Nabii na Mwokozi Wake
Katika njia fulani, masimulizi ya maisha ya Joseph Smith ni masimulizi ya yeye kusonga karibu na Yesu Kristo.
Kila Goti Litapigwa, na Dan Wilson
Masimulizi ya maisha ya Joseph Smith ni zaidi ya masimulizi tu ya maisha ya Joseph Smith.
Tunaposimulia kuhusu Urejesho wa injili ya Yesu Kristo, mara nyingi tunaanza kwa kusimulia juu ya Joseph Smith. Na hilo ni kawaida. Yeye mwenyewe alitoa masimulizi ya maisha yake ya mwanzoni mara kadhaa ili kuwasaidia watu kuelewa jinsi Urejesho ulivyoanza. Lakini katika njia fulani, masimulizi ya maisha ya Joseph Smith ni masimulizi ya yeye kusonga karibu na Yesu Kristo.
Ono la Msamaha
Kijana Joseph Smith alihisi kukanganywa kuhusu dini. Na kulikuwa na hisia za ziada ambazo zilimfanya kusali katika kijisitu hicho cha miti ambapo alipata Ono lake la Kwanza: “Nilihisi kuomboleza kwa ajili ya dhambi zangu mwenyewe.”
Mwokozi alipozungumza na Joseph, Alisema, “Joseph, mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”
Joseph alijifunza moja kwa moja kwamba Yesu Kristo yu hai. Pia alijifunza kwamba Yesu Kristo ni mwenye rehema na anasamehe dhambi. Ufahamu huu binafsi ulikuwa muhimu kwa Joseph. “Wokovu wa nafsi yangu ni wa umuhimu sana kwangu [kwa sababu] ninajua uhakika wa mambo ya milele,” aliwahi kusema.
Ufahamu huu kuhusu Yesu Kristo pia ulikuwa muhimu katika kazi ambayo Joseph aliitwa kufanya kama nabii. Alishuhudia kwa nguvu juu ya neema na rehema ya Yesu Kristo katika maisha yake yote. Kwa mfano, wakati mmoja alifundisha, “Mioyo yote lazima itatubu na kuwa safi, na Mungu atawaheshimu na kuwabariki kwa njia ambayo hawangeweza kubarikiwa kwa njia nyingine yoyote.”
Makosa na Rehema
Kazi ambayo Joseph Smith iliitwa kuifanya ilikuwa muhimu sana. Na Joseph alijifunza kuchukulia amri za Bwana na mashauri kwa umakini, kwa sehemu kupitia makosa aliyofanya.
Kwa mfano, wakati kurasa za muswada za Kitabu cha Mormoni zilipopotea, Bwana alichukua kipawa cha kutafsiri kutoka kwa Joseph na baadaye akamwambia: “Mara ngapi umevunja amri na sheria za Mungu. … Hupaswi kumwogopa mwanadamu zaidi kuliko Mungu” (Mafundisho na Maagano 3:6–7).
Lakini Bwana pia alikuwa na ujumbe huu kwa Joseph: “Kumbuka, Mungu ni mwenye huruma; kwa hiyo, tubu” (Mafundisho na Maagano 3:10).
Joseph alitubu na alipewa tena kipawa cha tafsiri. Uzoefu wote unaweza kuwa ulikuwa mchungu kwake, lakini alijifunza masomo muhimu—ikijumuisha kwamba tunaweza kutubu na kubarikiwa kwa sababu Bwana ni mwenye rehema.
Mwokozi na Rafiki
Joseph Smith alikuwa na maono kadhaa, matembezi, na mafunuo ambayo kupitia hayo alimwona au kumsikia Bwana Yesu Kristo au kujifunza kuhusu asili Yake, tabia, na misheni Yake (ona, kwa mfano, Mafundisho na Maagano 19; 76; 93; 110).
Ukweli mmoja aliojifunza ni kwamba kazi ya ukombozi ya Mwokozi ni kwa watu wote ambao waliwahi kuishi katika ulimwengu huu—na ulimwengu wote ambapo wana na mabinti wa Mungu wanaishi ( ona Mafundisho na Maagano 76:24).
Wakati huo huo alikuwa akijifunza jinsi kazi ya Mwokozi ilivyo kubwa, Joseph alikuwa pia akijifunza kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanamjua na kumpenda kila mmoja wetu binafsi. Wanataka uhusiano wa karibu na kila mmoja wetu. Wanatutaka tufanye maagano, kuyashika, na kuvumilia kwa uaminifu hadi mwisho. Uhusiano huu wa kina utatuletea furaha na kujiamini.
Uhusiano wa Joseph mwenyewe na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo ulikuwa wa kina sana kwamba katika mojawapo ya mambo ya chini kabisa katika maisha yake, wakati akiwa amefungiwa katika Jela ya Liberty, aliweza kusema:
“Nitajaribu kuridhika na kilichopangwa kwangu, nikijua kwamba Mungu ni rafiki yangu. Katika yeye nitapata faraja. Nimeyatoa maisha yangu mikononi mwake. Nimejitayarisha kwenda kwenye wito wake. Natamani kuwa pamoja na Kristo.”
Unapojifunza maisha na mafundisho ya Joseph Smith, unaweza kufuata mfano wake. Tubu, fanya na shika maagano, na endelea kuwa mwaminifu. Kisha wewe pia unaweza kujua kwamba Mwokozi ni Rafiki yako.