2025
Pata Shangwe katika Safari Yako ya Injili
Julai 2025


“Pata Shangwe katika Safari Yako ya Injili,” Liahona, Julai 2025.

Pata Shangwe katika Safari Yako ya Injili

Matokeo ya mwisho ya kuonyesha upendo wetu kwa Bwana kwa kutii amri Zake ni baraka ambazo huleta furaha na shangwe.

waumini wa Kanisa wanaotabasamu huko Thailand

Picha ya waumini wa Kanisa wenye shangwe nchini Thailand na Christina Smith

Wakati nikihudumu kama kiongozi wa misheni huko Japani miaka kadhaa iliyopita, nilihudhuria mkutano wa wikiendi katika mji wa vijijini kwenye moja ya pembe za mbali za misheni yetu. Rais wa wilaya alikuwa ameniandalia kufanya mahojiano na mtu ambaye alikuwa amejiunga na Kanisa mwaka mmoja nyuma na alikuwa akitafuta kupokea kibali cha hekaluni. Alitumaini kupokea endaumenti yake mwenyewe au karibu na maadhimisho ya mwaka mmoja wa ubatizo wake.

Wakati wa mazungumzo yetu, muumini huyu mpya alielezea jinsi alivyokuwa na shukrani kwa ajili ya baraka tele alizopokea katika mwaka tangu alipobatizwa. Alifurahia kuhudhuria sakramenti kila wiki na mikutano mingine. Alijihusisha sana na shughuli za tawi lake. Kwangu mimi, alitoa imani ya agano kutokana na kuelewa madhumuni yake ya injili, ambayo sasa ilikuwa sehemu yake muhimu. Alikuwa mfuasi mwongofu wa Kristo ambaye alipata mabadiliko makuu ya moyo ( ona Mosia 5:2).

Mazungumzo yetu yote yalifuata mpangilio wa matumaini. Tulijadili ibada na maagano ambayo yangekuwa sehemu ya uzoefu wake wa hekaluni. Kwa uwazi alijibu kila moja ya maswali ya kawaida yanayohusiana na kupokea kibali cha hekaluni.

Kufuatia mahojiano hayo, nakumbuka nikitoa maoni kwa rais wa wilaya jinsi nilivyokuwa na shukrani kukutana na mtu huyo bora. Nilimwambia jinsi nilivyovutiwa kwamba wamisionari na waumini walikuwa wamempata, na kumlea kiroho, mtu wa aina hiyo ya uadilifu na ahadi.

Nilishangazwa wakati rais wa wilaya aliposhiriki kwamba wakati mtu huyu alipoanza kupokea masomo kutoka kwa wamisionari na kuhudhuria kanisani zaidi ya mwaka mmoja uliopita, hakuwa na makazi na alikuwa mgumu sana—karibu kupoteza hali yote ya—tumaini. Rais wa wilaya kisha alielezea jinsi kujifunza injili kwa ndugu huyu na uongofu wake kwa kipindi cha miezi kulivyopelekea mabadiliko yake ya kimiujiza, kumweka kwenye njia ya kujitegemea kiroho na kimwili na kumpa hisia ya kusudi na shangwe.

Injili ilimpa picha wazi ya madhumuni ya maisha yake. Kweli halisi na za thamani za injili zilileta majibu kwa maswali muhimu ya maisha ya duniani, kuanzia na ufahamu kwamba “Mungu ni Baba yetu wa Mbinguni, na sisi ni watoto Wake. … Mungu anatujua sisi binafsi na anatupenda.” Katika mpango Wake, “Baba wa Mbinguni ametoa … vipawa vingi na miongozo kutusaidia kurudi kwenye uwepo Wake.”

Hiyo ndiyo ilikuwa baraka kwa mtu huyu, ambayo ipo sawa kwa watoto wote wa Mungu kupitia injili ya Yesu Kristo.

Madhumuni ya Maisha

Kwa sababu Yesu Kristo alirejesha injili Yake kupitia Nabii Joseph Smith, “tuna uelewa wa madhumuni ya maisha, ya sisi ni kina nani,” alitangaza Rais M. Russell Ballard (1928–2023). Katika ushuhuda wake wa mwisho kwa Kanisa, Rais Ballard, Wakati huo-Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alisema:

“Tunajua Mungu ni nani; tunajua Mwokozi ni nani, kwa sababu tunaye Joseph, ambaye alikwenda kwenye kijisitu kama mvulana, akitafuta msamaha wa dhambi zake. …

“Ninashangazwa na naamini ni vivyo hivyo kwa wengi wenu, juu ya jinsi gani ambavyo tumebarikiwa kujua kile tunachokijua na kujua kuhusu dhumuni letu kwenye maisha, kwa nini tuko hapa, kipi tunatakiwa kujitahidi kukifanya na kukikamilisha kwenye maisha yetu ya kila siku.”

Kwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, maarifa hayo yanajumuisha uelewa wa “mpango mkamilifu” wa Mungu wa wokovu. Pia unajulikana kama “mpango mkuu wa furaha,” “mpango wa ukombozi,” na “mpango wa rehema” (Alma 42:8, 11, 15), “unaondoa siri kutoka kwenye maisha na mashaka kutoka siku zetu za usoni.” Muhimu katika mpango huo ni “mafundisho ya Kristo,” ambayo ni kitovu cha madhumuni ya maisha.

Kwa sababu tuna injili, tunajua sisi ni watoto wa Mungu, tuliotumwa duniani kujaribiwa, kuboreshwa, na kutayarishwa “kuletwa kwa njia ya ufufuo wa wafu, kupitia kwa ushindi na utukufu wa Mwanakondoo” (Mafundisho na Maagano 76:39). Tunajua amri na tunaelekezwa “vya kutosha kwamba [sisi] tujue mema na maovu” (2 Nefi 2:5). Tunajua tuko duniani kupenda na kuhudumu. Na tunajua kwamba Mwokozi ametuita kuushinda ulimwengu na kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo (ona Yohana 16:33; Mafundisho na Maagano 64:2) katika maandalizi kwa ajili ya Ujio Wake wa Pili.

Tunapofokasi Kwake, kile ambacho Joseph Smith anachokiita “sauti ya kushangilia ya Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo” kitatuimarisha wakati wa siku ngumu na kuleta maana na lengo kwenye maisha yetu na katika maisha ya wengine.

Yesu Kristo

Kila Goti Litapigwa, na Dan Wilson, isinakiliwe

Utiifu, Baraka, Shangwe

Mungu ametupa haki ya kujiamulia kimaadili ili kwamba tuweze kuwajibika kwa chaguzi zetu (ona Mafundisho na Maagano 101:78; 2 Nefi 2:16). Kama sehemu ya “upinzani katika vitu vyote” (2 Nefi 2:11), Shetani anaruhusiwa kutujaribu kutumia vibaya haki yetu ya kujiamulia.

Lakini Bwana Yesu Kristo, “akijua majanga yajayo juu ya wakazi wa dunia” katika siku yetu, alimwita Nabii Joseph Smith, “akamwambia kutoka mbinguni, naye akampa amri” (Mafundisho na Maagano 1:17). Mpangilio huo ambao Bwana hufunua amri Zake na mapenzi Yake kwa manabii Wake unaendelea katika siku yetu na Rais Russell M. Nelson—na kwa sababu hiyo hiyo. Mungu anatamani kutuongoza kwenye furaha katika maisha haya na kwa utukufu wa selestia katika maisha yajayo.

Utiifu kwa amri za Mungu unapaswa kuja kutokana na kujitoa kwetu kwa na upendo kwa ajili Yake. Bwana Yesu Kristo Mwenyewe alitangaza kwamba kumpenda Mungu “ni amri ya kwanza na kuu” (ona Mathayo 22:37–38). Alitoa umaizi zaidi alipotangaza, “Mkinipenda mtazishika amri zangu” (Yohana 14:15).

Kuna thawabu ya kumpenda Bwana na kushika amri Zake. Katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu alielezea “sheria, isiyotenguliwa iliyowekwa mbinguni … , ambapo juu yake baraka zote hutoka—

“Na kama tunapata baraka yoyote kutoka kwa Mungu, ni kutokana na utii kwa sheria ile ambayo juu yake hutoka” (Mafundisho na Maagano 130:20–21).

Hivyo, matokeo ya mwisho ya kuonyesha upendo wetu kwa Bwana kwa kutii amri Zake ni baraka ambazo huleta furaha na shangwe.

Kuangalia maisha kupitia lenzi ya injili ya urejesho na ufunuo wa kisasa hutupatia uwazi. Tukiwa na mtazamo wazi wa asili yetu takatifu na hatima, tunajua kwamba “mambo yale yale yatakayofanya maisha [yetu] ya duniani kuwa bora zaidi kadiri iwezekanavyo yanaweza kuwa sawa kabisa na mambo yale yatakayofanya maisha [yetu] milele yote yawe bora zaidi!”

Hitimisho

Ninahitimisha nilipoanzia, nikikumbuka uzoefu wangu miaka iliyopita na mwongofu wa hivi karibuni huko Japani. Kupitia bidii yake na bidii ya wamisionari na waumini, alipata injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Katika kuipata injili, aligundua pia kusudi lake, ambalo lilipanua ono lake. Pia alipata mpango mkuu wa furaha. Utiifu kwa maagano ya injili ya mpango huo ulimletea baraka na shangwe, ukimwinua kimwili na kiroho.

Safari yake ikiongoza kwenye uumini katika Kanisa la Yesu Kristo ilimruhusu kuwa shahidi wa Yesu Kristo. Mzee Patrick Kearon wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili ameelezea shangwe inayofuata:

“Kwa sababu ya mpango wa upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mmoja wa watoto Wake, na kwa sababu ya maisha ya ukombozi na misheni ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo, tunaweza—na tunapaswa—kuwa watu wenye shangwe zaidi duniani! Hata kama dhoruba za maisha katika ulimwengu wenye mashaka mara nyingi hutujia, tunaweza kujenga hisia inayokua na ya kudumu ya shangwe na amani ya ndani kwa sababu ya tumaini letu katika Kristo na uelewa wetu wa nafasi yetu wenyewe katika mpango mzuri wa furaha.”

Ninatoa shukrani zangu kwa ajili ya, na ushuhuda wa, injili ya urejesho ya Yesu Kristo, ikijumuisha mpango mkuu wa furaha ulio ndani yake. Ninawaalika mpokee matunda ya injili na kuhisi shangwe zaidi katika maisha haya katika safari yenu kuelekea uzima wa milele.