1.
Mpango wa Mungu ni kwa ajili yako
Kabla ya wewe kuja duniani, uliishi na wazazi wako wa mbinguni. Wewe ni mtoto wao mpendwa. Mbinguni, ulijifunza kuhusu mpango wa Mungu kwa ajili ya familia Yake. Kwa shangwe wewe ulipokea mpango huu kwa sababu ungekusaidia kukua na kuendelea kuwa zaidi kama Mungu kwa kupokea mwili wa nyama na mifupa, kuwa sehemu ya familia ya kidunia, na kupata uzoefu wa maisha ya duniani. Baadhi ya uzoefu huu ungekuwa mgumu. Baba yetu alijua hili, hivyo kama sehemu ya mpango Wake, Alimtuma Mwokozi, Yesu Kristo, ili kukusaidia. Tunauita huu mpango wa wokovu au mpango wa furaha.
Kweli za milele
Baba wa Mbinguni ni mwandishi wa mpango huu. Yeye ni Baba wa roho yako, na Anakupenda. Anataka kukupa baraka Yake kuu zaidi—uzima wa milele pamoja Naye. Kwa maneno mengine, Anataka wewe uwe zaidi kama Yeye na kuishi maisha ya furaha, ya utukufu Yeye anayoishi. Yeye ana nguvu zote, na anajua yote. Unaweza kumtumaini Yeye, hata wakati maisha ni magumu.
Yesu Kristo anafanya mpango huu uwezekane. Kabla ya ulimwengu kuumbwa, Baba wa Mbinguni alimchagua Yeye kuwa Mwokozi wako. Yesu Kristo ndiye pekee anayeweza kukurudisha kwa Baba yako wa Mbinguni. Hii ndiyo sababu tunachagua kumfuata Yeye. Kila kitu kinategemea uchaguzi huo!
Ndoa na familia ni muhimu kwa mpango wa Mungu. Wewe ni sehemu ya familia ya Mungu, na watoto Wake wote wa kiroho huja duniani kupitia mama na baba. Mungu anataka mabinti zake na wanawe waendelee pamoja kuelekea ukamilifu wa milele. Wanaume na wanawake kila mmoja anachangia sawa sawa kwenye ndoa yenye upendo na umoja. Maisha ya familia hapa duniani—hata pamoja na mapungufu yake yote—yanaweza kuleta shangwe kuu. Yanakusudiwa kukuandaa wewe kwa ajili ya uzima wa milele pamoja na Mungu.
Mialiko
Shikilia mtazamo wa milele. Wakati wowote unapokabiliana na vishawishi, majaribu, kuvunjika moyo, au chaguzi ngumu, jikumbushe mwenyewe juu ya mpango wa Mungu. Ona jinsi kweli za milele unazozijua kuhusu mpango Wake zinavyoweza kukusaidia kuangalia changamoto zako kwa njia tofauti.
Tafuta mkono wa Mungu katika maisha yako. Tambua njia ambazo Mungu anakubariki. Yaweza kuwa tendo la ukarimu kutoka kwa mtu fulani, wakati wa amani, au jibu la sala.
Chagua kufuata mpango wa Mungu. Jifunze kuhusu kile Baba yako wa Mbinguni anachotaka ufanye. Tafuta mwongozo Wake unapojifunza maandiko, maneno ya manabii walio hai, tangazo la familia, na baraka yako ya kipatriaki. Hii itakusaidia wewe kujiandaa kumtumikia Bwana, kama mmisionari na katika maisha yako yote. Fanya huduma kwa Bwana, ndoa ya milele, na kuwalea watoto kuwa kipaumbele cha juu. Fanya sehemu yako ili kuwa na familia yenye furaha sasa kwa kufuata mafundisho ya Yesu Kristo.
Baraka Zilizoahidiwa
Unaweza kukabiliana na majaribu ya maisha kwa ujasiri na tumaini katika Kristo. Kwa sababu unajua kuhusu mpango wa milele wa Mungu, una chombo cha thamani ambacho kinaweza kukusaidia katika nyakati ngumu. Unajua kwamba kuna mengi zaidi kwenye maisha kuliko kile kinachotokea kati ya kuzaliwa na kifo. Unajua wewe ni nani hasa, dhumuni lako ni nini, na ni nani unaweza kuwa kwa msaada wa Mwokozi. Yesu Kristo ni nguvu yako.
Unaweza kupokea uzima wa milele unapomfuata Yesu Kristo. Atakupa uwezo wa kuwa zaidi kama Yeye, kurudi kwa wazazi wako wa mbinguni, na kuishi katika shangwe pamoja na wapendwa wako milele. Mtumaini Yesu Kristo.
Maswali na Majibu
Je, kwa nini maisha ni magumu sana wakati mwingine? Ninawezaje kupata nguvu? Uzoefu wako katika maisha haya—hata ule mgumu zaidi—unaweza kuwa kwa faida yako. Unaweza kukusaidia kukua na kuendelea pale unapomgeukia Mwokozi. Hakuna chochote unachopitia ambacho Yesu Kristo hakielewi kwa sababu ya dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Yeye anajua kwa usahihi jinsi ya kukusaidia. Fokasi maisha yako Kwake, na atakuinua juu ya mashaka yote na hofu zote.
Wakati mwingine, wazo la furaha katika familia na ndoa linaonekana kuwa mbali sana. Ni kwa jinsi gani ninaweza kupata kujiamini? Bila kujali hali yako, usikate tamaa juu ya mpango wa Baba wa Mbinguni. Yeye kamwe hatakata tamaa juu yako. Kama wewe ni mwaminifu kwa Mwokozi na maagano yako, utapata majibu katika mafundisho ya Yesu Kristo. Yeye anaelewa kila kitu unachopitia. Kupitia Kwake, utapata nguvu ya kutii amri za Mungu na kupokea baraka ambazo Yeye anaahidi. Mtumaini Yeye na injili Yake.
Ona 2 Nefi 9:13 (jinsi gani ulivyo mkuu mpango wa Mungu wetu!); Mosia 2:41 (wale wanaotii amri wanaweza kuishi na Mungu katika furaha isiyo na mwisho); Alma 12:28–34 (Mungu alifanya mpango wa ukombozi ujulikane kwa watoto Wake); Ibrahimu 3:22–26 (Mpango wa Mungu ulijumuisha kutupeleka duniani, ambapo tungeweza kuchagua wenyewe kufuata amri Zake).
Maswali ya kibali cha hekaluni
-
Je, una imani na ushuhuda juu ya Mungu, Baba wa Milele; Mwanaye, Yesu Kristo; na Roho Mtakatifu?