Sura ya 24
Binti wa Yairo Anafufuliwa kutoka Wafu
Siku moja Yairo, mtawala wa sinagogi, alianguka miguuni pa Mwokozi.
Marko 5:21–22
Yairo alisema kwamba binti yake wa miaka 12 alikuwa mgonjwa sana. Alimuomba Yesu aende na kumbariki. Aliamini kwamba Yesu angemponya.
Marko 5:23, 42
Yesu alianza kumfuata Yairo nyumbani, lakini alisimama ili kumponya mwanamke. Alipokuwa akiongea naye, mtu alikuja kumwambia Yairo kwamba alikuwa amechelewa sana—bintiye alikuwa amekufa.
Marko 5:24–35
Yesu alisikia kile kilichosemwa. Alimwambia Yairo asiwe na hofu lakini amuamini Yeye.
Marko 5:36
Kisha Yesu akaenda na Yairo nyumbani kwake. Nyumba ilikuwa imejaa watu ambao walikuwa wakilia kwa sababu ya kifo cha msichana huyo mdogo.
Marko 5:37–38
Yesu aliwaambia kwamba msichana hakuwa amekufa ila alikuwa amelala. Watu walimcheka. Walikuwa na uhakika msichana alikuwa amekufa.
Marko 5:39–40
Mwokozi alitaka kila mtu aondoke ndani ya nyumba isipokuwa wanafunzi Wake, Yairo na mkewe Yairo. Walienda chumbani ambako msichana huyo mdogo alikuwa amelala.
Marko 5:40
Yesu alimshika msichana kwa mkono. Alimwambia aamke. Alisimama na kutembea. Wazazi wake walishangaa. Yesu aliwaambia wasimwambie yeyote kile kilichotokea. Kisha Yeye aliwaambia wazazi wake wampe msichana kitu cha kula.
Marko 5:41–43