2025
Mtazame Kristo
Januari 2024


Dhima ya Vijana kwa Mwaka 2025

Mtazame Kristo

Mafundisho na Maagano 6:36

Dhima ya Vijana kwa mwaka 2025 itakusaidia kuchagua kutumaini badala ya kutilia shaka na imani badala ya hofu.

Nembo ya Dhima ya Vijana 2025

Kailey mwenye umri wa miaka kumi na saba alikuwa kiongozi wa timu ya ushangiliaji hadi ajali iliposababisha jeraha la ubongo. Mchakato wa uponaji wake ulimzuia kuhudhuria shule, na alianza kujihisi ametengwa na mpweke. Alihangaika kihisia na hakujua wapi pa kutafuta msaada. Rafiki alipendekeza kwamba awasikilize wamisionari. Wao walimfundisha kuhusu Upatanisho wa Yesu Kristo. Kujifunza zaidi kuhusu Kristo kulimpa tumaini, na alihisi kana kwamba Mungu Mwenyewe alikuwa anamfikia.

Kailey alimwambia mama yake, “Sijawahi kuhisi kwamba Mungu ananipenda. Lakini sasa najua ananipenda.”

Michelle, mama yake, alishangazwa kidogo. Yeye na mumewe, Brock, walikuwa wameliacha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wakati Kailey alipokuwa na miaka saba kwa sababu ya maswali mbalimbali, mashaka, na wasiwasi. Walidhani binti yao angekuwa na furaha zaidi bila mikutano yote na amri. Kamwe hawakufikiria uchaguzi wao ungemzuia Kailey kutoka kwenye muunganiko wa karibu na Mungu. Wakati Michelle na Brock walipotazama jinsi Kailey alivyobadilika, waligundua kwamba ilikuwa ni muda mrefu tangu walipohisi kuwa karibu na Mungu, na walitaka kuhisi hivyo tena.

Walikutana na askofu wao, na punde familia, ikiwa ni pamoja na Braeden, kaka yake Kailey walirudi tena kanisani. Kuhisi kuwa karibu na Mungu na kuungana naye tena—hasa kupitia sala—kulirejesha imani yao. Kurudi kanisani hakukutatua maswali yao yote au wasiwasi, lakini waligundua kwamba kuwa na muunganiko imara binafsi na Mungu ilikuwa muhimu zaidi kuliko kutoamini kwao.

Haya yote yalianza wakati rafiki—kijana kama wewe—alipomwalika Kailey kumtegemea Kristo. Na yeye alifanya hivyo!

Yesu Kristo amesema, ‘Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope’ (Mafundisho na Maagano 6:36). Huu ndio mwongozo wa kiungu ulio nyuma ya Dhima ya Vijana kwa mwaka 2025. Turuhusu tushiriki jinsi unavyoweza kuchagua kutumaini badala ya kutilia shaka na imani badala ya hofu unapomtegemea Kristo:

Urais Mkuu wa Wasichana

Kushoto kwenda kulia: Dada Runia, Rais Freeman, Dada Spannaus

Tamara W. Runia

Ninapopata changamoto, daima inanisaidia kufikiria Yesu Kristo akiwa amenyoosha mikono Yake. Ninapomtazama Yeye, nakumbuka maneno ya wimbo, “Nitatembea pamoja na Yesu”: “Hataniacha, hata wakati ninapoanguka.”

Emily Belle Freeman

Ninaposoma andiko hili la dhima, ninakumbushwa juu ya Petro kwenye Bahari ya Galilaya. Kufokasi kwenye dhoruba kuliongeza hofu na shaka yake, na kusababisha yeye kuzama kwenye mawimbi yenye dhoruba. Lakini kufokasi kwa Mwokozi kulimwezesha kutimiza kitu ambacho hakuwahi kukipata kabla: alitembea juu ya maji! Ni ya ajabu, kwa kweli. Unaweza kutimiza nini unapomtegemea Yeye?

Andrea Muñoz Spannaus

Ninapoanza kuhisi woga, bila kujali niko wapi au hali niliyonayo, kwa kukusudia nafikiria uhusiano wangu na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Ninarudia akilini mwangu mara kadhaa: MIMI NI BINTI WA MUNGU. Ninaendelea kufanya hivi mpaka ninapoanza kujisikia vizuri zaidi. Daima ninafanikiwa.

Urais Mkuu wa Wavulana

Kushoto kwenda kulia: Kaka Wilcox, Rais Lund, Kaka Nelson

Bradley R. Wilcox

Jiulize mwenyewe ni nani anayekujali na kukupenda zaidi. Je, ni wazazi wako na viongozi wako wa Kanisa? Je, ni watu kwenye mitandao ya kijamii ambapo wewe ni sehemu tu ya idadi? Mtegemee Baba wa Mbinguni na Kristo. Hakika wanajali!

Steven J. Lund

Kumbuka kile unachokumbushwa unapokariri dhima ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni na ya Wasichana: Wewe ni mwana au binti mpendwa wa Mungu. Kuwa na imani kwamba Baba yetu ana mpango kwa ajili yako. Kumtegemea Kristo humaanisha kuona kwamba Upatanisho Wake uko katikati ya mpango huo.

Michael T. Nelson

Kusoma maandiko ni kumtegemea Kristo! Mashaka na hofu kwa kawaida hufifia wakati tunapokumbushwa miujiza na mafundisho ya Yesu. Tuna bahati sana ya kuweza kuyafikia maneno Yake. Yanatumika katika kila hali tunayopitia katika maisha yetu.

Muhtasari

  1. Maneno na muziki na Stephen P. Schank (ona Rafiki, Feb. 2020, 27; ona pia Nyimbo za Dini- Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani, na. 1004).