Kushiriki Shangwe Nchini Kenya
Wakati Robert alipoipata injili, ilibidi aishiriki na kila mtu aliyemjua. Hapana, kweli—kila mtu.
Picha na Leslie Nilsson na Eric D. Snider
Tangu kubatizwa mnamo Agosti 2024, Robert L., 18, wa Kenya, amewaleta zaidi ya marafiki 50 kanisani—na kuwabatiza 25 kati yao!
Hiyo ilikuwa idadi tulipozungumza naye miezi michache iliyopita, hata hivyo. Labda imepanda tangu wakati huo.
Robert, mshiriki wa Tawi la Bukuru katika Wilaya ya Kisumu Kenya, alitambulishwa kwenye Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho mwanzoni mwa mwaka 2024, alipokutana na Mmarekani mmoja aliyekuwa akifanya kazi ya misaada ya kibinadamu nchini Kenya.
“Kwa kweli sikuwa nikitarajia kwamba maisha yangu yangekuwa bora,” Robert anasema. “Wazazi wangu hawakuwa na pesa; hawangeweza kunipeleka shule.” (Nchini Kenya, hata shule ya umma inagharimu pesa.)
“Lakini nilijua Baba wa Mbinguni angenisaidia. Nilianza kusali na kusoma Agano Jipya. Kisha nikakutana na mdhamini wangu.”
“Mdhamini” wake alikuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ambaye alibariki maisha ya Robert kwa njia mbili: alimsaidia kupata shule yake na, muhimu zaidi, alishiriki injili pamoja naye (kama alivyofanya kijana mwingine ambaye hivi karibuni alijiunga na Kanisa). Robert alibatizwa takribani miezi sita baadaye.
Robert L. wa Kenya amewaalika watu wengi kuja kanisani—majirani, wanafunzi wenzake, watoto anaocheza nao michezo—kila mtu.
Kurithisha Ukarimu
Kwa kawaida, Robert alitaka kushiriki baraka zake mpya na wengine. Hakuweza kudhamini elimu ya mtu yeyote. Lakini kwa hakika angeweza kuwafundisha injili!
Alianza kuwaalika watu kanisani—majirani, wanafunzi wenzake, watoto aliokuwa akicheza nao michezo—kila mmoja aliyemjua. “Nilikuja Jumapili moja na, kama, watano, kisha Jumapili nyingine nilikuja na 10,” anasema. “Kisha niliwatuma wamisionari kwao ili waweze kuelewa na kujua kwamba Kanisa hili ni la kweli na wanaweza kupata uzoefu wa kile ninachopitia.”
Haikuwa muda mrefu kabla baadhi ya marafiki wa Robert kuchagua kubatizwa na kumuomba afanye ibada hiyo.
Kanisa linakua kwa kasi barani Afrika, kwa sehemu kwa sababu ya wafuasi kama Robert. Aliwabatiza watu 10 wiki moja, 11 wiki iliyofuata, na 4 “pekee” wiki iliyofuata.
Robert anawaalika marafiki kwenye tawi lake la Kanisa, ambalo hukutana katika hema katika kiwanja cha nyasi.
Zaidi ya dazeni ya marafiki hao wapya waliobatizwa walikuwa pamoja naye katika mkutano wa KNV nchini Kenya mwezi Desemba mwaka jana, akiwemo rafiki mmoja ambaye tayari alikuwa amembatiza mmoja wa marafiki zake.
Unaona jinsi kasi inavyojengeka? Inajilisha yenyewe!
Kumhisi Roho
Fredrick A., 17, anasema kwamba wakati rafiki yake Robert alipomwalika kanisani, alihisi Roho kwa nguvu sana kiasi kwamba asingeweza kumkataa.
“Nilipofika kanisani, Roho wa Mungu alitumwa juu yangu,” Fredrick anasema. “Nilipopewa Kitabu cha Mormoni, nilianza kukisoma. Kama sielewi, mara zote namuuliza rais wangu wa tawi na kusali.”
Robert (kushoto) na Fredrick wamebaki kuwa marafiki tangu Robert alipomtambulisha kwenye injili.
Gift M., 18, ni rafiki mwingine ambaye Robert alimbatiza. “Nina furaha kuwa sehemu ya Kanisa la kweli—Kanisa pekee la kweli ulimwenguni,” Gift anasema kwa tabasamu.
Gift anatarajia kuhudumu misioni.
Wengi wa watu ambao Robert amewaalika kanisani wamechagua kubatizwa, na wanawaalika wengine waje pia.
Bado Kazi Zaidi Mbele
Robert anapanga kuhudumu misioni mara tu anapomaliza shule (kama vile Gift na Fredrick). Kwa nini anataka kufanya hivyo wakati anajua kwa uwazi kabisa jinsi ya kushiriki injili?
“Inabidi niende kuhudumu misioni ili nipate uzoefu zaidi na kujifunza zaidi,” Robert anasema. “Itaimarisha imani yangu na kubadili mtazamo wangu. Ndicho Mungu anachotaka mimi nifanye.”
Robert hajamaliza kushiriki injili. Anapanga kuhudumu misioni. “Ni kitu ambacho Mungu anataka nifanye,” anasema.