“Novemba 9–15. “Hakuna Mungu Mwingine Awezaye Kuokoa,”: Danieli 1–7,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Agano la Kale 2026 (2026)
“Novemba 9–15. ‘Hakuna Mungu Mwingine Awezaye Kuokoa’” Njoo, Unifuate: Agano la Kale 2026
Danieli Anatafsiri Ndoto ya Nebukadreza, na Grant Romney Clawson
Novemba 9–15: “Hakuna Mungu Mwingine Awezaye Kuokoa”
Danieli 1–7
Kuna uwezekano mkubwa hakuna mtu atakayetishia kukutupa kwenye tanuru la moto au tundu la simba kwa sababu ya imani yako katika Yesu Kristo. Lakini hakuna hata mmoja wetu anayepitia maisha haya bila jaribio la imani. Sote tunaweza kufaidika na mfano wa watu kama Danieli, Shadraka, Meshaki na Abednego, ambao walichukuliwa mateka wakiwa vijana na Dola kuu ya Babeli (ona 2 Wafalme 24:10–16). Vijana hawa walikuwa wamezungukwa na tamaduni isiyojulikana na maadili tofauti, na walikabiliwa na vishawishi vikubwa vya kuacha imani yao na mila za haki. Walakini walibaki wakweli kwenye maagano yao. Ni kwa jinsi gani walifanya hilo? Kwa kufanya vitu vidogo na rahisi Mungu ametuomba sisi sote—kuomba, kufunga, kuchagua marafiki wazuri, kumwamini Yeye na kuwa nuru kwa wengine. Kama Yusufu huko Misri na Esta huko Uajemi, Danieli na marafiki zake huko Babeli waliweka imani yao kwa Mungu, na Mungu alifanya miujiza ambayo bado inawavutia waumini hadi leo.
Kwa ajili ya muhtasari wa kitabu cha Danieli, ona “Danieli” katika Kamusi ya Biblia.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Danieli 1; 3; 6
Ninaweza kumwamini Bwana wakati imani yangu inapojaribiwa.
Kwa namna fulani, sisi sote tunaishi Babeli. Mara nyingi tunakabiliwa na majaribu ya kulegeza viwango vyetu na kugeuka mbali na imani katika Kristo. Unaposoma Danieli 1, 3, na 6, kumbuka njia ambazo Danieli, Shadraki, Meshaki, na Abednego walivyoshinikizwa kufanya mambo waliyojua hayakuwa sahihi. Ni kwa jinsi gani walijibu hali hizi? (ona Danieli 1:10–13; 3:15–18; 6:10). Matokeo ya imani yao yalikuwa nini? Unajifunza nini kutokana na uzoefu huu ambacho kinaweza kukusaidia wewe kumwamini Bwana wakati unakabiliwa na upinzani? Pia zingatia maswali yafuatayo:
-
Ni lini umehisi kushinikizwa kufanya kitu ulichojua kuwa ni makosa? Je, ni kwa jinsi gani Bwana amekubariki kwa kushika amri Zake?
-
Itakuwaje ikiwa imani yako haiongozi kwenye miujiza unayotafuta? (ona, kwa mfano, Alma 14:8–13). Kulingana na yale uliyosoma katika Danieli 3:13–18, unafikiri Shadraka, Meshaki na Abednego wangejibu vipi swali hili? Je, mfano wao unawezaje kuleta matokeo ya jinsi unavyoyakabili majaribu ya imani yako?
-
Ni kwa jinsi gani chaguzi zako za haki zinaweza kuwaongoza wengine kwenye imani kubwa katika Bwana? (ona Danieli 2:47; 3:28–29). Tafakari athari ambazo chaguzi zako zinaweza kuwa kwa wengine.
Ona pia Dieter F. Uchtdorf, “Usiogope, Amini Tu,” Liahona, Nov. 2015, 76-79.
Jaribu kumhusisha kila mmoja Mwokozi “anawaalika … wote waje kwake na wapokee wema wake” (2 Nefi 26:33) Kama unaifundisha familia yako au darasa, tafakari njia unazoweza kumpa kila mmoja fursa ya kushiriki kwa njia fulani. Kwa mfano, ungeweza kumpa kila mtu kifungu cha maandiko, sehemu ya ujumbe wa mkutano mkuu, au mstari kutoka kwenye wimbo ili kutafakari na kutoa maoni juu yake. Usimshinikize yeyote kushiriki, lakini uwape fursa.
Shadraka, Meshaki, na Abednego katika Tanuru La Moto Mkali, na William Maughan
Danieli 2
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani.
Kupitia ufunuo, Danieli aliona kwamba ndoto ya Nebukadreza ilitabiri falme za ulimwengu zijazo, pamoja na ufalme wa Mungu wa siku za usoni, ambao “hautaangamizwa kamwe” (Daniel 2:44). Kanisa ni ufalme ule ambao ulitabiriwa katika siku za mwisho,” Mzee D.Todd Christofferson alifundisha, “usioumbwa na binadamu, bali uliowekwa na Mungu wa Mbinguni na unasonga mbele kama jiwe lililochongwa kutoka mlimani bila mikono kujaza dunia” (“Kwa Nini Kanisa,” Liahona, Nov. 111). Fikiria juu ya ufalme wa Mungu wa siku za mwisho unaposoma maelezo ya jiwe katika Danieli 2:34–35, 44–45. Jukumu lako ni lipi katika kusaidia unabii huu kutimia?
Ona pia “Sikilizeni, Mataifa!,” Nyimbo za Dini, na. 152; “God Gave Them Knowledge” (video), ChurchofJesusChrist.org.
God Gave Them Knowledge
Danieli 2:1–30
Kupokea ufunuo kunahitaji maandalizi ya kiroho.
Unapopitia tena Danieli 2:1–15, fikiria jinsi ambavyo ungehisi kama ungejikuta katika nafasi ya Danieli. Danieli alifanya nini? (ona Danieli 2:16–18). Je, tunaweza kujifunza nini kutoka katika Danieli 1:17 kuhusu jinsi Mungu alivyomwandaa Danieli? Je, tunaweza kujifunza nini kutokana na maneno na vitendo vya Danieli baada ya kupokea msaada wa Bwana? (ona Danieli 2:19–30).
Danieli 7:13–14
Yesu Kristo ndiye Mwana wa Baba wa Milele.
Wakati wa huduma ya Mwokozi duniani, Wayahudi wengi walifikiria jina “Mwana wa Mtu” kutoka Danieli 7:13 lilimaanisha Masiya ajaye. Unajifunza nini kuhusu Masiya kutoka Danieli 7:13–14? ( ona pia Musa 6:57).
Mwokozi mara nyingi alijitambulisha kama “Mwana wa Mtu.” Fikiria kurejelea baadhi ya mifano: Mathayo 25:31; Marko 9:31; 10:45. Anafundisha nini kuhusu Yeye mwenyewe katika mistari hii? Katika Marko 14:61–64, Yesu alitumia jina hili katika siku ya mwisho ya maisha Yake duniani. Tazama majibu kutoka kwa watu waliosikia tamko Lake. Ni kwa jinsi gani unabii wa Danieli kuhusu Mwana wa Mtu unagusa hisia zako kuhusu kile kilichomtokea Yeye katika Marko 15?
Kama vile Yesu alivyochukiwa kwa kutangaza kwamba Yeye alikuwa “Mwana wa Mtu,” unaweza pia kukabiliana na mateso kwa kutangaza ukweli. Linganisha unabii katika Danieli 7:13–14 na ahadi katika Mafundisho na Maagano 121:29, 46.
Ona pia Mafundisho na Maagano 49:6; Mwongozo wa Maandiko, “Mwana wa Mtu,” Maktaba ya Injili.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Danieli 1; 3; 6
Yesu atanisaidia kufanya kilicho chema hata wakati inapokuwa vigumu.
-
Ili kuwasaidia watoto wako kujifunza hadithi za kuvutia kutoka katika kitabu cha Danieli, ungeweza kupata picha za matukio hayo katika Danieli 1, 3, na 6 (ona ukurasa wa shughuli ya wiki hii au kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 23, 25, 26). Kisha ungeweza kuweka picha zikiangalia chini na mwalike mtoto kugeuza moja na kuzungumza kuhusu hadithi inayowakilishwa nayo. (Kwa msaada, ona “Danieli na Rafiki Zake,” “Shadraka, Meshaki, na Abednego,” na “Danieli na Tundu la Simba” katika Hadithi za Agano la Kale, 54–56, 160–62, 163–65.)
1:39Daniel and His Friends
1:39Shadrach, Meshach, and Abed-nego
1:45Daniel and the Lions’ Den
-
Wasaidie watoto wako wafikirie hali ambapo wanaweza kushinikizwa kufanya uchaguzi usio sahihi, kama vile Danieli na rafiki zake walivyokuwa katika Danieli 1, 3, na 6. Shirikianeni jinsi mlivyobarikiwa kwa kufanya uchaguzi sahihi hata wakati ilipokuwa vigumu. Mngeweza pia kuimba pamoja wimbo unaohusiana na mada hii, kama vile “Chagua Jema” (Nyimbo za Dini, na. 135).
Kuamini Hekima ya Neno
Danieli 1:1–17
Baba wa Mbinguni anataka niutunze mwili wangu.
-
Kusoma hadithi kuhusu Danieli na rafiki zake kukataa nyama na divai ya mfalme kunaweza kutia msukumo wa mazungumzo kuhusu sheria ya afya ambayo Baba wa Mbinguni ametupa leo ( ona Mafundisho na Maagano 89). Pengine ungeweza kutafuta baraka ambazo Danieli na rafiki zake walipokea na kuzilinganisha na baraka zilizoahidiwa katika Neno la Hekima (ona Danieli 1:15–17 na Mafundisho na Maagano 89:18–21).
Danieli 2
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani.
-
Unaposoma Danieli 2:31–35, 44–45 pamoja na watoto wako, ungeweza kuwaalika wachore picha ya ndoto ya Nebukadreza. Wasaidie kuelewa jiwe katika ndoto huwakilisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Je, tunajifunza nini kuhusu Kanisa kutoka kwenye ndoto hii? Watoto wako wangeweza kutaja baadhi ya mambo aliyofanya Baba wa Mbinguni ili kuanzisha Kanisa Lake katika siku hizi za mwisho. Ikiwa wanahitaji msaada, ungeweza kuonyesha picha za matukio katika Urejesho wa Kanisa (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 90–95).
Danieli 6
Baba wa Mbinguni ananitaka nisali mara kwa mara.
-
Kwa nini kuomba kwa Baba wa Mbinguni ni muhimu sana kwa Danieli? Pengine wewe na watoto wako mngeweza kuzungumza kuhusu swali hilo mnaposoma Danieli 6 pamoja. Kisha mngeweza kuwaambiana kwa nini kusali ni muhimu kwenu. Watoto wako wangeweza kufurahia kuchora picha zao wenyewe wakisali katika hali mbalimbali. Wangeweza kutumia michoro yao kufundishana kwamba tunaweza kuomba kwa Baba wa Mbinguni bila kujali mahali tulipo au kile tunachohitaji.
Kwa ziada, ona toleo la mwezi huu la jarida la Rafiki .