6.
Mpende Mungu, mpende jirani yako
Mathayo 22:37–40
Ili kukusaidia wewe kufanya chaguzi nzuri, Mungu hutoa amri. Anafanya hivi kwa sababu anakupenda wewe. Na sababu nzuri ya kutii amri za Mungu ni kwamba unampenda Yeye. Upendo upo katika moyo wa amri za Mungu.
Kweli za milele
Mungu anakupenda. Yeye ni Baba yako. Upendo wake mkamilifu unaweza kukuvutia wewe kumpenda Yeye. Wakati upendo wako kwa Baba wa Mbinguni unapokuwa ushawishi muhimu mno katika maisha yako, maamuzi mengi yanakuwa rahisi zaidi.
Amri mbili kuu kuliko zote ni kumpenda Mungu na kumpenda jirani yako. Na jirani yako ni nani? Kila Mtu! Kitu kingine chochote kilichofundishwa katika maandiko na manabii kimeunganika kwenye amri hizi mbili.
Watu wote ni kaka zako na dada zako—ikijumuisha, ndiyo, watu ambao wako tofauti na wewe au wasiokubaliana na wewe. Baba wa Mbinguni anawataka watoto Wake wapendane. Unapowahudumia watoto Wake, unamhudumia Yeye.
Mialiko
Onyesha upendo kwa Mungu kwa kushika amri Zake. Kwa mfano, kwa kuitakasa siku ya Sabato, ikijumuisha kujiandaa na kupokea sakramenti kwa uaminifu, unamwonyesha Mungu kwamba uko tayari kuiweka wakfu Kwake siku moja kila wiki. Unapofunga na kulipa zaka na matoleo, unamwonyesha Mungu kwamba kazi Yake ni muhimu zaidi kwako kuliko vitu vya kidunia. Unapotumia majina ya Mungu na Kristo kwa heshima, kamwe siyo kwa njia isiyofaa au isivyo rasmi, unaonesha kuwa una shukrani kwa ajili ya yote ambayo Wao wamefanya kwa ajili ya yako.
Mtendee kila mtu kama mtoto wa Mungu. Kama mwanafunzi wa Yesu Kristo, unaweza kuwa mstari wa mbele katika kuwatendea watu wa mbari zote na dini zote na kundi lingine lolote kwa upendo na heshima—hususani wale ambao wakati mwingine ni waathiriwa wa maneno na vitendo vya kuumiza. Waendee wale ambao hujiona wapweke, wametengwa au wasio na msaada. Wasaidie wahisi upendo wa Baba wa Mbinguni kupitia wewe. Shiriki pamoja nao baraka alizokupa, na waalike wamfuate Yesu Kristo.
Hakikisha lugha yako inaakisi upendo kwa Mungu na kwa wengine—iwe unawasiliana uso kwa uso au kwa njia ya mtandao. Sema mambo ambayo yanainua—siyo kitu kinachoweza kuleta utengano, kinachoumiza au kinachokwaza, hata kama ni utani. Maneno yako yanaweza kuwa yenye nguvu kubwa. Acha yawe yenye nguvu kubwa kwa ajili ya mema.
Onyesha upendo kwa familia yako. Kuwapenda Watoto wote wa Mungu kunaanzia nyumbani. Timiza sehemu yako ili kuifanya nyumba yako kuwa mahali ambapo kila mtu anaweza kuhisi upendo wa Mwokozi.
Baraka Zilizoahidiwa
Uhusiano wako na Mungu utakuwa wa kina unapoonesha upendo wako kwa kutii amri Zake na kushika maagano yako na Yeye.
Uhusiano wako na wengine utakuwa wa kina unapoonesha upendo wako kupitia huduma kama ya Kristo. Utapata shangwe katika kuufanya ulimwengu kuwa mahali pa upendo zaidi.
Maswali na Majibu
Je, ninawezaje kuhisi upendo wa Mungu? Upendo wa Baba wa Mbinguni unapatikana siku zote. Zungumza Naye mara kwa mara kupitia sala. Shiriki hisia zako pamoja Naye, na kuwa msikivu kwa ajili ya misukumo kutoka Kwake. Soma maneno Yake katika maandiko. Tafakari kuhusu yote ambayo Yeye ameyafanya kwa ajili yako. Tumia muda katika sehemu na shughuli ambapo Roho Wake yupo.
Je, Bwana ananitarajia mimi kumpenda kila mtu, hata wale wanaonitendea vibaya? Bwana anakutarajia wewe kuwapenda maadui zako na kusali kwa ajili ya wale wanaokutendea vibaya. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba wewe unapaswa kukaa katika hali ambazo zinakusababishia maumivu kihisia, kimwili au kiroho. Weka mipaka ya kiafya ili kujiweka wewe mwenyewe salama. Kama unaonewa au kunyanyaswa, au kama unajua hii inafanyika kwa mtu mwingine, zungumza na mtu mzima anayeaminika.
Lini na kwa jinsi gani napaswa kuwajuwa waumini wa jinsia tofauti? Njia nzuri zaidi ya kuweza kuwajua wengine ni kupitia urafiki wa kweli. Unapokuwa kijana, jenga urafiki mwema na watu wengi. Katika baadhi ya tamaduni, vijana wanawajua wanajumuia wa jinsia tofauti kupitia shughuli za burudani za kikundi. Kwa ajili ya maendeleo na usalama wako kihisia na kiroho, shughuli na mtu mmoja mmoja zinapaswa kuahirishwa mpaka utakapokuwa umepevuka—umri wa miaka 16 ni mwongozo mzuri. Shauriana na familia yako na viongozi wako. Tunza uhusiano wa kipekee kwa ajili ya wakati utakapokuwa na umri mkubwa zaidi. Tumia muda na wale wanaokusaidia kutimiza ahadi zako kwa Yesu Kristo.
Je, nifanye nini kama nyumbani kwangu siyo mahali pa upendo? Mwokozi wako anajua hali yako na Yeye anakupenda. Kuwa na subira, endelea kushika amri za Mungu, na kuwa mfano mzuri kwa familia yako. Matendo yako rahisi ya upendo yanaweza kuleta tofauti kubwa. Unaweza pia kujenga uhusiano ndani ya familia yako ya kata. Jiandae sasa kujenga familia yako mwenyewe iliyojengwa juu ya msingi wa mafundisho ya Yesu Kristo. Kumbuka: Yesu Kristo ni nguvu yako!
Ona Isaya 58:3–11 (kusudi la kufunga); 58:13–14 (baraka za kuiheshimu Sabato); Malaki 3:8–10 (baraka za kulipa zaka); Luka 6:27–28 (wapende maadui zako); 10:25–37 (jirani yangu ni nani?); Yohana 3:16–17 (Mungu alitupenda, hata akamtoa Mwanaye); 14:15 (tunashika amri kwa sababu tunampenda Mungu); 1 Yohana 4:19 (tunampenda Mungu kwa sababu Yeye anatupenda); Mosia 2:17 (tunapowatumikia wengine, tunamtumikia Mungu).
Maswali ya Kibali cha Hekaluni
-
Je, unafuata mafundisho ya Kanisa la Yesu Kristo katika matendo yako ya faraghani na ya hadharani kwa wanafamilia yako na watu wengine?
-
Je, wewe ni mlipa zaka kamili?