2025
Kutoroka kutoka Vietinamu
Julai 2025


“Kutoroka kutoka Vietinamu,” Liahona, Julai 2025.

Hadithi kutoka Watakatifu, Juzuu ya 4

Kutoroka kutoka Vietinamu

Wakati Watakatifu wa Vietinamu walipoteseka kupitia vita, uhamisho, kambi na kugawanyika kutoka kwa familia zao, walishikilia kwa nguvu imani yao.

watu wawili wakitazama kifaru kikipita

Kielelezo na David Green

Katika Jumapili angavu ya Aprili 1975 katika nchi iliyoharibiwa na vita ya Vietinamu, Nguyen Van The (inatamkwa “Tay”), rais wa Tawi la Saigon, aliingia katika jumba la mikutano la eneo hilo. Mara moja, washiriki wa tawi walimzunguka, nyuso zao zimejaa kuchanganyikiwa na tumaini. “Rais The! Rais The!” waliita kwa sauti. “Je, una habari gani?”

“Nitawaambia kila kitu ninachojua baada ya mkutano wa sakramenti,” alisema. Aliwahimiza kila mtu katika umati kubaki mtulivu. “Maswali yenu yote yatajibiwa.”

rais wa tawi akipokea mchango wa zaka

Nguyen Van The, rais wa Tawi la Saigon, anapokea mchango wa zaka mwaka 1973—takribani miaka miwili kabla ya vita kuwalazimisha waumini kuondoka Saigon.

Kwa miongo kadhaa, Vietinamu ilikuwa nchi iliyogawanyika. Mgogoro ulizuka muda mfupi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Vikosi vya Marekani vilipigana pamoja na Wavietinamu ya Kusini dhidi ya utawala wa kikomunisti wa Vietinamu ya Kaskazini kwa takriban muongo mmoja, lakini majeruhi na vifo vingi kulisababisha kujiondoa kwa Marekani kutoka vitani. Sasa vikosi vya Kivietinamu Kaskazini vilikuwa vikikaribia mji mkuu wa kusini wa Saigon.

Wakati Rais The alipoingia kanisani na kuketi mbele ya chumba, aliweza kusikia mirindimo ya mizinga mikubwa. Vita ambavyo viliwaleta Watakatifu wengi wa Kivietinamu kwenye injili ya urejesho sasa vilikuwa vikipasua tawi.

Baada ya mkutano, Rais The aliwajulisha Watakatifu kwamba ubalozi wa Marekani ulikuwa tayari kuwahamisha waumini wa Kanisa. Waumini wa tawi walisisitiza kwamba familia ya Rais The ihamishwe mara moja ili aweze kutoa umakini wake wote kwenye kuhamishwa kwa kila mtu mwingine.

Mke wake, Lien, na watoto wao watatu, pamoja na mama na dada zake, waliruka na ndege kutoka Saigon saa chache baadaye.

Siku iliyofuata, Rais The na Mtakatifu mwenzake, Tran Van Nghia, walipanda pikipiki ili kutafuta msaada kutoka Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Lakini punde walikutana na kifaru kilicho na mzinga mkubwa ambacho kilikuwa kinawajia kwa haraka.

Nghia alichepuka nje ya barabara, na yeye na Rais The waliingia katika shimo kujificha. Kifaru kikavuma karibu nao.

Saigon sasa ilikuwa katika mikono ya Wavietinamu wa Kaskazini.

Wiki moja baadaye, mnamo Mei 1975, Le My Lien alishuka kutoka kwenye basi lililokuwa limejaa watu katika kambi ya kijeshi karibu na San Diego, California, katika Pwani ya Magharibi ya Marekani. Mbele yake ulikuwa mji wa mahema uliopangwa kuwahifadhi wakimbizi 18,000 kutoka Vietinamu.

Lien hakuwa na pesa na alizungumza Kiingereza kidogo. Na alikuwa na watoto wake watatu wa kutunza wakati akisubiri habari za mumewe huko Vietinamu.

Usiku wao wa kwanza kambini, Lien alifanya awezavyo kuwafanya watoto wake wawe na raha. Kambi haikumpa mablanketi bali kitanda kimoja tu cha mtoto. Wanawe wa kiume, Vu na Huy, walijikunja kwenye kitanda cha mtoto wakati mtoto mchanga alilala kwenye bembea ambayo Lien iliitengeza kutokana na shuka na mipira.

Hakukuwa na mahali pa Lien kulala chini, hivyo alilala amekaa pembeni mwa kitanda cha mtoto, akiegemea mhimili wa hema. Usiku ulikuwa baridi, na afya yake ikazidi kuwa mbaya. Punde aligundulika kuwa na kifua kikuu.

Alisali daima kwamba mume wake angebakia imara, akiamini kwamba kama yeye angeweza kunusurika na mateso yake, basi naye angeweza kustahimili mateso yake. Hakuwa amesikia chochote kutoka kwake tangu kukimbia kwake kutoka Saigon.

Lien alipombembeleza mtoto wake akilia kila asubuhi, naye alilia pia. “Tafadhali,” alimwomba Bwana, “acha niyapitie hivi leo tu.”

Mnamo 1976, Rais The alifungwa gerezani huko Thành Ông Năm. Alikuwa na hamu kubwa sana ya kupata habari za mkewe na watoto wake, lakini yote aliyoyajua kuhusu familia yake yalikuja kwa njia ya telegram kutoka kwa rais wa Misheni ya Hong Kong: “Lien na familia wako sawa. Pamoja na Kanisa.”

Sasa, zaidi ya mwaka mmoja baadaye, The alishangaa ni lini angekuwa huru tena.

Maisha katika kambi ya gereza yalikuwa ya udhalilishaji. The na mateka wenzake waliwekwa katika kambi zilizojaa panya. Walilala kwenye vitanda vilivyotengenezwa kwa mabamba ya chuma. Chakula haba na kilichoharibika, pamoja na hali mbaya kambini, ilileteleza hatari ya magonjwa ya kuhara damu na ugonjwa wa ukosefu wa Vitamini B mwilini (beriberi).

Uelimishaji upya wa kanuni za serikali mpya ulihusisha kazi ngumu sana na ufundishaji wa kisiasa. Mtu yeyote aliyevunja sheria za kambi anaweza kutarajia kupigwa kikatili au kufungwa kwenye upweke.

The alikuwa amenusurika hadi sasa kwa kutojitokeza sana na kushikilia imani yake. Kwa muda, alitafakari kutoroka kutoka kambini. Lakini alihisi Bwana akimzuia. “Kuwa mvumilivu, Roho alinong’ona. “Yote yatakuwa sawa katika wakati ufaao wa Bwana.”

Wakati fulani baadaye, The alisikia kwamba dada yake, Ba, angeruhusiwa kumtembelea kambini. Kama angeweza kumpenyeza barua kwa siri kwenda kwa familia yake, angeweza kuipeleka kwao.

Siku Ba alipomtembelea, The alisubiri katika mstari wakati walinzi walipokuwa wakifanya ukaguzi wa mwili wote kwa wafungwa mbele yake. Alikuwa ameficha ujumbe nyuma ya kitambaa ndani ya kofia yake. Kisha alikuwa ameweka daftari dogo na kalamu kwenye kofia. Kwa bahati yoyote, daftari lingewavuruga wale walinzi.

Walichunguza kalamu na daftari, kisha wakamruhusu apite.

Punde, The alimwona dada yake na kuikandamiza barua hiyo mikononi mwake. Alilia pale Ba alipompa chakula na pesa. Aliamini kwamba angepeleka barua yake kwa Lien.

Miezi sita baadaye, Ba alirudi kambini akiwa na barua. Ndani ilikuwa picha ya Lien na watoto. Alitambua kwamba asingeweza kusubiri tena.

Ilibidi atafute njia ya kutoka kambini na kuingia mikononi mwa familia yake.

Nguyen Van The akiwa na familia yake

Nguyen Van The na mkewe, Le My Lien, pamoja na mwana wao mnamo 1973. Lien na watoto wao watatu walipata kimbilio nchini Marekani, lakini The alilazimishwa kuhudhuria kambi ya gereza. Baadaye, alisema, “Niliweza kunusurika kambi ya ‘marekebisho kikanuni’ kwa sababu … nilikuwa na imani katika Yesu Kristo.”

Kama sehemu ya misheni yake ya kutunza familia, Huduma za Kijamii za WSM zilikuwa zimepanga na waumini wa Kanisa nchini Marekani kuwatunza wakimbizi wapatao 550 wa Kivietinamu, wengi wao hawakuwa waumini wa Kanisa. Lien na familia yake walidhaminiwa na Philip Flammer, profesa katika Chuo Kikuu cha Brigham Young, na mkewe, Mildred. Waliisaidia familia kuhama kutoka California hadi Provo, Utah.

Mwanzoni, Lien alihangaika kupata kazi. Philip alimpeleka kwenye duka la vifaa vilivyotumika ili kuomba nafasi ya mhudumu wa ofisi. Lakini wakati wa usaili, meneja huyo alichana diploma yake ya shule ya sekondari nusu na kumwambia, “Hii haitumiki hapa.”

Punde alipata kazi ya muda mfupi ya kuchuma cheri kwenye bustani iliyo karibu. Kisha akapata kazi kama mshonaji na kuongeza mapato yake kwa kuoka keki za harusi. Kwa msaada kutoka Philip, pia alipata pesa kwa kuchapa ripoti kwa wanafunzi wa BYU.

Katikati ya shida za familia yake, Lien alibaki mwaminifu kwa Bwana. Aliwafundisha watoto wake kuhusu nguvu ya sala, akijua inaweza kuwabeba kupitia mateso yao.

Kisha, mwishoni mwa mwaka 1977, Lien aligundua kwamba mumewe alikuwa katika kambi ya wakimbizi huko Malaysia. Alikuwa ameweza kuondoka Vietinamu kwenye mashua ya zamani ya uvuvi baada ya kuachiliwa kutoka Thành Ông Năm. Sasa alikuwa tayari kuungana tena na familia yake. Yote aliyohitaji ilikuwa ni mdhamini.

Lien alianza kufanya kazi saa zaidi ili kuweka akiba fedha za kutosha kumleta The Marekani.

Mnamo Januari 1978, Le My Lien alikaa kwa wasiwasi kwenye gari lililokuwa likielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Salt Lake City. Alikuwa njiani kukutana na mumewe kwa mara ya kwanza karibu miaka mitatu.

Baada ya kuwasili uwanja wa ndege, Lien alijiunga na marafiki wengine na waumini wa Kanisa ambao walikuwa wamekuja kumkaribisha The.

Kabla ya muda mrefu, Lien aliona The akishuka kwenye ngazi za umeme. Alionekana mnyenyekevu na alikuwa na mwonekano wa kupotea machoni mwake. Lakini Lien alipomuona, alimwita. Hisia zilichemka katika kifua cha Lien.

Alimvuta The katika kumbatio. “Asante Mungu wa mbinguni,” alinong’ona, “wewe uko nyumbani mwishowe!”

Muhtasari

  1. Nguyen and Hughes, When Faith Endures, 1, 5–7. Nukuu imehaririwa kwa ajili ya usahihi; badala ya “The,” chanzo asili kina tahajia ya kifonetiki ya “Tay.”

  2. Kiernan, Việt Nam, 385–91, 395–451; Taylor, History of the Vietnamese, 446–47, 478–83, 536–619.

  3. Nguyen and Hughes, When Faith Endures, 1, 6–18, 119, 127–33, 136–37; Britsch, From the East, 435–37; “Saigon Branch Evacuation List,” May 13, 1975, First Presidency, General Correspondence, CHL; Le, Oral History Interview, 1–3; Nguyen, “Escape from Vietnam,” 29.

  4. Le, Oral History Interview, 2–5, 9–10, 16–19, 21, 23, 27; Nguyen and Hughes, When Faith Endures, 236.

  5. Nguyen and Hughes, When Faith Endures, 158–60, 163, 184, 190. Nukuu imehaririwa kwa ajili ya usomaji; chanzo asili kina “LIEN AND FAMILY FINE WITH CHURCH.”

  6. Nguyen and Hughes, When Faith Endures, 160–62, 165–73, 174–79, 189; Vo, Bamboo Gulag, 62–63, 72, 77, 117–26, 143–46, 151–56. Nukuu imehaririwa kwa ajili ya usomaji; “ingekuwa” katika asili imebadilishwa kuwa “itakuwa.”

  7. Nguyen and Hughes, When Faith Endures, 190–94.

  8. Nguyen Van The, katika Water Tower Chronicles (blog), watertowerchronicles.weebly.com/the-van-nguyens-story.

  9. Le, Oral History Interview, 29, 45–63; Nguyen and Hughes, When Faith Endures, 195–98, 203–13, 220.