“Desemba 29–Januari 4. Agano la Kwanza la Yesu Kristo: Utangulizi wa Agano la Kale,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Agano la Kale 2026 (2026)
“Utangulizi wa Agano la Kale,” Njoo, Unifuate: 2026
Desemba 29–Januari 4: Agano la Kwanza la Yesu Kristo
Utangulizi wa Agano la Kale
Unapotafakari kujifunza Agano la Kale mwaka huu, je, unajisikiaje? Mwenye shauku? Usiye na uhakika? Mwenye kuogopa? Hisia hizi zote zinaeleweka. Agano la Kale ni moja ya mikusanyo ya zamani sana ya maandishi ulimwenguni, na hicho kinaweza kufanya vyote viwili kusisimua na kutisha. Maandishi haya yanatokana na utamaduni wa kale ambao unaweza kuonekana wa kigeni na nyakati zingine ya ajabu au hata kuwa ya wasiwasi sana. Na bado katika maandishi haya tunaona watu wakiwa na uzoefu ambao unaonekana wa kawaida. Tunatambua dhima za injili ambazo zinashuhudia uungu wa Yesu Kristo na injili Yake. Ndiyo, watu kama Ibrahimu, Sara, Hana, na Danieli waliishi maisha ambayo, katika njia fulani, yalikuwa tofauti sana na ya kwetu. Lakini wao pia walipatwa na shangwe ya kifamilia na kutoelewana kifamilia, nyakati za imani na nyakati za mashaka, na mafanikio na kushindwa—kama sisi sote tufanyavyo. Muhimu zaidi, wao walitumia imani, walitubu, walifanya maagano, na kupata uzoefu wa kiroho, na kamwe hawakukata tamaa katika ahadi ya Mwokozi. Tunapojifunza jinsi Mungu alivyotembea katika maisha yao, pia tunamwona Yeye katika maisha yetu, na tunasema kwa mtunga zaburi: “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na nuru ya njia yangu. … Kwa hiyo mtumishi wako analipenda” (Zaburi 119:105, 140).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Agano la Kale linashuhudia juu ya Yesu Kristo
Njia moja ya kupata lishe nzuri ya kiroho katika Agano la Kale ni kutafuta Mkate wa Uzima, Yesu Kristo (ona Yohana 6:48). Kwa mfano, ni kwa jinsi gani unaona Mwokozi katika yafuatayo?
-
Mana (Kutoka 16:4, 11–15; Yohana 6:35)
-
Mwanakondoo wa dhabihu (Kutoka 12:3–5; Yohana 1:29)
-
Nyoka wa shaba (Hesabu 21:4–10; Yohana 3:14–15).
-
Yona (Yona 1:4–17; Mathayo 12:38–41)
Mifano hii inakufundisha nini kuhusu Yeye? Ni marejeo gani mengine kwa Yesu Kristo katika Agano la Kale ambayo tayari unayafahamu?
Katika ujumbe wake “Yesu Kristo Ndiye Hazina,” Mzee Dale G. Renlund alituhimiza “tumkumbuke na daima tufokasi kwa Yesu Kristo” (Liahona, Nov. 2023, 98). Fikiria kusoma ujumbe wake, ukitafuta vitu unavyoweza kufanya ili kumpata Yesu Kristo si tu katika Agano la Kale bali pia katika maisha yako.
Ona pia “Aina au Ishara za Kristo” katika Mwongozo wa Maandiko, “Yesu Kristo,” Maktaba ya Injili; “Seek the Lord Early,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 108.
Tafuta Ishara ambazo hushuhudia juu ya Yesu Kristo. Bwana alimfundisha Adamu, “Vitu vyote vina mifano yao, na vitu vyote vimeumbwa na vimefanywa ili kunishuhudia Mimi” (Musa 6:63). Iwe unajifunza au unafundisha, kufokasi kwa Yesu Kristo kunaweza kukusaidia kupata maana katika maandiko na kuongeza upendo wako Kwake na imani katika Yeye. (Ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 7.)
Yesu Kristo ni Yehova katika Agano la Kale.
Baada ya hapo, Baba alimtambulisha Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo, awe Mwokozi na Mkombozi wetu na alitupa amri ya ‘kumsikiliza Yeye.’ Kutokana na maelekezo haya tunahitimisha kwamba taarifa za maandiko yaliyotamkwa na “Mungu” au “Bwana” daima yote ni maneno ya Yehova, Bwana wetu aliyefufuka, Yesu Kristo” (”Mafundisho ya Yesu Kristo,” Liahona, Mei 2023, 102).
Mafundisho ya Yesu Kristo
Wakati viongozi wa Wayahudi walipompa changamoto Yesu kuhusu utambulisho Wake, Yeye alitamka, “Kabla ya Ibrahimu kuwa, mimi nipo.” Maneno haya yaliwashtua watu waliomsikia Yesu, na walikuwa tayari kumpiga mawe (ona Yohana 8:58–59). Fikiria kusoma Kutoka 3:13–15; 6:3–5 kuona ni kwa nini Wayahudi wengine walikasirishwa sana na kile Yesu alichosema.
Kwa nini ni muhimu kwako kujua kwamba Yesu Kristo ndiye Yehova?
Bwana alirejesha “vitu vingi vilivyo wazi na vyenye thamani” kupitia Joseph Smith.
Katika ono, Bwana alimwonyesha Nefi ujio wa Biblia, akielezea kwamba “vitu vingi vilivyo wazi na vyenye thamani” vingetolewa kutoka kwayo. Fikiria kusoma 1 Nefi 13:21–29, 38–42, ukitafuta jinsi Bwana alivyopanga “kujulisha vitu vilivyo wazi na vyenye thamani.” Kulingana na 2 Nefi 3:12, Ni kwa jinsi gani Biblia na Kitabu cha Mormoni hufanya kazi pamoja?
Unapojifunza Agano la Kale mwaka huu, pia utajifunza baadhi ya “vitabu vingine” Nefi aliviona kabla. Hivi vinajumuisha:
-
Kitabu cha Musa, sehemu ya tafsiri ya Joseph Smith ya Biblia Inarejesha kweli na maelezo ambayo hayapatikani katika maandishi ya sasa ya Mwanzo 1–6.
-
Kitabu cha Ibrahimu, ambacho kilifunuliwa kwa Joseph Smith alipochunguza mafunjo ya kale ya Kimisri (ona Mada na Maswali, “Kitabu cha Ibrahimu,” Maktaba ya Injili).
-
Vifungu mbalimbali kutoka katika Joseph Smith Tafsiri, ambavyo vinaonekana katika tanbihi, kiambatisho cha Biblia, na Mwongozo wa Maandiko.
Hapa kuna baadhi ya mifano ya maelezo ya Agano la Kale yaliyorejeshwa kupitia Joseph Smith: Mji wa Henoko wa Sayuni (Musa 7:18–19), ono la Ibrahimu la baraza la mbinguni (Ibrahimu 3:22–28), na huduma ya Melkizedeki (Joseph Smith Tafsiri, Mwanzo 14:25–40). Kwa nini hadithi hizi ni “wazi na za thamani” kwako?
Adamu na Hawa,Wakitoa Dhabihu, na Keith Larson
Agano la Kale hunisaidia kuelewa uhusiano wangu wa kiagano na Mungu.
Agano la Kale ni hadithi ya Mungu akitafuta kutufanya “tunu ya kipekee” Yake kwa agano (Kutoka 19:5). Kwa sababu hiyo, njia nzuri ya kujiandaa kusoma Agano la Kale ni kujifunza kuhusu maagano—hasa agano lisilo na mwisho ambalo Mungu alilitoa kwa manabii wa kale kama Ibrahimu, Isaka, Yakoba, na vizazi vyao. Na njia kuu ya kujifunza kuhusu maagano ni kujifunza ujumbe wa Rais Russell M. Nelson “Agano la Milele” (Liahona, Oktoba 2022, 4–11).
Unaposoma, jiulize mwenyewe: Kwa nini maagano ni muhimu kwangu? Ni “aina gani maalumu ya upendo na rehema” ninayopokea kutoka kwa Mungu ninaposhika maagano yangu Naye? Unaposoma Agano la Kale mwaka huu, kuwa unaangalia mambo ambayo Mungu anataka kukufundisha kuhusu uhusiano wako wa agano na Yeye.
Ona pia Yeremia 31:31-34
Kwa mawazo zaidi, ona matoleo ya mwezi huu ya majarida ya Liahona na Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana .
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Ninaweza kujifunza juu ya Yesu Kristo katika Agano la Kale.
-
Maneno na utamaduni wa Agano la Kale yanaweza kuwa magumu kwa watoto kuelewa, lakini unaweza kuwasaidia kumwona Yesu Kristo katika ishara na hadithi. Pengine wewe na watoto wako mngeweza kutazama picha hapa chini, Nabii Isaya Anatabiri Kuzaliwa kwa Kristo. Acha watoto wako waoneshe kwa uwazi maelezo wanayoyaona. Vuta usikivu wao, hususani, kwa mtoto Yesu. Kisha ungeweza kusoma pamoja nao kile Isaya aliandika kuhusu kuzaliwa kwa Mwokozi katika Isaya 7:14; 9:6. Shiriki na watoto wako jinsi unavyohisi kuhusu kumtafuta Mwokozi katika Agano la Kale mwaka huu.
Isaya Anaandika kuhusu Kuzaliwa kwa Kristo (Nabii Isaya Akitabiri Kuzaliwa kwa Kristo), na Harry Anderson
-
Wewe na watoto wako mngeweza pia kusoma Zaburi 23 au Isaya 53:3–9 na kutafuta maneno ambayo yanakukumbusha juu ya Yesu Kristo. Je, maneno haya yanatufundisha nini kuhusu maisha yake na Upatanisho Wake?
Baba wa Mbinguni anataka kufanya maagano na mimi.
-
Maagano ni dhima kuu katika Agano la Kale. Ili kutambulisha dhima hii kwa watoto wako, ungeweza kuzungumza nao kuhusu ahadi wanazofanya na kuzitunza pamoja na familia au marafiki na kwa nini kutunza ahadi hizi ni muhimu. Kisha ungeweza kuangalia picha ya ubatizo na kuzungumza kuhusu ahadi, au agano, tunapofanya na Mungu wakati tunapobatizwa (ona Mosia 18:10, 13). Ungeweza pia kuonyesha picha ya hekalu na kushiriki hisia zako kuhusu maagano tunayofanya huko.
-
Ukurasa wa shughuli ya wiki hii ungeweza kuwasaidia watoto wako wawe na shauku ya kufanya na kushika maagano na Baba wa Mbinguni. Mngeweza pia kuimba wimbo kuhusu kufanya maagano, kama vile “When I Am Baptized” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 103).
Yesu Kristo ni Yehova katika Agano la Kale.
-
Je, watoto wako wanamjua yeyote anayejulikana kwa majina tofauti katika mazingira tofauti? Pengine mzazi au mwalimu ametajwa kitofauti kazini, nyumbani, na kanisani. Zungumza kuhusu majina hayo; kisha someni Kutoka 6:3 pamoja na waalike watoto wako watafute majina ambayo Yesu Kristo aliyajua kabla hajazaliwa (ona pia Joseph Smith Tafsiri katika tanbihic).
Kwa ajili ya mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la jarida la Rafiki .