2.
Mungu anataka kuwasiliana nawe
Urejesho wa injili ulianza wakati kijana aliyeitwa Joseph Smith aliposali, na Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, walimjibu. Mungu anaendelea kuliongoza Kanisa Lake kupitia manabii walio hai. Yeye pia anataka kuzungumza na wewe, mtoto Wake, kupitia Roho Mtakatifu. Kujifunza kutambua jinsi Roho Mtakatifu anavyozungumza nawe ni mojawapo ya ujuzi muhimu zaidi unaoweza kuupata.
Kweli za milele
Roho anakuongoza kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Huo ni wajibu muhimu wa Roho Mtakatifu. Yeye pia atakupa mwongozo wa kiungu wa kutubu na kumfuata Yesu Kristo ili uweze kupokea baraka za Upatanisho Wake. Unapotubu, Roho anakutakasa na kukusaidia kubadilika.
Roho Mtakatifu huzungumza kwenye akili na moyo wako. Jumbe kutoka kwa Roho zinaweza kuja akilini mwako kwa njia nyingi—kupitia mawazo yenye maongozi, maonyo, uelewa wa wazi, na kumbukumbu za kiroho. Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza na moyo wako kupitia hisia za kuinua kama faraja, kujiamini, amani, upendo, shangwe, unyenyekevu, shukrani, na subira.
Mialiko
“Pokea Roho Mtakatifu.” Maneno haya yalizungumzwa wakati ulipothibitishwa kuwa muumini wa Kanisa la Kristo. Ni kwa jinsi gani unampokea Roho Mtakatifu? Kwa kutii mafundisho ya Yesu Kristo. Yeye ni nguvu yako. Kumfuata Yeye kunamwalika Roho Mtakatifu katika maisha yako.
Mtafute Baba yako wa Mbinguni katika sala. Mimina moyo wako Kwake. Mshukuru Yeye kwa baraka nyingi nzuri alizokupa. Shiriki Naye shangwe, wasiwasi, na maswali yako. Tulia na usikilize majibu Yake, ambayo yanaweza kuja kama hisia za amani, mawazo akilini mwako, au misukumo ya kufanya kitu.
Sikiliza sauti ya Mungu katika maandiko. Maandiko ni maneno ya Mungu kwako! Jifunze kutoka kwenye maandiko kila siku ili kuigundua sauti Yake na kuhisi upendo Wake. Unaposoma, tafakari kile ambacho Yeye anaweza kuwa anakufundisha, na andika misukumo inayokuja. Ifanye iwe tabia ya kila siku ya kujifunza maandiko—hasa Kitabu cha Mormoni—maisha yako yote.
Ifanyie kazi misukumo unayopokea. Kama una wazo au msukumo wa kufanya kitu cha ukarimu ambacho kitambariki mtu fulani, fanya hivyo! Mambo yote mazuri hutoka kwa Mungu. Mwonyeshe Baba yako wa Mbinguni kwamba Anaweza kukutumaini wewe kufuata misukumo kutoka Kwake.
Baraka Zilizoahidiwa
Roho Mtakatifu atakufariji na kukuongoza. Yeye anajulikana kama Mfariji. Atakusaidia katika nyakati za majaribu. Atakusaidia kujua nini cha kusema au kufanya. Kwa ushawishi Wake, unaweza kueleza tofauti kati ya kile kilicho kweli na kile ambacho ni uongo. Anaweza kukusaidia kupata mazuri kwa wengine na ndani yako mwenyewe. Roho anaweza pia kukuonya juu ya hatari. Atakuongoza kuelekea kwa Yesu Kristo na mbali na dhambi.
Unaweza kupokea karama za roho. Kuna karama nyingi ambazo Mungu huwapa watoto Wake kupitia Roho Wake. Baadhi zilizotajwa katika maandiko zinajumuisha ufunuo, kuamini katika Yesu Kristo, kufundisha, utambuzi, na hekima. Omba ili umwulize Baba wa Mbinguni kuhusu karama za roho alizokupa, jinsi unavyoweza kuzikuza, na jinsi Anavyotaka uzitumie ili kuwabariki wengine.
Maswali na Majibu
Kwa nini watu wengine wana uzoefu mkubwa wa kiroho kuliko mimi nilio nao? Siyo uzoefu wote wa kiroho ni wa kimiujiza au wa kuvutia. Mara nyingi, Mungu huzungumza nasi kupitia mawazo kwenye akili zetu au hisia za upole katika mioyo yetu. Hii ni minong’ono ya kimya, ya sauti ndogo tulivu. Unaweza kuwa unamhisi Roho na hautambui hilo bado. Endelea kusali. Endelea kujifunza neno la Mungu. Kwa muda na mazoezi, utajifunza kumtambua Roho katika njia tofauti.
Ona 1 Wafalme 19:11–12 (Mungu huzungumza kwa sauti tulivu, ndogo); Yohana 15:26 (Roho humshuhudia Kristo); Moroni 10:3–5 (jua ukweli kwa Roho); Mafundisho na Maagano 11:12–13 (Roho huongoza kufanya mema); 45:57 (Mchukue Roho kama kiongozi wako); 46:8–26 (karama za roho).
Maswali ya Kibali cha Hekaluni
-
Je, una imani na ushuhuda juu ya Mungu, Baba wa Milele; Mwanaye, Yesu Kristo; na Roho Mtakatifu?