“Je, Tungemwona Mjukuu Wetu wa Kike Tena?” Liahona, Julai 2025.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Je, Tungemwona Mjukuu Wetu wa Kike Tena?
Uamuzi wetu wa kukubali mwaliko kutoka kwa Rais Nelson ulisababisha muujiza usiotarajiwa.
Kielelezo na David Malan/Malan Creative
Mnamo 1999 mwana wetu mkubwa alifariki. Alimwacha mke na binti wa mwaka mmoja nyumbani ambaye pamoja naye tulikuwa na uhusiano wenye kuburudisha na muingiliano wa ajabu, wa kila wiki.
Kwa sababu ya hali mbaya, kumbukizi ya siku ya tatu ya kuzaliwa kwa mjukuu wetu ilikuwa ni mara ya mwisho kuwa na mawasiliano yo yote naye. Kwa miaka mingi, tulisali, tulifunga, na tulitumaini kwa namna fulani tungeweza kumwona tena.
Wakati wa mkutano mkuu wa Oktoba 2018, Rais Russell M. Nelson alitoa mwaliko wenye ahadi: “Ninawasihi mtafute njia ya kufanya miadi ya kila mara na Bwana—kuwa katika nyumba Yake takatifu—kisha tunza miadi hiyo kwa usahihi na shangwe. Ninawaahidi kwamba Bwana ataleta miujiza anayojua mnahitaji mnapofanya dhabihu ya kutumikia na kuabudu katika mahekalu Yake.”
Niliposikia maneno haya, nilihisi kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa akizungumza nami kupitia nabii Wake. Kwa hiyo, mimi na mume wangu tulijitolea kuanza kuhudhuria hekaluni kila Jumanne na kuweka sharti hilo “kwa ukamilifu na shangwe.”
Siku moja mwaka 2019, mjukuu wetu wa kike wa miaka 21 alinitumia ujumbe mtandaoni bila kutarajia. Mawasiliano yake yalikuja taratibu mwanzoni, lakini ujumbe wake ulipoendelea, alianza kuuliza maswali ambayo yalifungua mtiririko wa ajabu wa mazungumzo. Alituruhusu sisi kuwa katika maisha yake kwa dhati mwanzoni na kisha mara kwa mara.
Mnamo mwaka 2021 tulimwalika kutumia muda wa Kutoa Shukrani na familia yetu. Alikubali, na tulikuwa na wakati mzuri sana wa kumjua. Kwa urahisi aliunganika na mashangazi, wajomba, binamu, na wapwa zake. Alitaka ziara yake ya Kutoa Shukrani kuwa desturi.
Mwaka mmoja baadaye, mwana aliyejitenga aliunganika nasi. Mnamo Machi 2024, kwa mara ya kwanza katika maisha ya familia yetu, tulikuwa na muungano wa familia ambao ulijumuisha kila mtoto aliye hai, wake zao, na wajukuu wote 16.
Daima nimeamini kwamba nabii huzungumza kwa niaba ya Bwana. Ninaamini kwamba muujiza huu uliohitajika sana ulikuja kwa sababu ya mwongozo na ahadi iliyofunuliwa ya Rais Nelson.
Ushuhuda na upendo wangu kwa Baba yangu wa Mbinguni na Mwanawe havikuwa, na siyo, sababu ya muujiza huu. Ninashangazwa, hata hivyo, jinsi upendo Wao binafsi ulivyo kwangu na jinsi gani ahadi Zao zinavyokuwa na nguvu ambazo huja kupitia nabii.