Vijana
11. Ukweli utakuweka huru


Mvulana katika nyakati za kale akisoma kutoka hati za kukunja kwa kuviringisha

Sherehekea Neno, na Liz Lemon Swindle Kwa hisani ya Havenlight

11.

Uweli utakuweka huru

Yohana 8:32

Baba yako wa Mbinguni ni Mungu wa ukweli. Anajua yote. Ukweli wote unakuja kutoka Kwake na unaongoza Kwake. Unaonesha kwamba unathamini ukweli pale unapotafuta kujifunza, kuishi kwa uadilifu, na kwa ujasiri kusimama kwa ajili ya kile unachojua ni sahihi—hata kama inabidi kusimama peke yako.

Kweli za Milele

Baba wa Mbinguni anataka mabinti zake na wanawe daima wawe wanajifunza. Unazo sababu zote mbili za kimwili na za kiroho za kutafuta na kupenda kujifunza. Elimu siyo tu kuhusu kupata pesa. Ni sehemu ya lengo lako la milele la kuwa zaidi kama Baba wa Mbinguni.

Kuishi kwa uadilifu inamaanisha unapenda kile kilicho sahihi mbele za Mungu—zaidi kuliko unavyopenda faraja binafsi, umaarufu, au urahisi. Inamaanisha kufanya kile kilicho sahihi kwa sababu tu ni sahihi.

Unacho kitu fulani cha thamani cha kushiriki na wengine. Injili ya Yesu Kristo ina majibu ya maswali ya maisha. Ni njia ya kuelekea kwenye amani na furaha. Yawezekana usijue kila kitu, lakini unajua vya kutosha kumpenda jirani yako, kushiriki kanuni za kweli pamoja nao, na kuwaalika kujifunza zaidi.

Mialiko

Daima uwe mwenye kujifunza. Tafuta fursa ili kukuza akili yako na ujuzi wako. Fursa hizi zinaweza kujumuisha elimu rasmi shuleni au mafunzo ya ufundi stadi, vile vile kujifunza kusiko rasmi kutoka kwenye vyanzo unavyoviamini. Mhusishe Bwana katika juhudi zako, na Yeye atakuongoza.

Jifunze kweli za kiroho. Unapojifunza kuhusu ulimwengu unaokuzunguka, jifunze pia kuhusu Mwokozi, aliyeumba huo ulimwengu. Jifunze maisha na mafundisho Yake. Fanya seminari, chuo, na mafunzo binafsi ya injili kuwa sehemu ya kujifunza maisha yako yote. Inaweza kukuandaa kuhudumu misioni na kushiriki injili maisha yako yote.

Ishi kwa uadilifu. Usiibe, usiseme uongo, usidanganye, au kulaghai kwa njia yoyote ile—iwe shuleni, kazini, mtandaoni, kila mahali. Kuwa mtu yule yule mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo hadharani na uwapo faraghani.

watu wakiwa wamepiga magoti mbele ya Yesu Kristo aliyefufuka

Baraka Zilizoahidiwa

Elimu huongeza uwezo wako wa kumtumikia Bwana, ikijumuisha kama mmisionari. Inakuwezesha wewe kuwabariki wengine, hususani familia yako. Kadiri unavyozidi kujifunza, ndivyo unavyoweza kusaidia kujenga ufalme wa Mungu na kuushawishi ulimwengu kwa mema.

Uaminifu unaleta amani na kujiheshimu. Wakati maneno na matendo yako vinapofungamana na ukweli, unaonesha kwamba unaweza kuaminiwa na watu wengine pia na Bwana.

Unaposimama imara kwa ajili ya mafundisho ya Yesu Kristo, Yeye anasimama nawe. Yesu Kristo ni nguvu yako! Wengine yawezekana wasikubaliane na imani zako wewe, lakini ujasiri wako na uaminifu wako vitaonekana. Iwe wengine wanafuata mfano wako au la, ushuhuda wako, kujiamini kwako na imani yako katika Yesu vitakua.

Maswali na Majibu

Je, siyo sahihi kuwa na maswali kuhusu Kanisa? Je, ninawezaje kupata majibu? Kuwa na maswali siyo ishara ya udhaifu au kupungukiwa na imani. Ukweli ni kwamba, kuuliza maswali kunaweza kusaidia kujenga imani. Urejesho wa injili ulianza wakati Joseph Smith mwenye umri wa miaka14 alipouliza maswali kwa imani. Tafuta majibu katika maandiko, katika maneno ya manabii wa Mungu, kutoka kwa viongozi wako na washiriki wa familia walio waaminifu na kutoka kwa Mungu Mwenyewe. Kama majibu hayaji mara moja, kuwa na tumaini kwamba utajifunza mstari juu ya mstari. Endelea kuishi kwa kile ambacho tayari unakijua na endelea kutafuta ukweli.

Ninawezaje kusimama imara kwa kile kilicho sahihi bila kuwaudhi wale walio na imani tofauti? Anza kwa kuhakikisha maneno yako na matendo yametiwa msukumo na upendo kwa ajili ya Mungu na watoto Wake. Kushiriki injili hakupaswi kufanywa katika roho ya kubishana bali kwa uwazi, upole, na ukarimu. Unaweza kuwa mwenye upendo kwa wengine hata kama hukubaliani na maoni yao. Kuwa mfano mzuri wa mfuasi wa Yesu Kristo kwa jinsi unavyoishi.

Ona Mathayo 5:14–16 (nuru yenu na iangaze); Yohana 14:6 (Yesu ni kweli); 1 Petro 3:15 (mwe tayari siku zote kushiriki tumaini lenu katika Kristo); Mafundisho na Maagano 88:77–80 (mambo ambayo Bwana anataka tujifunze); 88:118 (tafuteni hekima kutoka kwenye vitabu vizuri); 93:36 (utukufu wa Mungu ni akili); 124:15 (uadilifu maana yake ni kupenda yaliyo ya haki); 130:18 (akili yetu itafufuka pamoja nasi katika ufufuko).

Maswali ya Kibali cha Hekaluni

  • Je, unajitahidi kuwa mwaminifu katika yote unayoyafanya?

  • Je, unaunga mkono au kutangaza mafundisho yoyote, matendo au kanuni zilizo kinyume na zile za Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa siku za Mwisho?