shangwe ya uzima wa milele katika uwepo Wake. Pamoja na ukuhani huu, na funguo za kuongoza kazi ya ukuhani huu, kuna vyote mamlaka na utaratibu katika Kanisa.

“Katika Kanisa, mamlaka yote ya ukuhani yanatumika chini ya maelekezo ya wale ambao wanashikilia funguo za ukuhani.

“Waumini wanaume wa Kanisa wanaostahili wanapokea mamlaka ya ukuhani kupitia utunukiwaji wa ukuhani na kutawazwa kwenye ofisi za ukuhani. Waumini wote wa Kanisa wanaweza kutumia mamlaka yaliyonaibishwa ya ukuhani pale wanaposimikwa au kupangiwa kazi ya kusaidia katika kutimiza kazi ya Mungu.”

akina dada wamisionari

Umerejeshwa katika Siku Yetu

Wakati Kitabu cha Mormoni kikitafsiriwa mnamo 1829, Bwana alianza kuweka mahali pake muundo wa ukuhani Wake. Katika kujibu sala ya Joseph Smith na Oliver Cowdery kuhusu ubatizo, Yohana Mbatizaji mfufuka alitokea na kuwatunukia juu yao Ukuhani wa Haruni, ambao “unashikilia funguo za huduma za malaika, na za injili ya toba, na za ubatizo kwa kuzamishwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi” (Mafundisho na Maagano 13:1). Kwa mamlaka hayo, Joseph na Oliver walibatizana na wao wakawabatiza wengine Kanisa lilipoanzishwa rasmi.

Si muda mrefu baadaye, Mitume wa kale Petro, Yakobo, na Yohana walitokea na kutunuku Ukuhani wa juu au wa Melkizedeki, ikijumuisha “funguo za ufalme wangu, na kipindi cha injili kwa … utimilifu wa nyakati!” (ona Mafundisho na Maagano 27:12–13; 128:20).

mvulana akiwa amewekewa mikono kichwani mwake

Mamlaka ya ziada ya ukuhani yalikuja wakati manabii watatu wa kale, Musa, Elia, na Eliya, walipomtokea Joseph na Oliver katika Hekalu la Kirtland na kuwakabidhi funguo za kukusanyika kwa Israeli na za kazi ya mahekalu ya Bwana (ona Mafundisho na Maagano 110:11–16).

wamisionari

Nguvu ya Kubariki

Katika neno, dhumuni la mamlaka ya ukuhani na nguvu ambazo Yesu Kristo alirejesha ni kubariki. Inawawezesha waumini wote wa Kanisa kutumia nguvu za Mungu katika kuwahudumia na kuwabariki wengine Kanisani, nyumbani, na kote ulimwenguni. Waumini wanaungana na Mwokozi katika kukamilisha kazi Yake ya wokovu na kuinuliwa, wakitumia karama takatifu na nguvu kupita zao wenyewe ili kusaidia ufalme wa Mungu kukua kuijaza dunia (ona Mafundisho na Maagano 65:2, 5–6).

Bwana amefafanua kwamba “ukuhani huu mkuu [Melkizedeki] husimamia injili na hushikilia ufunguo wa siri za ufalme, hata ufunguo wa ufahamu wa Mungu.

“Kwa hiyo, katika ibada zake, nguvu za uchamungu hujidhihirisha” (Mafundisho na Maagano 84:19–20).

Ibada ni sherehe zinazosimamiwa na ukuhani ambazo kwa hizo tunafanya maagano na Mungu, tukianzia na ubatizo na kuendelea kupitia maagano yaliyopokelewa katika nyumba ya Bwana. Ni katika kushika maagano haya kwamba tunabadilishwa kutoka kuwa wanaume na wanawake “wa tabia ya asili” na kuwa watakatifu (ona Mosia 3:19) kwa neema ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi na kuwa wenye kuhesabiwa haki na kutakaswa—bila hatia na bila doa—mbele ya Mungu (ona Mafundisho na Maagano 20:29–31; 3 Nefi 27:16–20).

Yesu Kristo

Kristo huko Amerika, na Ben Sowards

“Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo la Maadhimisho ya Miaka Mia Mbili kwa Ulimwengu,” lililotolewa na Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, linaelezea muhtasari unaofaa:

“Tunatangaza kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lililoanzishwa mnamo Aprili 6, 1830, ni Kanisa la Kristo la Agano Jipya lililorejeshwa. Kanisa hili limeweka nanga katika maisha makamilifu ya jiwe lake kuu la pembeni, Yesu Kristo, na katika Upatanisho Wake usio na mwisho na Ufufuko wake halisi. Yesu Kristo kwa mara nyingine tena amewaita Mitume na amewapa mamlaka ya ukuhani. Yeye anatualika sote kuja Kwake na kwenye Kanisa Lake, ili kupokea Roho Mtakatifu, ibada za wokovu, na kupata shangwe ya kudumu.”