Vijana
3. Unaweza kusaidia katika kazi ya Mungu


Yesu Kristo akiwachunga na kuwatunza kondoo Wake.

3.

Unaweza kusaidia katika kazi ya Mungu

Musa 1:39

Baba wa Mbinguni anawapenda watoto Wake wote. Anataka kuwasaidia kupata furaha na shangwe, kurudi Kwake, na kupata uzima wa milele. Hii inaitwa kazi Yake ya wokovu na kuinuliwa, na Yeye anakualika kusaidia!

Kweli za milele

Kazi na utukufu wa Mungu ni kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu. Kutokufa ni kuishi milele tukiwa na mwili uliofufuka. Uzima wa milele, au kuinuliwa, ni kuwa zaidi kama Mungu na kuishi katika uwepo Wake milele kama familia. Haya yote yanawezekana kwa sababu ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Unaweza kumtumaini Yeye.

Unaweza kusaidia katika kazi ya Mungu kwa kuja kwa Kristo na kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo. Wakati wowote unapofanya chochote cha kumsaidia mtu kumfuata Yesu Kristo, unasaidia katika kazi ya Mungu.

Mialiko

Ishi injili. Jenga imani yako katika Yesu Kristo. Tubu kila siku. Pokea ibada za ukuhani wa Mungu na shika maagano yako. Fanya mpangilio huo kwa maisha yako yote.

Wajali wale walio katika shida. Tafuta njia za kuwahudumia na kuwatumikia wengine, ikijumuisha familia yako, marafiki zako, na jumuiya yako. Njia mojawapo kuu ya kuwasaidia watu wenye shida ni kutii sheria ya mfungo na kutoa matoleo ya mfungo.

Waalike wote kuipokea injili. Acha maneno yako na matendo yako yaakisi imani yako katika Yesu Kristo. Kuwa tayari kumwambia yeyote anayekuuliza kuhusu tumaini na furaha uliyo nayo kama mwanafunzi Wake. Kwa wavulana, kuhudumu misioni ni jukumu la ukuhani. Kwa wasichana, ni fursa yenye nguvu; sali ili kujua kama Bwana angetaka wewe uhudumu misioni. Jiandae kushiriki injili maisha yako yote.

Ziunganishe familia milele kwa kufanya historia ya familia na kazi ya hekaluni. Jifunze kuhusu mababu zako. Tafuta nani anahitaji ibada za hekaluni. Nenda hekaluni mara nyingi kadiri uwezavyo ili kubatizwa na kuthibitishwa kwa niaba yao. Kama unahitaji msaada, nenda kwenye FamilySearch.org.

Yesu Kristo akihudumu katika Mabara ya Amerika

Baraka Zilizoahidiwa

Utakuwa na msaada wa Mungu. Baba wa Mbinguni hatarajii wewe ufanye kazi hii pekee yako. Yeye yu pamoja nawe. Kwa unyenyekevu unapotoa muda na moyo wako, Yeye atafanya mambo ya kushangaza kupitia wewe. Yesu Kristo ni nguvu yako!

Utajawa na shangwe. Kazi ya Mungu ni kazi ya shangwe! Unaposhiriki katika kazi hii, unaweza kujisikia mwenye shangwe kama Yeye anavyojisikia. Fikiria shangwe utakayoshiriki na Baba wa Mbinguni na watoto Wake hao ambao wewe ulimsaidia kuwaleta Kwake!

Maswali na Majibu

Je, Mungu anaweza kweli kunitumia mimi katika kazi Yake? Ndiyo! Kuna njia nyingi za kusaidia katika kazi hii. Inaweza kuonekana kama watu wengine wana kipaji au ujuzi zaidi, lakini Baba yako wa Mbinguni anaona uwezekano wako. Amekupa karama ambazo unaweza kuzitumia kuwahudumia na kuwakusanya watoto Wake. Ni SAWA kama karama hizi ni tofauti na zile watu wengine walizo nazo. Kwa kweli, hiyo ndio sababu karama zako ni za thamani sana. Unahitajika!

Ona Mathayo 10:39 (kama utapoteza maisha yako katika huduma ya Mwokozi, utayaona); 1 Wakorintho 12:14–27 (viungo vyote vinahitajika katika mwili wa Kristo); Wafilipi 1:6 (jiamini kwamba Mungu anafanya kazi ndani yako); Yakobo 5:72 (Bwana wa shamba la mizabibu anafanya kazi pamoja nawe); Mafundisho na Maagano 18:15–16 (shangwe yako itakuwa kubwa kwa wale unaowaleta kwa Kristo); 64:33–34 (kazi kubwa huja kutokana na vitu vidogo na rahisi); Musa 1:6 (“Ninayo kazi kwa ajili yako”); 6:31–34 (Mungu huwastahilisha wale anaowaita, hata kama wanahisi hawatoshi).

Maswali ya Kibali cha Hekaluni

  • Je, unao ushuhuda juu ya Urejesho wa injili ya Yesu Kristo?