Vijana
4. Yesu Kristo atakusaidia


Yesu Kristo

4.

Yesu Kristo atakusaidia

Zaburi 147:3

Yesu Kristo ni nguvu yako. Yeye amefanya kila kitu kilicho muhimu kwa ajili yako ili uwe na shangwe katika maisha haya na milele. Kwa kumchagua Yeye na injili Yake, unachagua furaha na shangwe ya milele.

Hata wakati unapojaribu kwa uwezo wako wote ili kufanya chaguzi nzuri, wakati mwingine utafanya makosa. Utafanya mambo ambayo ungetamani usingeyafanya. Kila mtu anafanya hivyo. Wakati hili linapotokea, ni rahisi kujisikia kukata tamaa au kujiuliza kama utaweza kuwa mwema vya kutosha. Lakini kuna habari njema—ya kupendeza, habari yenye tumaini! Kwa sababu Mungu unakupenda, Alimtuma Mwanaye, Yesu Kristo, aliyejichukulia juu Yake dhambi zako ili uweze kutubu, kusamehewa, na kuendelea kukua.

Kweli za milele

Yesu Kristo atakuimarisha. Yeye atakusaidia kubadili matamanio yako, mawazo yako, na matendo yako. Unapokuwa na wasiwasi, woga au unapopambana katika njia yoyote, Yeye atakufariji. Atakusaidia katika vipengele vyote vya maisha yako. Unaweza kumtumaini Yeye.

Toba siyo adhabu kwa ajili ya dhambi, ni njia ambayo kwayo Mwokozi anatuweka huru kutokana na dhambi. Kutubu maana yake ni kubadilika—kugeuka mbali na dhambi na kumgeukia Mungu. Inamaanisha kufanya vizuri zaidi na kupokea msamaha. Aina hii ya badiliko siyo tukio la wakati mmoja, bali ni mchakato endelevu.

Mialiko

Mfanye Yesu Kristo kuwa fokasi ya maisha yako. Tafuta msaada Wake katika yote unayoyafanya.

Tubu. Mgeukie Bwana ukiwa na matamanio ya kufanya vizuri zaidi. Unapokuwa umefanya jambo fulani baya, kwa uaminifu kiri mbele ya Mungu na, kama inavyohitajika, kwa askofu wako na mtu yeyote ambaye umemuumiza. Fanya kadiri uwezavyo kurekebisha mambo yawe sawa.

Shangilia katika zawadi ya kufanya vizuri zaidi na kuwa bora zaidi. Hata wakati inapokuwa siyo rahisi na inachukuwa muda mrefu zaidi kuliko unavyopenda, kamwe usiache kujaribu. Endelea kulifanyia kazi na kutumaini katika Bwana. Yeye atakusaidia kila hatua ya safari yako.

Yesu ameketi kisimani na mwanamke Msamaria

Baraka Zilizoahidiwa

Yesu Kristo atakusamehe na kukuponya unapotubu. Atabadilisha hatia yako kwa kukupa amani na shangwe. Hatakumbuka dhambi zako tena. Yesu Kristo ni nguvu yako, na kwa nguvu Zake, tamanio lako la kushika amri Zake litaongezeka.

Ataubadilisha moyo wako na maisha yako. Kidogo kidogo, utakua na kuwa zaidi kama Yeye.

Maswali na Majibu

Ninajuaje kama Mungu amenisamehe? Mungu anaahidi kwamba atawasamehe wale wanaotubu. Wakati unapohisi faraja kutoka kwa Roho, unaweza kujua kwamba nguvu ya Mwokozi ya kukomboa inafanya kazi katika maisha yako.

Ni wakati gani ninahitaji msaada wa askofu ili kutubu? Askofu wako anashikilia funguo za ukuhani na ana karama za roho ili kukusaidia wewe utubu. Unaweza kutafuta msaada wake na ushauri wake wakati wowote. Kama umefanya makosa makubwa, kama vile kuvunja sheria ya usafi wa kimwili, kutana na askofu wako. Yeye hatakuhukumu. Yeye ni mwakilishi wa Yesu Kristo na atakusaidia kujua jinsi gani ya kutubu kikamilifu na kupokea nguvu ya Mwokozi yenye kuponya na kuimarisha.

Ninajaribu kutubu, lakini ninarudia makosa yale yale. Je, ninapaswa kufanya nini? Usikate Tamaa. Mgeukie Kristo, na uweke imani yako Kwake. Neema yake yatosha. Jaribu tena. Kamwe hauko peke yako katika juhudi zako za maendeleo. Yesu Kristo siku zote yupo nawe.

Ona Enoshi 1:6 (hatia inaweza kuondolewa); Mosia 4:3 (kupitia Roho Mtakatifu, Mungu anaruhusu ujue kuwa umesamehewa); 26:30 (Mwokozi husamehe kila mara tunapotubu); Etheri 12:27 (Neema ya Mwokozi inaweza kufanya vitu dhaifu kuwa vyenye nguvu); Moroni 6:8 (wale wanaotubu wanasamehewa); 10:32 (kamilishwa katika Kristo); Mafundisho na Maagano 1:32 (Bwana anawasamehe wale wanaotubu); 58:42–43 (toba inajumuisha kuungama na kuacha dhambi)

Maswali ya Kibali cha Hekaluni

  • Je, una ushuhuda juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo na wa jukumu Lake kama Mwokozi na Mkombozi wako?

  • Je, kuna dhambi kubwa katika maisha yako zinazohitaji kutatuliwa kwa mamlaka za ukuhani kama sehemu ya toba yako?