Yesu Kristo Ni kwa Ajili ya Siku Njema Pia
Wakati mambo yanapokwenda vizuri, tunawezaje kubaki tumefokasi kwa Mwokozi? Haya ni baadhi ya mawazo.
Fikiria kama rafiki alitumia muda pamoja nawe wakati tu walipokuwa wanasumbuka na kukuepuka wakati walipokuwa na furaha. Je, huo ni uhusiano wenye afya? Hakika siyo.
Je, tumewahi kufanya hivyo kwa Mwokozi wetu—kumtafuta Yeye katika nyakati ngumu na kumsahau Yeye katika nyakati nzuri?
Tunazungumza mengi kuhusu jinsi Yesu Kristo anavyotusaidia kupitia nyakati zetu ngumu, pengine kwa sababu kila mtu, wakati mmoja au mwingine, anakabiliwa na mambo magumu.
Lakini kuna baadhi ya siku—wiki au hata miaka, ikiwa tuna bahati—ambapo mambo yanakwenda vizuri sana. Wakati mwingine tunamsahau Mwokozi katika nyakati hizo. Watu wa Kitabu cha Mormoni walifanya hivyo. Walifanikiwa kutokana na baraka za Mungu kwa muda lakini hatimaye waliangukia kwenye kiburi walipomsahau Yeye.
Nyakati nzuri hazimaanishi kwamba ghafla hatumhitaji Yesu Kristo tena. Nyakati za mafanikio ni nyakati kamilifu za kushangilia pamoja na Mwokozi, na si kumsahau Yeye.
Kwa hiyo ni kwa jinsi gani tunabaki tumeunganika na Yesu Kristo na Baba yetu wa Mbinguni wakati ambapo majaribu hayatukumbushi kuwageukia Wao?
Baki mnyenyekevu
Wakati mambo yanapokwenda vizuri, ni vizuri kusherehekea baraka zako na mafanikio yako. Lakini usisahau ni nani aliyefanya iwezekane kwako kuwa mahali ulipo. Mfalme Benyamini aliliweka hivi katika mahubiri yake kwenye Kitabu cha Mormoni:
“Kwani tazama, si sisi wote ni waombaji? Je, si sisi sote tunamtegemea yule Mmoja, aliye Mungu, kwa mali yote tuliyo nayo, kwa chakula na mavazi, na kwa dhahabu, na kwa fedha, na kwa kila utajiri tulio nao?” (Mosia 4:19).
Kuwa mnyenyekevu kuhusu mafanikio yako kwa kukumbuka kile ambacho Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wamefanya kwa ajili yako ni njia nzuri ya kuwajumuisha Wao katika nyakati zako nzuri.
Baki mwenye Shukrani
Shukrani ni mojawapo ya tiba bora za kiburi na usahaulifu. Kumshukuru Mungu kutakusaidia kumkumbuka Yeye na mema yote ambayo Yeye na Mwanawe wanayafanya katika maisha yako. Hii ni yenye ufanisi katika nyakati nzuri kama ilivyo katika nyakati ngumu.
Baki Makini
Mojawapo ya mashambulizi pendwa ya Shetani ni “kukupatanisha, na kukulaghai [wewe] kwenye usalama wa kimwili” (2 Nefi 28:21). Kwa maneno mengine, angependa kama ungehisi kuridhika sana na salama katika nyakati zako nzuri kwamba ungesahau kile kilicho muhimu zaidi. Kwa hiyo, usimsahau Mungu! Unapobaki makini kwenye hila za adui na kuzipinga hata wakati wa nyakati zako nzuri, unaweza kuwa karibu na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
Mchungaji Mwema, na Michael Malm
Baki Umejikita katika Kristo
Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Wakati fokasi ya maisha yetu inapokuwa katika mpango wa Mungu wa wokovu … na Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kujisikia wenye shangwe bila kujali nini kinatokea—au kutotokea—katika maisha yetu. Shangwe huja kutoka Kwake na kwa sababu Yake. Yeye ndiye chanzo cha shangwe yote.”
Ni mara ngapi unafikiria ukweli huu kuhusu shangwe wakati maisha yanapokwenda vizuri? Huu sio tu ushauri wa kufariji kwa ajili ya wakati mambo yanapokuwa mabaya. Ni kweli daima, ikiwa ni pamoja na kwenye siku zako nzuri sana. Kwa hivyo fanya yote uwezayo kufokasi kwa Kristo, yaje mabaya au mazuri.