“Novemba 16–22. ‘Nitawapenda kwa Ukunjufu wa Moyo’: Hosea 1–6; 10–14; Yoeli,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Agano la Kale 2026 (2026)
“Novemba 16–22. “Nitawapenda kwa Ukunjufu wa Moyo,’” Njoo, Unifuate: Agano la Kale 2026
Novemba 16–22: “Nitawapenda kwa Ukunjufu wa Moyo”
Hosea 1–6; 10–14; Yoeli
Agano la Israeli na Bwana lilikusudiwa kuwa la kina na lenye maana kiasi kwamba Bwana alililinganisha na ndoa. Agano, kama ndoa, lilijumuisha kujitolea kwa milele, uzoefu wa pamoja, kujenga maisha pamoja, uaminifu wa kipekee, na zaidi ya yote, upendo wa moyo wote. Kwa huzuni, Waisraeli hawakuwa waaminifu katika agano lao. Na bado ujumbe wa Bwana kwao haukuwa “Nitakukataa milele.” Badala yake ulikuwa “nitakualika urudi” (ona Hosea 2:14–15). “Nitakuposa uwe wangu katika haki,” Yeye alitangaza kupitia nabii Hosea (Hosea 2:19). “Nitaponya kurudi nyuma kwao, nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo” (Hosea 14:4). Huu ni ujumbe ule ule Yeye anaotupatia leo tunapotafuta kuishi maagano yetu kwa upendo na kwa kujitolea kwa dhati.
Yoeli alishiriki ujumbe kama huo: “Mgeukie Bwana Mungu wako: kwa kuwa yeye ndiye mwenye neema na rehema, si mwepesi wa hasira, na mwingi wa fadhili” (Yoeli 2:13). Kusoma maneno ya manabii hawa kunaweza kukupa msukumo kutafakari uhusiano wako na Bwana—kufikiria kuhusu jinsi uaminifu Wake kwako unavyokuvutia kuwa mwaminifu Kwake.
Kwa ajili ya muhtasari wa vitabu vya Hosea na Yoeli, ona “Hosea au Hoshea” na “Yoeli” katika Kamusi ya Biblia.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Hosea 1–3; 14
Bwana daima hunialika kurudi Kwake.
Mke wa Hosea, Gomeri, hakuwa mwaminifu kwake, na Mungu alionyesha tukio hili la kusikitisha ili kuwafundisha Waisraeli jinsi alivyojisikia kuhusu wao na maagano yao na Yeye. Unaposoma Hosea 1–3, tafakari jinsi Bwana anavyoona uhusiano Wake na watu Wake wa agano. Ni kwa jinsi gani kufanya agano na Bwana ni kama kuingia katika ndoa? Ni kwa jinsi gani kushindwa kushika agano hilo ni kama kutokuwa mwaminifu kwa mwenzi? (ona Hosea 2:5–7, 13). Ni nini Hosea 2:14–23 inatufundisha sisi kuhusu upendo na rehema za Bwana? Je, ni kwa jinsi gani wewe unamwonyesha Yeye upendo na uaminifu wako?
Katika Hosea 14, tafuta ahadi nyingi nzuri ambazo Bwana hufanya kwa wale wanaorudi Kwake. Kishazi “nitawapenda kwa moyo mkunjufu” kinamaanisha nini kwako? (mstari wa 4). Je, sitiari ya mmea katika mstari wa 5–8 inatufundisha nini kuhusu baraka za Bwana, ikijumuisha baraka ya toba? Kama sehemu ya kujifunza kwako, fikiria kuimba au kusikiliza wimbo kuhusu rehema ya Mwokozi, kama vile “Njoo kwa Yesu” (Nyimbo za Dini, na. 59).
Gomeri, ambaye anawakilisha nyumba ya Israeli na maagano yao yaliyovunjika, alipewa ukombozi na Bwana. Kielelezo na Deb Minnard, kilichopewa leseni kutoka goodsalt.com
Hosea 6:4–7; Yoeli 2:12–13
Kujitolea kwa Mungu lazima kuhisiwe kwa ndani, sio kuonyeshwa kwa nje tu.
Watu katika siku za Hosea walikuwa wakitoa dhabihu za wanyama, lakini walikuwa wakivunja amri muhimu zaidi. Unafikiria inamaanisha nini kwamba Bwana “alitaka rehema, na sio dhabihu; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa”? (Hosea 6:6). Unafikiria inamaanisha nini kwa haki kuwa kama wingu au kama umande? (ona Hosea 6:4). Je, haki yetu inapaswa kuwa kama nini? (ona Isaya 48:18; 1 Nefi 2:9–10).
Ungeweza pia kusoma Mathayo 9:10–13; 12:1–8 ili kuona jinsi Mwokozi alivyotumia Hosea 6:6 wakati wa huduma Yake. Je, vifungu hivi vinakusaidiaje kuelewa maneno ya Hosea?
Wakati unaposoma Yoeli 2:12–13, ingeweza kusaidia kujua kwamba mtu kurarua au kuchana nguo zake ilikuwa ishara ya nje ya kuomboleza au kujuta. Je! Ni kwa jinsi gani kurarua mioyo yetu ni tofauti na kurarua mavazi yetu?
Yoeli 2
“Nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili”
Ni mifanano gani unayoiona kati ya siku yetu na siku ambayo Yoeli aliiona? (ona hasa Yoeli 2:1–2, 11, 18–32). Je, ni kitu gani kinakuvutia kuhusu baraka alizoahidi Bwana katika Yoeli 2:12–32? Kwa nini baraka hizi zingeweza kuwa zenye thamani hususani leo?
Ingeweza kuwa ya kuvutia kusoma kile Moroni alichosema kuhusu Yoeli 2 wakati alipomtembelea Joseph Smith mwaka 1823 (ona Joseph Smith—Historia 1:41). Je, unahisi unabii katika Yoeli 2:28–32 unatimizwa vipi katika siku yetu? (ona pia Matendo ya Mitume 2:1–21). Unafikiri inamaanisha nini kwamba Bwana “atamimina roho [Yake] juu ya wote wenye mwili.”? (Yoeli 2:28).
Ungeweza kutafakari maneno haya kutoka kwa Rais Russell M. Nelson: “Katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila mwongozo, maelekezo, faraja na ushawishi endelevu wa Roho Mtakatifu.” (“Ufunuo kwa Kanisa, Ufunuo kwa Ajili ya Maisha Yetu,” Liahona,” Mei 2018, 96). Kwa nini ufunuo ni muhimu kwa kunusurika kwako kiroho?
Ni nini tunaweza kufanya kama tunahisi hatupokei ongezeko la mmiminiko kama huo? Hapa kuna baadhi ya mifano ambayo inaweza kusaidia. Watu katika maandiko haya walifanya nini ili kupokea mmiminiko wa Roho wa Bwana?
Unaposoma maneno haya kutoka kwa Mzee David A. Bednar, tafakari inamaanisha nini kwako kuhisi mmiminiko wa Roho Mtakatifu katika maisha yako ya kila siku:
“Mara nyingi tunafanya iwe vigumu kupokea ufunuo binafsi. Kwa kusema hilo ninamaanisha, ahadi ya agano ni kwamba tunapoheshimu maagano yetu, tunaweza daima kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi wetu wa kudumu. Lakini tunaongea juu yake na tunachukulia kama kusikia sauti ya Bwana kupitia Roho Wake ni tukio la nadra. … [Roho] anapaswa kuwa pamoja nasi nyakati zote. Sio kila sekunde, lakini kama mtu anajitahidi vizuri awezavyo—hauhitaji kuwa mkamilifu—lakini kama wewe na mimi tunajitahidi tuwezavyo na hatutendi dhambi nzito, basi tunaweza kutegemea Roho Mtakatifu anatuongoza. …
“… Tunaonekana kuamini kwamba Roho Mtakatifu ni mkubwa na mkubwa na wa ghafla, wakati bado ni tulivu na mdogo na kuongezeka baada ya muda” (“Mzee David A. Bednar Discussion” [evening with a General Authority, Feb. 7, 2020], broadcasts.ChurchofJesusChrist.org).
Ona pia Gary E. Stevenson, “Ushawishi wa Roho,” Liahona, Nov. 2023, 42–45; “Enemy Territory” (video), Gospel Library.
Enemy Territory
Tengeneza mazingira ya kiroho. “Umeona nini ambacho kinachangia katika mazingira ya kiroho ya kujifunza injili? Ni nini kinayapunguza? … Fikiria kuhusu mazingira ambayo kwayo mara nyingi unafundisha [au kujifunza]. Unajisikiaje unapokuwa hapo? Ni kwa jinsi gani unaweza kwa tija zaidi kumwalika Roho awepo hapo? (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 7).
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Hosea 2:19–20
Ninaweza kushika maagano yangu kwa uaminifu.
-
Katika kitabu cha Hosea, Bwana alilinganisha maagano Yake na watu Wake na ndoa. Ili kujifunza kutokana na ulinganisho huu, wewe na watoto wako mngeweza kutazama picha ya bibi harusi na bwana harusi na kuzungumza kuhusu jinsi Baba wa Mbinguni anavyotaka mume na mke kutendeana. Wasaidie watoto wako watafute maneno katika Hosea 2:19–20 ambayo yanaelezea jinsi Bwana anavyojisikia kuhusu sisi. Ni jinsi gani tunaweza kumwonesha Bwana kwamba tunampenda na tutakuwa waaminifu Kwake?
Hosea 10:12
“Ni wakati wa kumtafuta Bwana.”
-
Hosea 10:12 hurejelea kupanda mbegu, kuvuna, majira na mvua ili kutualika sisi kumtafuta Bwana. Unaposoma mstari huu, ni mawazo gani ya ubunifu huja akilini ambayo yanaweza kuwapa ushawishi watoto wamtafute Yeye? Kwa mfano, pengine watoto wako wangeweza kuchora saa na kuandika njia wanazoweza kumtafuta Bwana kwa nyakati tofauti siku nzima. Wimbo kama “Anytime, Anywhere” (Gospel Library) ungeweza kukusaidia kufundisha kwamba daima ni wakati mzuri wa kumtafuta Bwana.
-
Au watoto wako wangeweza kufanya vitendo rahisi vinavyoendana na mstari, kama vile kujifanya kupanda mbegu, kuchuma mboga, au kusimama katika mvua. Wasaidie watoto wako walinganishe kupanda mbegu na kuvuna chakula kizuri na kuishi kwa uadilifu na kupokea baraka za Bwana. Kisha mngeweza kusimiliana kuhusu baraka ambazo Bwana amezimimina juu yako wakati ulipojaribu kumtafuta Yeye.
Hosea 13:4, 14
Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wangu.
-
Ili kusisitiza ukweli katika Hosea 13:4 kwamba hakuna Mwokozi isipokuwa Yesu Kristo, ungeweza kuwaonyesha watoto wako picha za watu kadhaa, ikijumuisha Yesu. Watoto wako wangeweza kuchukua zamu kumwonyesha mtu ambaye ana uwezo wa kutuokoa kutokana na dhambi na kifo. Shiriki ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo na Upatanisho Wake.
-
Watoto wako wangeweza kutafuta maneno katika Hosea 13:4, 14 ambayo yanamwelezea Yesu Kristo. Je, maneno haya yanatufundisha nini kumhusu Yeye? Fikiria kuwasaidia watoto wako kutumia Mwongozo wa Maandiko kutafuta maandiko mengine ambayo yanafundisha kwamba Yesu ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Shirikianeni jinsi mnavyojisikia kuhusu Yesu Kristo.
Yoeli 2:28–29
Roho Mtakatifu anaweza kuniongoza.
-
Pengine ungeweza kuwasaidia watoto wako waelewe Yoeli 2:28–29 kwa kuwaacha wamimine kimiminiko na kisha kukitofautisha na tone au mchuruzo. Inaweza kumaanisha nini kwa Roho “kumiminwa” juu yetu?
-
Mnaposoma Yoeli 2:28–29 pamoja, mnaweza kuwaalika watoto wako waweke majina ya kila mmoja badala ya virai “wana wenu” na “mabinti zenu.” Kisha wasaidie kupekua maandiko kama Yohana 14:16; Moroni 10:5; Mafundisho na Maagano 42:17 ili kujua jinsi Roho anavyoweza kuwasaidia.
Kwa ziada, ona toleo la mwezi huu la jarida la Rafiki .