Vijana
5. Enenda katika nuru ya Mungu


Yesu Kristo akichunga kundi la kondoo

Sitapungukiwa na Kitu, na Yongsung Kim Kwa hisani ya Havenlight

5.

Enenda katika nuru ya Mungu

Wagalatia 5:25

Unafanya chaguzi bora unapoona mambo kwa uwazi zaidi. Hiyo ndiyo sababu nuru ni muhimu sana; nuru inafanya iwe rahisi kuona njia sahihi. Baba wa Mbinguni amekupa wewe fursa ya kukifikia chanzo cha nuru ya mbinguni—kipawa cha Roho Mtakatifu—ili kukusaidia kuona kwa uwazi kilicho chema na kibaya, sahihi na kisicho sahihi.

Kweli za milele

Unaweza kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenza wako daima. Wakati ulipothibitishwa kuwa muumini wa Kanisa, ulialikwa “kumpokea Roho Mtakatifu.” Fursa ya kuwa na Roho kama mwenza wako daima ni mojawapo ya zawadi kuu za Mungu kwako.

Kufanya chaguzi nzuri kunaboresha uwezo wako wa kumhisi Roho. Kuna mambo mengi mazuri na yenye kuleta siha katika ulimwengu huu. Kama vile mwili wako unavyoathiriwa na kile unachokula na kunywa, akili yako na roho yako vinaathirika kwa kina kwa kile unachosoma, kuangalia na kusikiliza.

Mialiko

Tenga muda kwa ajili ya Bwana kila siku. Jifunze kuhusu Yeye. Daima mkumbuke Yeye. Sali kwa Baba yako wa Mbinguni. Jifunze maandiko matakatifu na maneno ya manabii walio hai. Kisha jitahidi kuishi kwa kile unachojifunza.

Tafuta kile ambacho kinainua, kinavutia na kinamwalika Roho. Unapofanya chaguzi kuhusu nini cha kuangalia, kusoma, kusikiliza au kushiriki, fikiri kuhusu jinsi kinavyokufanya wewe ujisikie. Je, kinaalika mawazo mazuri? Kaa mbali na kitu chochote ambacho kinadhihaki vitu vitakatifu au kile ambacho siyo cha kimaadili. Usishiriki katika kitu chochote ambacho kinafifisha uamuzi wako au usikivu wako kwa Roho, kama vile vurugu, kileo, na dawa za kulevya. Kuwa na ujasiri wa kuzima video au mchezo, kutoka nje ya sinema au dansi, kubadilisha muziki wako, au kugeuka kabisa mbali na chochote ambacho hakina maelewano na Roho.

Tumia mitandao ya kijamii ili kuinua. Mitandao ya kijamii inaweza kuwa nyenzo yenye nguvu kimawasiliano. Kama unaitumia, fokasi kwenye nuru, imani na ukweli. Usifananishe maisha yako na kile watu wengine wanachokipitia. Kumbuka kwamba thamani yako inakuja kutokana na kuwa mtoto wa wazazi wa mbinguni, siyo kutokana na mitandao ya kijamiii.

Tafuta matukio yenye kuleta siha na uhusiano wa kweli, na wa kudumu. Kuwa makini kwamba matumizi yako ya teknolojia na mitandao ya kijamii havichukui nafasi ya wewe kutumia muda binafsi pamoja na familia na marafiki. Mitandao ya kijamii na teknolojia nyinginezo vinaweza kuchukua muda wako mwingi bila kukupa thamani ya kutosha kama malipo. Pumzika kutoka kwenye ulimwengu wa mitandao na unganika na watu katika maisha halisi.

Yesu Kristo akiongoza kundi la kondoo juu ya shamba la nyasi

Baraka Zilizoahidiwa

Roho anaweza kuwa pamoja na wewe siku zote. Ahadi hii ni sehemu ya agano unalofanya kila wakati unaposhiriki sakramenti. Roho Mtakatifu atatoa ushahidi kwako juu ya Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Yeye atakufariji, atakuongoza, atakuonya na kukutakasa. Yeye atakusaidia kutambua ukweli na kuona mema katika ulimwengu.

Maswali na Majibu

Nawezaje kujua kama ninamhisi Roho Mtakatifu? Kujifunza kumtambua Roho inachukuwa muda, mazoezi na subira. Yeye huzungumza na watu tofauti katika njia tofauti. Usidharau vitu rahisi—hisia za amani unazopata kwa kusikiliza ushuhuda wa mtu fulani au hisia ya kukosa amani unayopata baada ya kufanya uchaguzi usio sahihi. Pekua kwenye maandiko ili kujua njia tofauti ambazo Roho huwasiliana, sali kuhusu hilo, na endelea kutafuta kwa ajili ya fursa za kumhisi Roho.

Ponografia ni nini? Kwa nini ninapaswa kuiepuka? Ponografia ni uwakilishi, katika picha au maneno, ambao umesanifiwa ili kuamsha hisia za kujamiiana. Ponografia inakuja katika aina nyingi, ikijumuisha video, picha, vitabu, michezo, na muziki. Inaweza pia kuwa jumbe au picha zilizotumwa kati ya marafiki. Ponografia inavitendea vitu ambavyo ni vitakatifu—maumbile yetu ya kimwili na hisia za kijinsia—bila heshima. Yawezekana ukakutana na ponografia pasipo kukusudia kufanya hivyo. Iwe umekutana na ponografia kwa kukusudia au la, achana nayo mara moja. Unaweza pia kuzungumza na mzazi au mtu mzima mwingine anayeaminika. Kuangalia kwa makusudi ponografia ni dhambi na inadhuru uwezo wako wa kumhisi Roho. Inadhoofisha uwezo wako wa kujitawala na inaathiri jinsi unavyojiona wewe mwenyewe na unavyowaona wengine. Yesu Kristo anao uwezo wa kukusaidia kuishinda ponografia na kutubu. Mgeukie Yeye na ondoka kutoka kwenye giza. Askofu wako anaweza kukusaidia kupata nguvu na msamaha kupitia kwa Mwokozi. Yesu Kristo ni nguvu yako!

Ona Zaburi 119:105 (Neno la Mungu ni kama nuru kwenye njia yetu); Amosi 5:14 (tafuteni mema); Wagalatia 5:22–23 (tunda la Roho); Moroni 7:18–19 (nuru ya Kristo); Mafundisho na Maagano 6:23 (Bwana husema amani); 20:77, 79 (sala za sakramenti).

Maswali ya kibali cha hekaluni

  • Bwana amesema kwamba mambo yote lazima “yafanyike katika usafi” mbele Yake (Mafundisho na Maagano 42:41). Je, unajitahidi kwa usafi wa kimaadili katika mawazo na tabia zako?