Habari Njema kwa ajili Yako na kwa Ulimwengu
Unaweza kupokea habari njema za upendo na shangwe kwa sababu Yesu Kristo amerejesha Kanisa Lake ili kuwabariki watoto wote wa Mungu.
Kijisitu Kitakatifu, na Al Rounds
Ujumbe wetu wa tumaini na amani kwa wote ni kwamba Yesu Kristo yu hai na amerejesha injili Yake na Kanisa Lake katika siku hizi za mwisho. “Ni ya kushangaza jinsi gani mambo haya matakatifu kwa wanadamu!” Nabii Joseph Smith alitamka. Ni “habari njema ya shangwe kuu kwa watu wote… ambayo inapaswa kuijaza dunia na kuifurahisha mioyo ya kila mmoja inaposikika masikioni mwake.”
Habari hizi njema ni dhihirisho kubwa la upendo usio na mwisho wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu. Zitawabariki watu wote na kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya siku Yesu Kristo atakaporudi. Ninafurahia kwamba ninaweza kutumia maisha yangu nikitangaza kweli hizi kwa ulimwengu wote.
Asubuhi ya Ufufuko, na Sarah Hatch
Visivyowezekana na vya Kustaajabisha
Katika kijisitu cha miti, Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, walimtokea na kuzungumza na Joseph Smith kwenye kujibu sala ya Joseph kuhusu ni kanisa gani anapaswa kujiunga nalo (ona Joseph Smith—Historia 1:16–20). Yesu alimwambia Joseph asijiunge na kanisa lolote. Aliahidi kwamba utimilifu wa injili Yake ungefunuliwa kwa Joseph katika siku zijazo.
Kwa wengi, Joseph alionekana kutowezekana kabisa kuitwa kwenye kazi muhimu kama hiyo. Machoni mwao, alikuwa tu mvulana asiye na elimu kutoka katika shamba dogo. Lakini kupitia Joseph, Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kweli wangefanya ya kustaajabisha kabisa. Joseph angepewa amri, mafunuo ya thamani, na mafundisho muhimu kuhusu mpango wa upendo wa Baba wa Mbinguni na upendo wenye kukomboa na Upatanisho wa Yesu Kristo ili kutubariki na kutusaidia kujua jinsi tunavyoweza kurudi nyumbani.
Ushuhuda Wenye Nguvu wa Upendo wa Mungu
Malaika Moroni alimtokea Joseph Smith na kumwambia Joseph juu ya kumbukumbu, iliyoandikwa juu ya mabamba ya dhahabu, yaliyozikwa karibu na hapo (ona Joseph Smith—Historia 1:33–34). Hatimaye, Joseph alitafsiri kumbukumbu hiyo katika kile ambacho kingekuwa Kitabu cha Mormoni, ambacho kinasimama sambamba na Biblia kama shahidi mwingine wa Yesu Kristo.
Kote katika Kitabu cha Mormoni, watu, mamia ya miaka kabla ya Kristo, walijua na kutabiri juu ya ujio Wake na kutamani ujio Wake. Pia tunasoma jinsi Mwokozi alivyowatokea na kuwahudumia Wanefi. Aliwaalika wote kuja Kwake. Aliwaponya wagonjwa, viwete, vipofu, na wote walioteseka. Kisha aliwabariki watoto wadogo na kusali kwa ajili yao (ona 3 Nefi 11:14–15; 3 Nefi 17:7–9; 3 Nefi 17:21).
Kitabu cha Mormoni kinatufundisha mengi kuhusu upendo na huruma ya Mwokozi. Kwa kweli kinashuhudia kwamba “Yesu ndiye Kristo.” Kina uzuri wa injili Yake isiyo na mwisho. Kitabu cha Mormoni kinatoa picha iliyo wazi ya jinsi gani Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu wanavyotupenda zaidi ya chochote tunachoweza kufikiria.
Mabamba ya Dhahabu, na Robert Theodore Barrett
Baraka za Ukuhani na Kanisa
Wajumbe wengine wa mbinguni walikuja kwa Joseph Smith. Yohana Mbatizaji alikuja kurejesha mamlaka ya kubatiza. Petro, Yakobo, na Yohana walirejesha utume na funguo za mamlaka ya ukuhani. Wengine pia walikuja, ikiwa ni pamoja na Eliya, aliyerejesha mamlaka ya kuunganisha familia pamoja milele katika uhusiano usio na mwisho ambao unavuka mipaka ya kifo.
Yesu Kristo kisha alianzisha Kanisa kupitia Nabii Joseph katika mpangilio kama lile alilolianzisha katika nyakati za Agano Jipya (ona Makala ya Imani 1:6). Kupitia Yesu Kristo na mitume na manabii Wake, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho hufanya baraka za nguvu za ukuhani uliorejeshwa zipatikane kwa watoto wote wa Mungu.
Ningesema kwamba kama unajisikia kuwa umelemewa na unajisikia kwamba hautoshi au kwamba haustahili kuwa sehemu ya, uwe mkarimu zaidi kwako wewe mwenyewe na utambue jinsi unavyopendwa na Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Mwokozi wetu, zaidi ya unavyoweza kufikiria. Wote wanaalikwa kuja kwa Kristo na Kanisa Lake. Kanisa siyo kwa ajili ya wakamilifu. Ni kama hospitali ambapo tunatafuta uponyaji. Kanisani tunageuka, kuwahudumia wengine kwa upendo, na kushiriki injili. Tunaweza “kukumbukwa na kulishwa na neno zuri la Mungu” (Moroni 6:4). Tunaweza kupata amani na uponyaji. Ni baraka kuu iliyoje!
Sababu ya Shangwe Kuu
Baba wa Mbinguni na Mwanawe mpendwa, Yesu Kristo, wanakupenda na wanatamani—zaidi ya chochote—kukuleta wewe nyumbani na milele kuwa na aina ya maisha wanayoyaishi. Urejesho unaonyesha kwamba Wamefanya kila kitu ili kufanya hili kuwa uwezekano mtukufu kwako. Nyakati zingine, unaweza kupata uzoefu wa majaribu na magumu, lakini wewe upo “ili kwamba [wewe] uwe na shangwe” (2 Nefi 2:25) katika maisha haya na yajayo. Nabii Joseph alijua hili vizuri zaidi ya mengi. Utagundua kwamba unaweza kuwa na shangwe unapotubu kila mara na kumgeukia Baba yako wa Mbinguni na Mwokozi wako.
Joseph alikabiliwa na upinzani na mateso ya mara kwa mara, lakini bado “aliendeleza tabia yake ya asili ya furaha” (Joseph Smith—Historia 1:28). Alibakia mwenye furaha, imara, na thabiti, na alikamilisha kazi aliyopewa kufanya. Vivyo hivyo ni kweli kwa wote waliomrithi.
Ilikuwa vigumu katika siku za mwanzo za Kanisa, na inaweza kuwa vigumu leo, lakini Urejesho uliendelea wakati huo—na unaendelea leo. Yesu Kristo analiongoza Kanisa Lake. Manabii walio hai wanaendelea kutuongoza. Nyumba za Bwana zitaendelea kujengwa. Upendo wa Mungu na Yesu Kristo utaenea ulimwenguni kote tunapofuata amri ya Mwokozi ya kuwalisha kondoo Wake na kushiriki injili Yake. Kweli za Urejesho zitasonga mbele katika njia na kwenye sehemu ambazo hazingefikirika katika siku ya Joseph. Tutajitahidi kuufanya ulimwengu kuwa wenye ongezeko la ukarimu na usio na mgawanyiko.
Unapojifunza injili mara kwa mara, kusali kila mara, na kuwahudumia wengine, ujumbe wa Urejesho utagusa moyo wako na kubadilisha maisha yako. Inaweza isitokee kwa ghafla, lakini itakuletea shangwe—kama ilivyofanya kwa Nabii Joseph.
Na habari njema ya upendo na shangwe ambayo Urejesho huleta vibariki na kuongoza maisha yako—sasa na daima.