Vijana
7. Ibada na maagano hukupa kuzifikia baraka za Mungu


Yohana Mbatizaji anambatiza Yesu Kristo

7.

Ibada na maagano hukupa kuzifikia baraka za Mungu.

Mafundisho na Maagano 84:20

Baba yako wa Mbinguni ana hamu ya kukufundisha na kukubariki. Njia mojawapo anayofanya hili ni kupitia ibada kama ubatizo, uthibitisho, na sakramenti. Kupitia ibada kama hizi, tunafanya agano, au ahadi, na Mungu. Kushika maagano kunaongeza nguvu za Mungu katika maisha yako na hukusaidia kujiandaa kwa ajili ya uzima wa milele. Hii ndiyo sababu ibada na maagano ni vya thamani kwetu—kwa sababu yanaimarisha muunganiko wetu kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu na kutusaidia kuwa zaidi kama Wao.

Kweli za milele

Ibada zinakuelekeza kwa Yesu Kristo. Ibada ni sherehe takatifu yenye maana ya kiishara ambayo inafundisha kuhusu Yesu Kristo. Sakramenti, kwa mfano, si tu mkate na maji. Inatukumbusha juu ya Mwokozi.

Maagano ni ishara ya upendo, uaminifu na matarajio ya Mungu. Yanachukua uhusiano wako na Mungu kwa kiwango cha kina zaidi. Kufanya agano kunaonyesha kwamba unampenda Mungu na umejitolea kwa dhati Kwake. Unaweza kumtumaini Yeye, na Yeye anaweza kukuamini. Kwa ahadi hiyo ya kina huja ufikiaji mkubwa wa nguvu Zake na msaada kadiri unavyoshika maagano yako.

Unafanya maagano na Mungu wakati unapobatizwa na unaposhiriki sakramenti. Unapobatizwa, unaahidi kujichukulia juu yako jina la Yesu Kristo, kumtumikia Yeye, na kushika amri Zake maisha yako yote. Wakati wa sakramenti, pia unaahidi daima kumkumbuka Yeye. Hizi ni ahadi zako. Unapokuwa tayari kuzishika, Mungu anaahidi kukupa Roho Mtakatifu kama mwenza wa kudumu.

Mialiko

Ichukulie sakramenti kama zawadi takatifu. Onyesha ahadi yako kwa Yesu Kristo kwa kujiandaa kwa ajili ya tukio takatifu wakati wa sakramenti. Tafakari kile unachoweza kufanya ili kufanya ibada hii kuwa kielelezo chako cha kiroho cha wiki yako.

Mtafute Mwokozi katika ibada. Unapotazama au kushiriki katika ibada, jiulize, “Ninajifunza nini kutokana na hili kuhusu Yesu Kristo?” au “Ni kwa jinsi gani kinanileta karibu Naye?” Toa usikivu kwa kile Roho anachokufundisha.

Acha maagano yako yaongoze matendo yako. Unapokuwa na uchaguzi wa kufanya, kumbuka uhusiano wako wa agano na Mungu. Kuwa mwaminifu Kwake. Jiulize: Je, hili linaendana na maagano yangu? Kwa mfano, je, ninawapenda na kuwatumikia wengine, kuwafariji watu wanaohitaji faraja, na kusimama kama shahidi wa Kristo—kila mahali na daima?

Kristo mezani akiandaa sakramenti kwa ajili ya Wanefi

Baraka Zilizoahidiwa

Unaweza kuwa na uwezo wa kushinda vishawishi, dhambi, na majaribu ya maisha. Kufanya na kushika maagano hukupa kuzifikia nguvu za Mungu. Kwa nguvu hiyo, unaweza kukabiliana na cho chote kwa kujiamini. Yesu Kristo ni nguvu yako!

Unaweza kuwa safi na uliyesamehewa. Sehemu ya ahadi ya Mungu kwako kwa kushika agano lako la ubatizo ni ondoleo la dhambi zako. Hiyo inamaanisha kwamba unapotubu na kushika ahadi zako kwa Mungu, Yeye atakusamehe na kukusaidia kufanya vizuri zaidi.

Roho Mtakatifu anaweza kuwa pamoja na wewe siku zote. Ahadi nyingine iliyounganishwa kwenye ubatizo na sakramenti ni wenza wa kudumu wa Roho Wake na kuhudumiwa na malaika. Huna haja ya kuzikabili changamoto za maisha peke yako. Mungu kamwe hawatelekezi watoto Wake wa agano—unaweza kutegemea hilo.

Unaweza kuwa na msaada wa watu wa Mungu wa agano. Wewe ni wa sehemu ya watu wa agano katika Kanisa la Mwokozi. Mnainuana na kuhimizana. Mnaomboleza pamoja na kushangilia pamoja. Mnabebeana mizigo. Familia yako, askofu, viongozi, na waumini wengine wa Kanisa wako hapa kukusaidia, na wewe unaweza kuwasaidia.

Maswali na Majibu

Je, ninaweza kuwa mfuasi mzuri wa Yesu Kristo bila ibada na maagano? Kuna watu wengi wazuri ambao kwa dhati wanamfuata Yesu Kristo, ingawa hawajawahi kubatizwa au kufika hekaluni. Hata hivyo, Baba wa Mbinguni anawataka watoto Wake wote wapokee ibada Zake na kufanya maagano na Yeye ili kwamba waweze kupata ufikiaji mkubwa wa usaidizi Wake, rehema, na nguvu Zake. Hiyo ni mojawapo ya sababu kuu ambazo Yesu Kristo alirejesha Kanisa Lake! Kila mtoto wa Mungu atakuwa na fursa hiyo—katika maisha haya au yajayo—kukubali ibada na maagano yanayohitajika kwa ajili ya uzima wa milele.

Sijawahi daima kuwa mwaminifu kwa maagano yangu. Je, kuna tumaini kwa ajili yangu? Ndiyo! Injili ya Yesu Kristo ni injili ya matumaini na mianzo mipya! Hii ndiyo sababu tunapokea sakramenti kila wiki. Baba wa Mbinguni alijua tungefanya makosa na kuhitaji mwanzo mpya. Mwokozi alitoa uhai Wake ili kukupa njia ya kurudi. Unapotumia imani katika Yesu Kristo na kutubu, unaweza kupata tena ufikiaji wa nguvu za Mungu.

Ona 1 Wakorintho 11:23–26 (kupokea sakramenti kunaonyesha kwamba tunaamini katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake); Mosia 18:10, 13 (agano la ubatizo); Mafundisho na Maagano 13 (Ukuhani wa Haruni unajumuisha funguo za toba, ubatizo, na huduma za malaika); 20:37 (masharti ya ubatizo); 20:77, 79 (sala za sakramenti).

Maswali ya Kibali cha Hekaluni

  • Je, unajitahidi kuitakasa siku ya Sabato, kote nyumbani na kanisani; kuhudhuria mikutano yako; kujiandaa na kupokea sakramenti kwa kustahili; na kuishi maisha yako sawa sawa na sheria na amri za injili?