2025
Kuliwazwa na Bwana ili Kulala
Julai 2025


“Kuliwazwa na Bwana ili Kulala,” Liahona, Julai 2025.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Kuliwazwa na Bwana ili Kulala

Mungu alisaidia kumtuliza mwana wetu na kunifariji wakati tulipohitaji sana.

kielelezo cha mtoto amelala akiwa amewekewa mashine ya EEG

Kielelezo na David Malan/Malan Creative

Wakati mtoto wetu wa kwanza, Caden, alipokuwa na umri wa miezi 10, mume wangu, David, pamoja nami tulimwacha akiwa chini ya utunzaji wa wazazi wangu kwa mara ya kwanza. Tulienda nje kwa chakula cha jioni na kisha tukaenda kwenye ukumbi wa sinema. Mara tulipopata bisi zetu na kukaa chini, mama yangu alipiga simu.

Mtoto wetu hakuwa anapumua, na gari la wagonjwa lilikuwa njiani!

Tuliendesha gari kurudi nyumbani kwa hofu na kukimbia ndani na kumwona Caden mikononi mwa mama yangu, akitabasamu kwa wahudumu wa dharura. Alikuwa sawa, lakini alikuwa amepitia mshituko wa moyo.

Madaktari hawakuweza kuamua chanzo cha mshituko huo au mishtuko mawili ya baadaye, lakini waliagiza dawa ili kusaidia. Kama mama wa mara ya kwanza, nilihuzunishwa. Caden alionekana sawa, lakini uzoefu ulitikisa imani yangu. Niliumia sana kwa mfadhaiko na wasiwasi.

Miaka miwili baadaye mtaalamu wa neva alipendekeza kufanya electroencephalogram (EEG) kwa Caden, uchunguzi ambao ungepima hali ya utendaji wa ubongo wake akiwa amelala. Ikiwa matokeo yalionekana mazuri, angeweza kuacha kutumia dawa za mshituko wa moyo.

Nilikuwa na wasiwasi juu ya uchunguzi huu kwa sababu Caden alikuwa ameacha kupata mapumziko madogo ya usingizi mwaka mmoja uliopita. Ni kwa jinsi gani tungemfanya kulala katika ofisi ya daktari mwenye shughuli nyingi na elektrodi kichwani mwake?

Usiku kabla ya uchunguzi, David alimpa Caden baraka ya ukuhani. Baraka ilipoanza, nilihisi uwepo imara wa Roho. Nilijua kila kitu kitakuwa SAWA. Hii ilikuwa ndio mara ya kwanza tangu mshituko wake wa kwanza kwamba nilihisi amani.

Siku iliyofuata madaktari walishikiza elektrodi kwenye kichwa cha Caden. Kisha tukamweka kwenye meza ya uchunguzi na kuzima taa.

Alilala ndani ya dakika chache. Hii inaweza kuonekana kama muujiza, lakini hakuwa amepata mapumziko ya usingizi mwenyewe kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Baba wa Mbinguni hakuwa ametusahau. Roho wake alikuwa pale katika ofisi ya daktari, akimtuliza Caden na kunifariji. Mtazamo wangu juu ya majaribu na baraka za ukuhani ulibadilika siku hiyo. Ninajua kwamba nguvu ya ukuhani ni halisi.

Caden sasa ni kijana mkubwa. Hajapata mshituko tangu alipokuwa mtoto. Amekumbana na changamoto zingine lakini ameshinda nyingi kati ya hizo. Ninajua kwamba Bwana anaendelea kumlinda na kutuliza hofu zangu (ona Luka 8:50).