8.
Ibada na maagano ya hekaluni hukupa ufikiaji mkubwa zaidi kwenye baraka za Mungu
Baadhi ya baraka za Baba wa Mbinguni ni takatifu sana, Ametuamuru kuweka kando sehemu maalum, takatifu ambapo tunaweza kuzipokea: mahekalu. Hekaluni, nyumba ya Bwana, unaweza kupokea ibada Zake za juu zaidi—endaumenti na kuunganishwa—na kupokea ahadi Zake kuu.
Kweli za Milele
Endaumenti ni zawadi ya maarifa na nguvu. Katika ibada za endaumenti ya hekaluni, unajichukulia jina la Mwokozi juu yako mwenyewe kwa ukamilifu zaidi. Unaahidi kumtii Mungu, kujitolea dhabihu ya kufanya mapenzi Yake, kuishi injili ya Yesu Kristo, kutii sheria ya usafi wa kimwili, na kuweka wakfu—au kujitolea kwa dhati—maisha yako na vyote ambavyo Mungu amekupa kwa Kanisa Lake. Hizi ni ahadi zako. Mungu anaahidi kukubariki kwa ufahamu mkubwa, ulinzi, na ufikiaji wa nguvu Zake. Yeye pia anaahidi kukupa uzima wa milele pamoja Naye. Kama sehemu ya endaumenti, unapokea fursa takatifu ya kuvaa gamenti ya ukuhani mtakatifu. Gamenti ni ishara ya Yesu Kristo na ukumbusho wa maagano yako ya hekaluni.
Kuunganishwa hekaluni kunawaunganisha wanandoa na familia milele. Katika ibada ya kuunganishwa hekaluni, wewe na mwenza wako mtafanya agano na Mungu na ninyi kwa ninyi. Mtaahidi kuwa watiifu kikamilifu kwa Mungu na ninyi kwa ninyi, kupendana na kutumikiana, na kufanya kazi pamoja ili kutii sheria za Mungu. Hii ni ahadi yenu. Mungu anaahidi kwamba uhusiano wako na mwenza wako na watoto wako unaweza kudumu milele. Yeye pia anaahidi kwamba unaweza kupokea utukufu wa juu zaidi pamoja Naye katika ufalme wa selestia unaposhika maagano yako. Baraka hii inaitwa kuinuliwa.
Mialiko
Daima kuwa na kibali cha hekaluni. Kutana na mshiriki wa uaskofu wako ili kupokea kibali. Atakuuliza maswali kuhusu jinsi unavyoishi viwango vya Bwana kwa ajili ya kuingia katika nyumba Yake takatifu. Rejelea maswali haya mara kwa mara. (Unaweza kuyapata katika kiambatisho cha mwongozo huu.) Hata kama unaishi mbali na hekalu, acha kibali chako kiwe ishara ya upendo wako kwa Bwana na ahadi yako ya kuishi viwango Vyake.
Rejea hekaluni mara nyingi kadiri uwezavyo. Ukiwa na kibali chako cha hekaluni, unaweza kuingia katika nyumba ya Bwana na kubatizwa na kuthibitishwa kwa niaba ya mababu zako, ili nao waweze kupokea baraka ulizopewa. Chukua nafasi ya kila fursa ya kuwa hekaluni. Mtafute Bwana katika nyumba Yake. Mtafute Yeye katika ibada, ishara, na Roho unayemhisi. Utampata.
Jiandae kufanya maagano katika nyumba ya Bwana. Mojawapo ya njia bora ya kufanya hivyo ni kushika agano lako la ubatizo. Lifanye kuwa mojawapo ya malengo yako ya kuongoza kupokea ibada za hekaluni na kuwa mshika maagano wa maisha yote. Anza sasa kuishi sheria utakazoahidi kutii hekaluni: utiifu kwa amri za Mungu, dhabihu, injili ya Yesu Kristo, usafi wa kimwili, na kuweka wakfu. Familia yako, askofu, na viongozi wengine wa Kanisa wanaweza kukusaidia.
Baraka Zilizoahidiwa
Unaweza kuwa zaidi kama Yesu Kristo. Atakusaidia kuwa mfuasi mkubwa wa haki. Ibada na maagano ya hekaluni vitakufundisha jinsi ya kuingia katika uwepo wa Mungu na kupokea uzima wa milele pamoja Naye.
Utakuwa umejikinga kwa nguvu za Mungu. Maagano ya hekaluni huja na ahadi kwamba nguvu na utukufu wa Mungu vitakuwa juu yako. Malaika zake watakulinda.
Muda hekaluni utakuunganisha kwa karibu zaidi na Yesu Kristo na Roho Mtakatifu. Utahisi amani na pumziko la Mungu. Utaisikia sauti Yake kwa uwazi zaidi. Mbingu zitakufungukia, na utaelewa vyema njia Zake. Utakuwa na nguvu kubwa ya kukabiliana na changamoto zako kwa sababu moyo wako umeunganishwa na Wake.
Maswali na Majibu
Lini ninaweza kupokea endaumenti? Uamuzi wa kupokea endaumenti yako ni wa binafsi; fanya uamuzi huu kwa sala. Shauriana na familia yako na viongozi wako wa Kanisa. Ili kupokea endaumenti, unahitaji kuwa angalau na umri wa miaka 18 na haupo tena katika shule ya upili au sekondari. Utapokea endaumenti kabla ya kuhudumu misioni au kuunganishwa, lakini huna haja ya kusubiria mojawapo ya matukio haya kabla ya kupokea endaumenti. Unahitaji tu hamu na maandalizi ya kufanya na kushika maagano ya ziada na Baba yako wa Mbinguni. Askofu wako au rais wa tawi anaweza kukusaidia kujua kama umejiandaa. Usione endaumenti kama kazi kwenye orodha ya milele ya kuweka alama ya vema. Ione kama sehemu nzuri na tukufu ya safari yako ya milele ya kuja kwa Kristo na kupokea baraka kuu za kiroho za Mungu.
Kwa nini ninahitaji kibali cha hekaluni ili kuingia hekaluni? Hekalu ni nyumba ya Bwana, na Yeye ndiye anayeweka viwango vya kuingia ndani yake. Ibada hizi na maagano haya ya hekaluni ni matakatifu sana kiasi kwamba yanahitaji maandalizi maalum ya kiroho. Usaili wa kibali cha hekaluni unakusudiwa kuhakikisha kwamba umejiandaa kiroho kwa ajili ya fursa za juu zaidi za maagano ya hekaluni. Baba wa Mbinguni anawaalika watoto Wake wote kujiandaa kufanya ahadi na Yeye katika nyumba Yake takatifu.
Je, ninahitaji kuwa mkamilifu ili kufanya maagano ya hekaluni? Hakuna mtu aliye mkamilifu. Mungu anakuomba uwe mwaminifu na aliye tayari kutii amri Zake. Kufanya na kushika maagano na Mungu ndicho kinachokupa nguvu ya kuwa mkamilifu kupitia Yesu Kristo. Yeye ni nguvu yako!
Ona Isaya 2:2–3 (Mungu hutufundisha njia Zake hekaluni); Mathayo 11:28–30 (jitieni nira ya Mwokozi); 1 Nefi 14:14 (nguvu za Mungu ziko juu ya watu Wake wa agano); Mafundisho na Maagano 97:15–16 (Uwepo wa Mungu na utukufu Wake viko katika nyumba Yake); 109:22 (ndani ya hekalu tunakingwa kwa nguvu za Mungu); 131:1–4; 132:4–6, 15–20 (ili kupokea uzima wa milele, mwanamume na mwanamke lazima watiwe muhuri kwa milele kupitia agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa); Ibrahimu 1:2 (Ibrahimu alitaka kuwa mfuasi mkubwa wa haki na kupokea maarifa makubwa zaidi).
Maswali ya Kibali cha Hekaluni
-
Je, unajiona kuwa ni mwenye kustahili kuingia katika nyumba ya Bwana na kushiriki katika ibada za hekaluni?