Vijana
10. Mwili wako ni mtakatifu


baba na mama na mtoto

Familia Ikitazama Kuelekea Kwenye Nuru, na Lovetta Reyes Cairo. Kwa hisani ya Havenlight

10.

Mwili wako ni mtakatifu

1 Wakorintho 6:18–20

Mwili wako ni zawadi ya kupendeza kutoka Baba wa Mbinguni. Kuwa na mwili kunakupa wewe ongezeko la nguvu ya kutumia uhuru wako wa kuchagua kati ya kilicho sahihi na kisicho sahihi. Injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo inaweza kukusaidia kuuona mwili wako katika mtazamo wa Mungu. Na hiyo inaleta tofauti kubwa katika chaguzi zako kuhusu nini cha kufanya kwa mwili wako na jinsi ya kuutunza.

Kweli za Milele

Mwili wako ni katika mfano wa Mungu—Kiumbe aliye mtukufu, wa kifalme zaidi katika ulimwengu huu. Maandiko yanaifananisha miili yetu na hekalu takatifu, mahali ambapo Roho anaweza kuishi. Ni kweli, mwili wako siyo mkamilifu kwa sasa. Lakini mambo unayopitia kwa mwili wako yanaweza kukusaidia kujiandaa siku moja kupokea mwili mkamilifu, uliofufuliwa, mwili uliotukuka.

Nafsi yako imeundwa na mwili wako na roho yako. Kwa sababu hii, afya ya kimwili na afya ya kiroho vina uhusiano wa karibu. Mwokozi alifunua neno la hekima ili kufundisha kanuni za kuutunza mwili wako na kuahidi baraka za kimwili na za kiroho.

Hisia za kijinsia ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu ili kuunda ndoa zenye furaha na familia za milele. Hisia hizi siyo za dhambi—ni takatifu. Kwa sababu hisia za kijinsia ni takatifu mno na zenye nguvu mno, Mungu amekupatia sheria Yake ya usafi wa kimwili ili kukuandaa wewe kutumia hisia hizi jinsi Yeye anavyokusudia. Sheria ya usafi wa kimwili inasema kwamba Mungu anaidhinisha shughuli za kujamiiana kati ya mwanamume na mwanamke tu ambao wamefunga ndoa. Watu wengi wanapuuza au hata kudhihaki sheria hii ya Mungu, lakini Bwana anatualika sisi kuwa wanafunzi Wake na kuishi kiwango cha juu zaidi.

Mialiko

Utendee mwili wako—na miili ya wengine—kwa heshima. Unapofanya maamuzi kuhusu mavazi yako, mtindo wa nywele na mwonekano, jiulize mwenyewe, “Je, ninauheshimu mwili wangu kama zawadi takatifu kutoka kwa Mungu?” Baba wa Mbinguni anatutaka sisi kumwona kila mmoja wetu jinsi tulivyo kiuhalisia: siyo tu maumbile ya kimwili bali kama watoto Wake wapendwa wenye hatima ya kiungu. Epuka mitindo ambayo inatia mkazo au kuvuta hisia zisizo sahihi kwenye maumbile ya mwili wako badala ya wewe ni nani kama mtoto wa Mungu mwenye siku za baadaye za milele. Acha usafi wa kimaadili na upendo kwa Mungu viongoze chaguzi zako. Tafuta ushauri kutoka kwa familia yako.

Fanya mambo ambayo yataimarisha mwili wako—siyo mambo ambayo yatauumiza au kuuharibu. Furahia kwa shukrani vitu vizuri vingi ambavyo Mungu amevitoa. Kumbuka kwamba vileo, tumbaku, kahawa, chai na madawa na vitu vingine vya kulevya siyo kwa ajili ya mwili wako wala kwa roho yako. Hata vitu vyenye kusaidia, kama vile dawa ambazo ni maagizo ya daktari, zinaweza kuwa na uharibifu kama hazikutumika kwa usahihi.

Fanya jinsia na hisia za kujamiiana kuwa takatifu. Hazipaswi kuwa suala la mzaha au burudani. Nje ya ndoa kati ya mwanamume na mwanamke, ni makosa kugusa sehemu za siri, sehemu takatifu za mwili wa mtu mwingine hata kama amevaa nguo. Katika chaguzi zako kuhusu nini cha kufanya, kutazama, kusoma, kusikiliza, kufikiri kuhusu, kuposti au kuandika ujumbe, epuka kitu chochote kile ambacho kwa makusudi kinaamsha hisia za matamanio kwa wengine au kwako wewe mwenyewe. Hii inajumuisha ponografia katika aina yoyote. Kama unaona kwamba hali au shughuli hizo zinafanya majaribu kuwa yenye nguvu, ziepuke. Unajua hali na shughuli hizo ni nini. Na kama huna hakika, Roho, familia yako na viongozi wako wanaweza kukusaidia kujua. Mwonyeshe Baba yako wa Mbinguni kwamba unaheshimu na kujali nguvu takatifu za kuumba uhai.

Yesu Kristo akifikiria na kuegemea fimbo yake

Baraka Zilizoahidiwa

Kujiheshimu kwako wewe mwenyewe na kuwaheshimu wengine kutaongezeka unapokuwa unauheshimu mwili wako kupitia tabia yako, mwonekano wako na uvaaji wako.

Bwana ameahidi hazina kuu za maarifa kwa wale wanaoshika Neno la Hekima. Mwili wenye afya, ulio huru kutokana na uraibu, pia unaongeza uwezo wako wa kupokea ufunuo binafsi, kufikiri kwa uwazi na kumtumikia Bwana.

Kuishi sheria ya usafi wa kimwili kunaleta kukubalika na Mungu na nguvu binafsi ya kiroho. Kunakulinda wewe na familia yako ya baadaye. Utakapofunga ndoa, sheria hii italeta upendo mkubwa zaidi, tumaini, na umoja kwenye ndoa yako. Kutii sheria hii kutakuwezesha wewe kuendelea milele na kuwa zaidi kama Baba yako wa Mbinguni. Kujiamini kwako kutakua unapoishi kama mwanafunzi wa Yesu Kristo.

Maswali na Majibu

Je, ni nini kiwango cha Bwana juu ya mavazi, maadili, chanjo za michoro ya mwilini, na kutoga? Kiwango cha Bwana ni kwa wewe kuheshimu utakatifu wa mwili wako, hata wakati ambapo hiyo inamaanisha kuwa tofauti na watu wengine. Acha ukweli huu na Roho viwe mwongozo wako unapofanya maamuzi—hususani maamuzi ambayo yana matokeo ya kudumu kwenye mwili wako. Kuwa mwenye busara na mwaminifu na tafuta ushauri kutoka katika familia yako na viongozi wako.

Ni kwa jinsi gani ninaweza kushinda majaribu na mazoea mabaya? Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanao uwezo wa kukusaidia. Jaza maisha yako kwa vitu ambavyo vinaalika uwezo Wao katika maisha yako, kama vile sala, kujifunza maandiko na huduma kwa wengine. Mgeukie Yesu Kristo na injili Yake na utagundua kwamba udhaifu unaweza kuwa uthabiti. Tafuta msaada kutoka kwenye familia, viongozi na washauri wenye taaluma kama inahitajika. Wanaweza kukusaidia kupata tena udhibiti wa maisha yako. Yawezekana ikachukuwa muda, kwa hiyo kuwa na subira, na kamwe usikate tamaa.

Ninavutiwa na watu wa jinsia kama yangu. Ni kwa jinsi gani viwango hivi vinahusika kwangu? Kuhisi kuvutiwa na mtu wa jinsia moja na wewe siyo dhambi. Kama unazo hisia hizi na huzifuatilii au kuzitendea kazi, unaishi sheria takatifu ya usafi wa kimwili ya Baba wa Mbinguni. Wewe ni mtoto mpendwa wa Mungu na ni mwanafunzi wa Yesu Kristo. Kumbuka kwamba Mwokozi anaelewa kila kitu unachopitia. Kupitia muunganiko wako wa agano na Yeye, utapata nguvu ya kutii amri za Mungu na kupokea baraka ambazo Yeye anaahidi. Mtumaini Yeye na injili Yake.

Nilifanyiwa unyanyasaji na ninaona aibu. Je, nina hatia ya dhambi? Hapana. Kuwa mwathirika wa unyanyasaji wowote au shambulio lolote hakukufanyi wewe uwe na hatia ya dhambi. Mwokozi anakupenda. Yeye ni nguvu yako. Yeye anataka kukusaidia, kukuponya na kukupa amani. Wataalamu wa ushauri, washiriki wa familia yako na viongozi wako wanaweza pia kukusaidia.

Ona Mwanzo 1:27 (tupo katika mfano wa Mungu); Yohana 14:18 (Mwokozi anaahidi faraja); Wafilipi 4:7 (amani ya Mungu hupita uelewa); Mosia 2:41 (wale wanaotii amri za Mungu wanabarikiwa kimwili na kiroho); Mafundisho na Maagano 88:15 (roho na mwili ni nafsi); 89 (Neno la Hekima); 121:45 (mawazo mema huelekeza kwenye ongezeko la kujiamini).

Maswali ya Kibali cha Hekaluni

  • Bwana amesema kwamba mambo yote lazima “yafanyike katika usafi” mbele Yake (Mafundisho na Maagano 42:41). Je, unajitahidi kwa ajili ya usafi wa kimaadili katika mawazo na tabia zako?

  • Je, unatii sheria ya usafi wa kimwili?

  • Je, unaelewa na kutii Neno la Hekima?